Domino kuibeba Zanzibar kiuchumi

Domino kuibeba Zanzibar kiuchumi

Muktasari:

  •  Siku moja baada ya gazeti hili kuchapisha habari kuhusu ujenzi wa jengo la kifahari la Domino Commercial Tower mjini Unguja, Zanzibar, wananchi, wadau na wataalamu wa utalii wamesema wamepokea kwa furaha maana linaenda kubadilisha taswira ya Zanzibar katika sura ya dunia na kuwa kama Japan.


Unguja. Siku moja baada ya gazeti hili kuchapisha habari kuhusu ujenzi wa jengo la kifahari la Domino Commercial Tower mjini Unguja, Zanzibar, wananchi, wadau na wataalamu wa utalii wamesema wamepokea kwa furaha maana linaenda kubadilisha taswira ya Zanzibar katika sura ya dunia na kuwa kama Japan.

Jengo hilo lenye urefu wa mita 385 kwenda juu na ghorofa 70, linatarajiwa kujengwa katika kisiwa cha Chwapani, kilomita 15 kutoka Mji Mkongwe, Unguja katika eneo la mita za mraba 370,000.

Mdau wa utalii, Khamis Mussa alisema hatua hiyo inatokana na dhamira na utashi wa kisiasa walionao viongozi wakuu wa Taifa.

“Kama tunavyojua Zanzibar inabebwa zaidi na masuala ya utalii, kwa hiyo kuwapo kwa mradi mkubwa kama huu itaisaidia Serikali kukuza uchumi wake.

Alisema jengo hilo litakalokuwa na hoteli na maeneo mengine ya kibiashara, litaongeza idadi ya watalii kwa sababu watakuwa wamepata sehemu sahihi ya kufikia na kupumzika kutokana na hadhi yake.

Alisema iwapo ujenzi wa jengo hilo utakamilika upo uwezekano mkubwa hata siku moja itakapotokea kombe la dunia likaletwa Afrika itakuwa moja ya sehemu ambazo timu kubwa zinaweza kufikia na kuweka kambi.

Kuhusu ajira

Khamisi alisema jengo hilo litaweza kutoa ajira nyingi kwa vijana kuanzia wakati linajengwa hadi litakapokamilika, hivyo kupunguza tatizo la ajira nchini.

“Yaani ukitazama katika muktadha huo utaona jinsi mradi huu unavyoweza kubeba matumaini makubwa kwa Wazanzibari,” alisema na kuongeza:

“Tunaiona Zanzibar inaelekea kuwa kama Japan, huu ndio mwelekeo wa Taifa tunaoutaka sasa,” alisema.

Naye Shafii Seif Mohamed ambaye ni mwanafunzi wa fani ya utalii katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), alisema huenda jengo hilo likawa suluhisho la ajira kwa vijana tofauti na ilivyo sasa.

“Ajira zitaongezeka, mahitaji ya masuala ya kitalii nayo yataongezeka, kikubwa tunaomba uwe mradi wa kweli maana wakati mwingine miradi huwa inaishia kwenye makaratasi na midomoni,” alisema.

Kuufunika Mji Mkongwe

Khamis alisema Mji Mkongwe ni urithi wa dunia hivyo utaendelea kuwa kama ulivyo, bali kuwapo kwa jengo hilo litachochea zaidi na kuleta hamasa kwa wageni kuutembelea baada ya kufikia kwenye hoteli hiyo.

Kwa upande wa Ali Makame, alisema hayo ndiyo mambo waliyokuwa wakiyataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kwa kipindi cha muda mrefu.

Alisema mara nyingi viongozi wengi wamekuwa wakisema bila utekelezaji, lakini kwa sasa tunaanza kuona kaulimbiu ya Rais Hussein Mwinyi ya kwamba “Tumpe muda yajayo yanafurahisha, kweli tunaanza kuyaona’.

“Ikiwa jengo hilo litajengwa basi tutasema Rais anapita kwenye maneno yake, yajayo ni mema kwa sababu litakuwa ni jengo la aina yake na litakuwa ni moja kati ya vivutio vizuri kwa watalii na kuitangaza Zanzibar,” alisema.

Alisema Zanzibar inategemea mapato yake katika utalii kuliko hata zao kubwa la karafuu.

“Nashauri kila kinachostahili na kuonekana kinaweza kuimarisha utalii ni wajibu Serikali kukifanya ili kuongeza mapato ya Taifa na ajira kwa wananchi wake,” alisema.

Alisema ajira ni moja ya majukumu ambayo amejibebesha Rais Mwinyi. “Yalikuwa maneno yake kila alikopita wakati wa kampeni, hivyo ana wajibu wa kuhakikisha anafanya kila mbinu kuongeza ajira katika uongozi wake, kwahiyo likijengwa hata akiondoka madarakani ataacha alama isiyofutika kamwe, huku akitimiza kile alichokuwa akikisema mara kwa mara,” alisema Makame.

Hata hivyo, Makame alisema bado wanakuwa na wasiwasi maana hata uongozi uliopita uliwahi kutoa ahadi ya kujenga mji mpya kwa kuwaonyesha ramani lakini mpaka sasa hakuna kilichoendelea.

“Kuna hoteli ya Bwawani ilivunjwa tukaambiwa tunajenga mji mpya, lakini jambo hilo halikufanyika.”

Alisema kuna wakati mambo yakizungumzwa kama hayajatendwa wananchi wanakuwa hawaamini, lakini jambo hilo linawezekana kufanyika “hata zaidi ya hili lakini inategemea nia njema ya viongozi.”

Alisema hata alivyofanya Rais wa kwanza, Abeid Amani Karume kuifanya Zanzibar kuwa na majengo makubwa ya Michenzani, ulikuwa ni utashi, majengo ambayo mpaka sasa bado yanaendelea kuweka kumbukumbu nzuri ya kiongozi huyo.