Edwin Mtei bado aamini upinzani utashika dola
Muktasari:
Unapozungumzia historia ya vyama vingi nchini, huwezi kuacha kumtaja Edwin Mtei, mmoja wa waasisi wa Chadema ambacho hivi sasa kimeshika usukani kikiongoza upinzani.
Unapozungumzia historia ya vyama vingi nchini, huwezi kuacha kumtaja Edwin Mtei, mmoja wa waasisi wa Chadema ambacho hivi sasa kimeshika usukani kikiongoza upinzani.
Mtei, aliyewahi kuwa waziri wa fedha katika Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere, aliasisi chama hicho akishirikiana na hayati Bob Makani na wengine.
Pamoja na kuwa nje ya ulingo wa siasa kwa muda mrefu sasa, Mzee Mtei, ambaye pia alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na katibu mkuu wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki (EAC), bado anaamini upinzani unazidi kuimarika na utakuja kuing’oa CCM madarakani.
Anasema anaridhishwa mwenendo wa upinzani, hasa Chadema, katika kazi zake za kisiasa za kusaka kuongoza dola.
Mzee Mtei anasema chama hicho kimekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake na anajivunia vijana wa chama hicho.
“Wanafanya kazi nzuri kuendeleza mageuzi nchini kama ambayo tuliasisi, kwa sasa siwezi kuingilia lolote wanakwenda vizuri wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe,” anasema
Anaongeza kuwa “chama cha demokrasia na maendeleo, ipo siku kitashika dola na haya ndio malengo yetu, wanafanya kazi kazi nzuri na Watanzania wengi wanawaunga mkono,” anasema.
Anasema siri ya Watanzania kuendelea kukiamini chama hicho ni kwa kuwa kina sera nzuri za kutatua matatizo yao.
Mzee Mtei anasema changamoto ambazo chama hicho kimekuwa kikipitia, ndizo zinazokiongezea ukomavu na ari ya kufanya vizuri zaidi katika siasa.
“Kila chama kina changamoto, hata sisi wakati wa kuasisi chama hiki kulikuwa na changamoto nyingi lakini tuliweza kuzikabili na hadi leo chama kimeendelea kuwa hai,” anasema.
Mtei ambaye kwa sasa ana umri ya miaka 90, ni miongomwa Watanzania wanaoamini kuwepo umuhimu wa kupatikana Katiba mpya.
Anasema ndiyo itaendeleza haki na uhuru wa watu kujieleza na kufanya shughuli zao za kiuchumi bila vikwazo.
Hoja ya uwezekano wa upinzani kushika dola Mtei aliwahi kuitoa pia Julai 2014 alipohojiwa na mwananchi. wakati huo alisema wapinzani wanaweza kutwaa dola mwaka 2015 bila hata kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya sasa.
“Wapo watu wanaojidanganya kuwa Katiba ya sasa haiwezi kuwaingiza madarakani wapinzani katika uchaguzi mkuu ujao, hao wanapotoka,” alisema.
Alisema siri pekee ya wapinzani kuingia Ikulu ni kuacha ubinafsi na kuamua kumuunga mkono mgombea mmoja anayekubalika, kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kukiangusha chama tawala, CCM.
“Ipo mifano mingi ya ushirikiano wa wapinzani bila kulazimika kuunganisha vyama vyao. Kitu pekee kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni ukomavu wa kisiasa.
“Tayari hilo limeanza kule bungeni ambako tunayo Serikali ya kivuli iliyoundwa na vyama vyetu (Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi) inafanya vizuri na huu ni mfano tosha kwamba kwa umoja wa upinzani tutashinda.”
Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa “lazima tutumie mbinu inayofaa. Hapa ninasema kuna kitu kinaitwa Mtei Technique (mbinu ya Mtei). Hii ni ya kutafuta mtu makini na ambaye anafaa kati yetu, tunamsimamisha kama mgombea wetu, kisha sote tumuunge mkono.
Aliongeza, “sisi wapinzani, lazima tukae chini, tukubali kuwa sisi ni wanasiasa wazuri kuliko CCM. Tuwaambie CCM, waache kutupuuza, tuwaonyeshe kuwa tunao uwezo wa kuwaondoa madarakani.
Kuhusu vyama vya upinzani kukumbwa na migogoro mara kwa mara, Mtei alisema wakati huo kuwa wanasiasa ni binadamu, lazima watofautiane kimawazo na kimtazamo, lakini lazima wavumiliane kwa masilahi na ustawi wa vyama.
“Kamwe wasiruhusu tofauti hizo ziwagawe na kuwasambatisha. Wakumbuke kwamba kila unapotokea mzozo, lazima upo mkono wa mpinzani wako, mkono wa CCM, ndiyo unaovuruga upinzani.
Nchi ipo salama
Mtazamo wa Mzee Mtei kwamba miaka 30 ya vyama vingine imekuwa ya mafanikio, unaungwa mkono na baadhi ya wakazi wa Arusha, wanaosema tofauti na mataifa mengine, mafanikio makubwa ni kwamba nchi bado ipo salama.
Joram Munisi anasema Tanzania kuendelea kuwa salama bila migogoro mikubwa kama yalivyo mataifa mengine ni jambo la kujivunia wakati wa kuadhimisha miaka 30 tangu kuanza vyama vya upinzani.
“Tunaona mataifa mengi kuna vita na migogoro, mikubwa kutokana na tofauti za kisiasa lakini kwetu licha ya kuwepo changamoto kadhaa bado vyama vimekuwa vikistahimili na kuvumiliana,” alisema
Neema Lukumay vyama vingi vimesaidia Taifa kujikosoa pale ambapo kuna changamoto lakini pia kuboresha mara sera na sheria kwendana na wakati na maoni wa wengine.
“Ni jambo zuri, miaka 30 hii Taifa limekuwa na umoja na mawazo ya vyama vya upinzani yamekuwa yakichukuliwa na kufanyiwa kazi japo kwa uchache,” anasema.
Mfanyabiashara Lucan Chuma anasema Watanzania walio wengi mwaka 1992 ilipokuja hoja ya kuanzisha upinzani walikuwa na hofu kuwa Taifa litakwenda kuingia katika machafuko lakini sasa wameona vyama vingi si uadui. “Binafsi nilikuwa mmoja ya waliopiga kura kura kutaka vyama vingi, nashukuru tunakwenda vizuri japo miaka sita iliyopita kulikuwa na changamoto,” anasema.