Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu: Serikali itaimarisha mifumo ili vijana wapate mitaji

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akizingumza wakati wa kilele cha fainali ya shindano la vijana uchumi challenge, lenye lengo la kuibua mawazo bunifu kutoka kwa vijana.

Muktasari:

  • Dirisha la shindano hilo lilifunguliwa Aprili 2026 na kufungwa Mei 2026, ambapo jumla ya mawazo bunifu 7852 ya vijana kutoka Tanzania bara na visiwani, yalipokewa na Wizara ya Maendeleo ya Vijana na kuchujwa hadi kubaki 10.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inakusudia kupeleka sheria bungeni ambayo itahalalisha dhamana zinazohamishika ili ziweze kutumika katika kupata mkopo kwa wananchi.

Pia, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kupata mitaji kwa kuimarisha mfumo jumuishi na rafiki utakaowapa fursa bila kujali umbali wa kijiografia.

Dk Mwigulu amesema hayo leo Jumapili, Julai 5, 2026 wakati wa kilele cha fainali ya shindano la Vijana Uchumi Challenge, iliyokwenda sambamba na utoaji wa zawadi kwa mshindi wa kwanza hadi watatu, ambao wameshinda mawazo ubunifu ya utatuzi wa changamoto katika jamii.

 “Kundi la vijana ni kundi kubwa na muhimu sana na hii ndio sababu Serikali imeamua kuwekeza kwa vijana na kwamba imeweka msisitizo katika kutoa elimu na ujuzi unaoendana na fursa, ajira na soko  ili kuimarisha uchumi” alisema na kuongeza

“Lakini kwa vijana wetu, wahitimu wa ngazi mbalimbali, tunakusudia  kuanzisha cheti kitakachotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), ili kiweze kutumika kama dhamana kwa ajili vijana  kuchukulia mkopo kwa ajili ya kufanyia shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akizingumza wakati wa kilele cha fainali ya shindano la vijana uchumi challenge, lenye lengo la kuibua mawazo bunifu kutoka kwa vijana.

Amesema pia itaweka kipaumbele katika kupatia ufumbuzi wa changamoto za vijana sambamba na kuwahakikisha kuwa inawashirikisha katika mpango wa kuwatafutia fursa mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema Serikali inaendelea kuboresha na kuratibu kuwezesha mikopo yenye masharti nafuu na kusimamia kikamilifu mafunzo na programu kwa vijana.

Awali, akifafanua kuhusu shindano hilo,  Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Jennifer Omolo amesema shindano hilo lilianzishwa Aprili 2026 na kufungwa Mei 2026 na limekuwa jukwaa muhimu na limetoa nafasi ya kuibua fikra na ubunifu wa vijana, kujenga ujasiri, na kuonyesha kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kubuni suluhisho za changamoto za kiuchumi na kijamii.

“Serikali inataka vijana wawe sehemu halisi ya maendeleo na kushiriki kikamilifu na si watazamaji tu,”amesema Olomo

Mshindi wa Shindano la Vijana Uchumi Challenge, Geofrey Sanga, ambaye ni Mtaalamu wa kilimo na Mifugo, akizingumza na waandishi wa habari. Hata hivyo Sanga amejinyakulia zawadi ya pesa taslimu Sh50milioni. Picha na Hadija Jumanne

Aidha ameeleza kuwa kabla ya mchakato wa kuwapata washindi watatu, walipokea mawazo bunifu 7,852 kutoka vijana wa Tanzania bara na visiwani na kuchujwa hadi kufikia mawazo 100 ambayo vijana hao walipatiwa mafunzo na kusisitiza kuwa Serikali itaunda mfumo wa kuwafuatilia baada ya shindano.

“Ili mawazo yao yasibaki kwenye makabati wataunganishwa na fursa, taasisi za fedha na viongozi ili mawazo yaweze kuleta tija kwa jamii na kusaidia vijana wengine.” Ameongeza Olomo.

Amesema shindano hilo lenye kauli mbiu ya ‘Wana tunafikiri, Taifa linasonga’ ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuwashirikisha vijana kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Mwenyekiti wa majaji wa shindano hilo, Profesa Neema Mori, amesema vijana 100 walichujwa na kupelekwa katika kambi ya mafunzo ilifanyikia katika chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha.

“Tulikutana na vijana 100, ambao tuliweza kukaa nao na kuwasikiliza kuwashauri na kisha kuwachuja na kupata vijana30 na kwa kiasi kikubwa hatukuwa sehemu ya kujaji bali ilikuwa ni kujifunza kutoka kwao kuhusu mawazo bunifu waliyoyawasilisha” amesema Profesa Mori

Profesa Mori amesema katika kuwasikiliza washiriki hao kuna maeneo matatu wameona yanapaswa kufanyiwa kazi ambapo wamebaini vijana wana uwezo mkubwa wa kutatua changamoto zilizopo, lakini wanaunga mkono Serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo na wana uwezo wa kufikiri na kuwasilisha mawazo yao kwa kuyahusisha na dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema shindani hilo ni daraja la kuwaunganisha vijana katika kukuza mawazo bunifu.

“Mbali na shindano hili, wizara itaendelea kushirikiana na vijana na pia tutaendelea kushirikiana na vijana hao 100 ambao tuliwapa mafunzo kule Kibaha” amesema Nanauka.

Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza ni mtaalamu wa kilimo na mifugo kutoka Dodoma, Geofrey Sanga ambaye ameshinda Sh50 milioni kupitia wazo lake la uhamishaji viini tete kwa ng’ombe (kuboresha mbegu bora za ng’ombe wa maziwa).

Mshindi wa pili ni Jacob Mugisha ambaye alipata Sh30 milioni kupitia wazo lake la suluhishi jumuishi la ufugaji wa samaki na huku Robert Mwalonge, akipata Sh20 milioni kupitia wazo la kutengeneza vifungashio kwa kutumia mabaki ya matunda na vyakula.

Hata hivyo Dk Mwigulu amesema mshindi wa kwanza hadi wa tatu, atawaongezea Sh5 milioni kila mmoja, huku mshindi wa nne hadi wa 10, kila mmoja atamuongezea Sh2 milioni.

Akizungumzia ushindi huo, Sanga amesema anaamini Serikali italichukua wazo lake na kulifanyia kazi.