Dk Ndumbaro ataka elimu kwa wananchi matumizi ya Tehama

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akizungumza akifungua kikao kazi cha mafunzo ya namna ya kutumia Tehama kwenye upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wasajili wasaidizi wa watoa huduma za masaada wa kisheria jijini Arusha.
Muktasari:
Dk Ndumbaro amesema kuwa, Wizara yake imeweka vipaumbele 14 ikiwemo kuhakikisha kunakuwepo na matumizi ya Tehema katika mifumo yote ya sheria ili haki ipatikane kwa kasi na kwa gharama nafuu zaidi.
Arusha. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amewataka watoa huduma za msaada wa kisheria nchini kutoa elimu juu ya matumizi ya mifumo ya Tehama kwa wananchi kwa ajili ya upatikanaji wa haki zao kwa wakati.
Ameyasema hayo jana Oktoba 17 jijini hapa wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo ya namna ya kutumia Tehama kwenye upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wasajili wasaidizi wa watoa huduma za masaada wa kisheria.
"Tunawaomba wadau mnaohudhuria mafunzo haya mkatoe elimu hiyo kwa wananchi, kwani umefika wakati kwa vyombo vya haki kushuka katika ngazi za chini kwa wananchi kwa haraka bila usumbufu," amesema Dk Ndumbaro.
Naye Mkuu wa kitengo cha Tehama cha wizara hiyo, Gabriel Omari amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau hao ili wapate uelewa wa kutosha wa Tehama.
Amesema kuwa, Tehama imetoa mchango mkubwa ikiwa pamoja na kuwepo kwa utunzaji wa kumbukumbu sahihi za wananchi, kuweka uwazi na uwajibikaji wa utoaji huduma hususani panapokua na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Nyingine ni kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuondoa mianya ya rushwa kwenye utoaji huduma kwa kuwa hakuna mwingiliano kati ya mtoa huduma na mteja.
Naye Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha, David Lyamongi amesema kuwa, utoaji wa elimu hiyo kwa wananchi kutasaidia sana kutatua changamoto na malalamiko yaliyokuwepo kutokana na kuchelewa kupata haki zao kwa wakati.