Dk Mwigulu aja kivingine kwa asasi za kiraia

Muktasari:

  • Baada ya kuibuka mjadala mkali kutokana na kauli aliyoitoa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali haina nia ya kuchukua fedha za Asasi za Kiraia (Azaki) kutoka kwa nchi wa hisani ila ufadhili huo unapaswa kuendana na malengo ya nchi.

Dar es Salaam. Baada ya kuibuka mjadala mkali kutokana na kauli aliyoitoa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali haina nia ya kuchukua fedha za Asasi za Kiraia (Azaki) kutoka kwa nchi wa hisani ila ufadhili huo unapaswa kuendana na malengo ya nchi.

Mwigulu ametumia ukurasa wake wa Twitter kutoa ufafanuzi huo kama alivyofanya juzi alipotoa kauli iliyoibua utata na kupokelewa kwa hisia tofauti na wana Azaki.

Kauli yake ilisomeka, “Leo kupitia kikao tulichofanya kwa njia ya mtandao, nimeliomba Shirika la USAID kuelekeza kiasi cha msaada wa Sh3 trilioni inazotaka kuipatia Tanzania kupitia asasi za kiraia, zielekezwe kwenye miradi ya kimkakati ya Serikali ya Awamu ya Sita. Tutazisimamia vizuri,”.

Kauli hiyo ilionekana kuwashutua viongozi wa asasi za kiraia akiwemo Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa aliyeeleza kwa kuwa kazi zinazofanywa na asasi za kiraia hazitoki nje ya mipango ya Serikali na asasi zinawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.

“Alichotakiwa kufanya waziri ni kusisitiza asasi za kiraia kufanya kazi zake kwa kufuata hiyo miradi ya Serikali, lakini si kuzuia fedha zisielekezwe upande huo, asasi zina umuhimu wake na zinahitaji fedha ili zijiendeshe na kuwafikia kwa ukaribu zaidi wananchi kupitia miradi,” alisema Olengurumwa.

Katika ufafanuzi wake aliutoa jana, Mwigulu alisema akiwa waziri mwenye dhamana ya fedha ana wajibu wa kuwaeleza washirika wa maendeleo kuhusu mifumo ya bajeti huku akiwasihi kuongeza fedha kwa asasi za kiraia.

“Ndicho nilifanya katika mazungumzo na USAID. Hatuna nia ya kuzichukua fedha zinazokwenda kwa Azaki isipokuwa ufadhili uendane na malengo yetu. Fedha ambazo washirika wa maendeleo wanazipeleka moja kwa moja kwa Azaki zinasimamiwa na menejimenti, bodi ya Azaki kwa mujibu wa sheria ya NGO.

“Fedha zinazotumiwa na Serikali zinapaswa kufuata sheria ya bajeti na sheria za fedha za umma. Hatujataka fedha za Azaki zije hazina”.

Kupitia andiko hilo, Mwigulu aliziomba Azaki kuainisha shughuli zao na malengo ya dira ya maendeleo ya Taifa 2025 na mpango wa maendeleo wa miaka mitano ili Serikali, sekta binafsi na jamii kufanya kazi kwa lengo moja katika kuleta maendeleo.

Akizungumzia ufafanuzi wa waziri, Olengurumwa alisema hoja yake ni sahihi kwa sababu asasi za kiraia kazi zinazofanya zinaendana na ziko ndani ya miradi au mikakati ya maendeleo hapa nchini.

“Ninachoona waziri amekazia na kusisitiza iendelee kuwa hivyo, tumelipokea hilo na hatuna tatizo lolote. Tufahamu licha kuwa tunafanya kazi kwa mujibu wa miradi na mikakati mbalimbali ya Serikali, haimaanishi kuwa Azaki zinazuiwa kuwa na miradi mingine ambayo ipo kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema.

Alisema kuoanisha kazi za Azaki na miradi ya maendeleo kunawezesha mchango wa asasi za kiraia uwezo kutambulika na kuwekwa kwenye mipango na sera mbalimbali za Serikali.