Dk Mwinyi: SMZ inazishughulikia changamoto za uwekezaji

Friday June 24 2022
mwinyipiic
By Jesse Mikofu

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali imejipanga kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu, bandari, umeme na huduma ili kuvutia wawekezaji wenye mitaji mikubwa kuja kuwekeza Zanzibar.

Alitoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 23, 2022 wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Wafanyabiashara wa Ulaya kwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji kupitia Mamlaka ya Kukuza Uchumi Zanzibar (Zipa) hafla iliyofanyika hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeelelekeza nguvu zake kubwa katika kukuza uwekezaji na kuimarisha sekta ya utalii ambapo hasa ikizingatiwa kwamba maeneo hayo yaliathiriwa na Uviko-19.

“Kwa kipindi cha miezi 19 kati ya Novemba 2020 hadi Mei 2022, jumla ya miradi 136 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 1.4  imewekezwa Zanzibar ambayo inatarajiwa kutoa ajira 9,000,” amesema Rais Mwinyi na kuongeza

Kwasasa tunaboresha miundombinu, badari, barabara na umeme kuweka mazingira bora ya uwekezaji,”

Alisema kwamba Zanzibar imekuwa na ushirikiano na uhusiano wa kiuchumi na biashara karne nyingi zilizopita kati yake na nchi za Ulaya na kueleza kwamba amefurahi uhusiano huo umezidi kuendelezwa ambapo wawekezaji kutoka nchi mbalimbali za Ulaya wamekuja kuwekeza Zanzibar.

Advertisement

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Zipa, Sharifu Ali Sharifu amesema hadi sasa Zanzibar imepokea zaidi ya wawekezaji 300 kutoka bara la Ulaya ambao wamesaidia kuongeza ajira nchini.

Naye Balozi wa Umoja wa nchi za Ulaya nchini Tanzania,  Manfredo Fanti alisema kwamba nchi za Ulaya zimevutiwa na sera na mipango ya Serikali ya Zanzibar katika kukuza uwekezaji pamoja na kuitangaza sekta ya utalii.

Balozi wa Uholanzi Wiebe de Boer  alimpongeza Rais Dk Mwinyi kwa juhudi anazoendelea kuchukua katika kuitangaza Zanzibar duniani kote huku akieleza kwamba katika kipindi kifupi tokea kuingia madarakani ameongeza imani kwa wawekezaji kuja kuekeza na kuleta mitaji yao hapa Zanzibar


Advertisement