Dk Mpango kumwakilisha Samia Ufaransa
Muktasari:
- Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kimataifa wa "Kizazi cha Usawa" utakaofanyika Paris, Ufaransa Juni 30 hadi Julai 2, 2021.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kimataifa wa "Kizazi cha Usawa" utakaofanyika Paris, Ufaransa Juni 30 hadi Julai 2, 2021.
Mkutano huo una lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kupunguza pengo kati ya wanaume na wanawake na kuleta usawa kwa kuwainua wanawake katika nyanja zote hasa za kiuchumi.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu Juni 28, 2021 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema mkutano huo unafanyika miaka 26 baada ya mkutano wa Beijing ambao amesema haujafikia malengo.
Amesema Rais Samia amejizatiti kufanyia kazi suala la haki za wanawake kiuchumi ikiwa ni moja kati ya mambo sita ambayo viongozi wa mataifa mbalimbali wamejipanga kuyafanya.
"Makamu wa Rais ataondoka leo jioni kumwakilisha Rais Samia katika mkutano huo ambao utafanyika kuanzia Juni 30. Tayari Rais amejizatiti kufanyia kazi suala la haki za wanawake kiuchumi hadi ifikapo mwaka 2026," amesema Balozi Mulamula.
Katika kutekeleza hilo, Serikali itahakikisha ifikapo mwaka 2026 wanawake wanamiliki ardhi, inapunguza pengo la kijinsia na kuongeza idadi ya kampuni zinazomilikiwa na wanawake.
Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini, Frederick Clavier amesema kongamano hilo la kihistoria linafanyika baada ya maazimio ya mkutano wa Beijing kushindwa kupunguza pengo la kijinsia.
Amesema Ufaransa na Mexico wameshirikiana kubuni na kuandaa kongamano hilo kwa lengo la kufikia usawa wa kijinsia ifikapo mwaka 2030.
"Yapo mafanikio katika miaka hiyo 26 ya mkutano wa Beijing lakini zinahitajika juhudi zaidi ili kuhakikisha Kuna usawa wa kijinsia," amesema Balozi Clavier na kuongeza kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa na wanapasa kupaza sauti katika hili.