Dk Nchimbi, wanajamii wamlilia Thadei Ole Mushi
Thadei Mushi, maarufu Thadei Ole Mushi enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Waeleza Thadei Ole Mushi alivyoiteka mitandao ya kijamii kwa uchambuzi na uchangiaji wa mada mbalimbali, hususani za kisiasa na jinsi kifo chake kilivyowagusa wengi.
Moshi/Dar. Wanasiasa na wanajamii wameelezea namna walivyoguswa na kifo cha Thadei Mushi, maarufu Thadei Ole Mushi, aliyeiteka mitandao ya kijamii kwa uchambuzi na uchangiaji wa mada mbalimbali, hususani za kisiasa.
Ole Mushi, ambaye ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amefariki dunia jana Februari 4, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Victor Tesha, rafiki wa karibu wa familia ya Ole Mushi, akizungumza na Mwananchi Digital leo Februari 5, 2024 amesema kesho saa tano asubuhi kutafanyika misa na baadaye kuaga mwili wake katika Kanisa Katoliki la St Peter's Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Amesema baadaye mwili utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukisindikizwa na mkewe na ndugu wa karibu kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
"Mwili wa ndugu yetu Thadei Mushi utawasili Uwanja wa Ndege wa KIA saa 1:30 usiku,” amesema.
Tesha amesema mwili wa Ole Mushi utaenda kulala nyumbani kwao Kitandu karibu na Shule ya Msingi Chombo, wilayani Moshi.
Marehemu ni mzaliwa wa Kijiji cha Shinga, Kata ya Uru Kusini, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Tesha amesema maziko yatafanyika Jumatano, Februari 7, 2024 nyumbani kwao.
Amesema Ole Mushi ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliwahi kuhuduma katika shule mbalimbali mkoani Kilimanjaro.
Mwaka 2006-2014 alikuwa mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Masoka, mwaka 2015 -2019 alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kirimajuu.
Mwaka 2020 alikuwa mratibu elimu Kata ya Marangu Magharibi na kuanzia Oktoba 2020 mpaka alipofikwa na umauti alikuwa ofisa elimu taaluma sekondari katika Wilaya ya Hai.
CCM wamlilia
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amezungumzia kifo cha Ole Mushi akisema wakati wa uhai wake alikuwa na mchango mkubwa wa kutoa mawazo ya kukijenga chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Februari 5, 2024 Balozi Nchimbi amesema taarifa za kifo cha Ole Mushi zimewashtua na wamepata pengo kubwa kutokana na mchango wake wa kimawazo aliokuwa anautoa.
“Licha ya misimamo yake lakini kipindi cha uhai wake alikuwa na mchango mkubwa wa kimawazo na kiushauri katika chama chetu, ni pengo kubwa na tumepungukiwa,” amesema.
Amesema namna nzuri ya kuenzi mema na maono yake ni muhimu kwa makada wengi kuendelea kusaidia kukikuza chama hicho kwa kutoa mawazo.
“Tutamkumbuka daima kama mtu aliyekuwa mzalendo,” amesema Balozi Nchimbi.
Taarifa ya CCM mtandaoni
Kabla ya Dk Nchimba hajazungumza na Mwananchi, ilitolewa taarifa rasmi ya CCM kuhusu kifo cha ole Mushi iliyozua utata kutokana na kukosewa tarehe, lakini katibu mkuu huyo amekiri kuifahamu.
“Nimepigiwa simu na waandishi wengi wakiulizia suala hili, ni kweli imetolewa na CCM ila kuna makosa yametokea badala ya kuandikwa Februari 4, imeandikwa Februari 3, 2024,’’ amesema Balozi Nchimbi.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilirekebishwa na kutumwa nyingine huku ikijadiliwa kwenye mitandao ya kijamii kwa namna mbalimbali.
Baada ya kusambaa taarifa za kifo cha Ole Mushi jana Februari 4, 2024, katika ukurasa wa Instagram wa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliandika:
"Kaka, rafiki na ndugu yangu, Thadey Ole Mushi, Mungu baba yetu akupe pumziko la milele mbinguni, kizazi chetu kimepoteza mwalimu, mchambuzi na mwanajamii kijana aliyetumia maarifa na kalamu yake kutoa maoni na hisia zake katika nyanja nyingi za kijamii, kisiasa, kiuchumi.
“Maandishi yako yataishi, hakika umetuliza sisi marafiki zako, mimi na familia yangu tunatoa pole nyingi sana kwa familia yako, mke na wanao, wazazi na ndugu zako, hakika hii dunia tu wapitaji, tuonane kwenye ile asubuhi njema na iliyo kuu, nimekuwa Speechless (nimekosa maneno)... machozi yangu."
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: "Sina la kuandika itoshe kukuombea kwa Mwenyezi Mungu, mema yako yote yakufikishe kwake, nakulilia nenda kijana mwema."
Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe kwenye ukurasa wake wa Facebook aliweka picha ya Ole Mushi na kuandika: "Pumzika kwa amani, pole sana shemeji yangu, pole sana wana familia wote."
Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema katika mtandao wa X ameandika: “Natoa pole nyingi kwa mke wako na watoto na kuwatakia nguvu ya Mungu katika nyakati hizi wanapojaribu kutaka kutokukubali kuwa umelala moja kwa moja sasa.”