Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mollel kula sahani moja na waganga

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel (kulia) akipata maelekezo katika moja ya mabanda ya kutoa huduma katika kilele Cha Maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa yasiyoambukiza kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja leo Novemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel amewaasa waganga wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia maeneo yao kwa uadilifu, huku akisema watawajibika kwa tatizo lolote litakalotokea katika maeneo endapo uzembe ukigundulika.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amewataka waganga wakuu wa Mikoa na wilaya kuwa waadilifu, akiwaonya kuwa watawajibika kwa uzembe wowote utakaobainika iwapo kutatokea tatizo.

 Akizungumza leo Novemba 18, 2023 katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza kitaifa, katika viwanja vya Mnazimmoja jijini hapa, Dk Mollel amesema Serikali imejitahidi kuimarisha miundombinu ya afya nchini hivyo asingependa kuona uzembe katika utoaji huduma.

"Niwaambie waganga wakuu katika mikoa na wilaya, kwamba ikitokea tatizo kwenye eneo lako, utakuwa mtuhumiwa namba moja kabla hatujamshulikia mtumishi ambaye amefanya kosa," amesema Dk Mollel.

Aidha ameeleza kutoridhishwa na mabaraza ya manesi na madaktari katika usimamizi wa taaluma hiyo akisema yanapaswa kusimamia maadili na miiko ya taaluma hiyo ipasavyo.

"Hatutaki kusikia wanaenda kwenye tukio lililotokea, wanatakiwa wafike kule chini kuboresha maadili, miiko na huduma za afya kabla tukio baya halijatokea, tunahitaji watu wote wawe na maadili ya kiafya," amesema Dk Mollel.

Dk Mollel amewataka viongozi hao kushughulikia changamoto katika ngazi za chini kwani katika ngazi hiyo kiwango cha huduma si cha kuridhisha kwani bado Watanzania walalamika.

"Leo hii kwenye sekta ya afya, daktari akikosea tu kidogo kuna mtu anapoteza maisha au kupata ulemavu, maana yake afya ni suala la ulinzi na usalama. Niwaombe Wakuu wa Mikoa na Wilaya walifanya suala la afya kuwa ni mjadala katika vikao vya kamati za ulinzi na usalama," amesema.

Kwa upande wake Msimamizi wa Programu ya Magonjwa yasiyoambukiza, Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini, Dk Alphoncine Nanai amesema watu wengi hawafahamu kwamba wanaishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutokana na utamaduni wa kutokupima afya zao mara kwa mara.

Akitolea mfano shinikizo la damu amesema takwimu zinaonyesha idadi kubwa ya watu wana tatizo hilo bila kujua ikiwa ni matokeo ya kutokupima afya.

"Tuligundua kuwa katika Kila watu wanne, mmoja ana shinikizo la damu na takriban asilimia 90 ya wale tuliokuta na shinikizo la damu, hawajui kwamba walikuwa na tatizo hilo," amesema Dk Nanai.

Amesema zaidi ya asilimia 65 ya magonjwa yasiyoambukiza hayasababishwi na vigezo vya afya peke yake isipokuwa mtindo wa maisha wa kawaida, ikiwemo vyakula, vinywaji, mazoezi na elimu.

Pia ameongeza kuwa shirika hilo linaendelea kusaidia masuala ya walemavu, utengemavu na kupunguza sukari.