Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biashara haramu ya mkaa inavyoiteketeza Shinyanga



Dar/Shinyanga. Jioni jua linapokaribia kuzama katika vijiji vya Tinde, Samuye na Ishina Bulaindi wilayani Shinyanga, baiskeli na pikipiki zilizobeba magunia ya mkaa huanza kuonekana zikitokea kwenye njia za vumbi na kukatiza baadhi ya maeneo ya lami katika maeneo yanayounganisha vijiji hivyo na manispaa ya mji wa Shinyanga.

Pembeni mwa njia hizo, visiki vya miti iliyokatwa na maeneo yaliyobaki wazi yakizungukwa na weusi baada ya kuchomwa yanaonyesha kasi ya shughuli za uzalishaji wa mkaa katika eneo hilo.

Aidha, kwa wakazi wengi, mkaa si nishati ya kupikia pekee, bali ndiyo nguzo ya uchumi unaowapa kipato katika mazingira yenye fursa chache za ajira.

Lakini nyuma ya biashara hiyo kuna taswira inayotia wasiwasi. Takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha asilimia 95 ya mkaa unaozalishwa na kusafirishwa kutoka Shinyanga huingia sokoni kinyume cha sheria, hali inayokwepa mfumo wa leseni, tozo za Serikali na masharti rasmi ya usafirishaji.

Takwimu hizo zilizomo katika ripoti ya ‘The Potential and Optimal Strategies for Charcoal Sub-Sector Development in Tanzania 2019’ zinaashiria karibu kila gunia la mkaa linalotoka mkoani humo huzalishwa, husafirishwa au huuzwa nje ya mfumo rasmi unaotambuliwa na sheria.

Kwa mujibu wa sheria ya misitu, uvunaji wa mazao ya misitu kwa matumizi ya kibiashara unahitaji vibali rasmi, huku usafirishaji wa mkaa ukitakiwa kuambatana na hati maalumu za usafirishaji.

Sheria hiyo pia imeipa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) mamlaka ya kukagua, kukamata na kuzuia usafirishaji haramu wa mazao ya misitu.

Hata hivyo, ushahidi uliokusanywa katika vijiji vilivyotembelewa wakati wa uchunguzi wa makala hii unaonyesha biashara hiyo ikiendelea kwa kiwango kikubwa nje ya mfumo rasmi wa usimamizi.

Wafanyabiashara wa mkaa wanasema mkaa husafirishwa kupitia njia zisizo rasmi zinazojulikana kama njia za panya, ambazo huunganisha Tinde, Samuye, Ishina Bulaindi na vijiji vingine na masoko ya mijini.

Wafanyabiashara hao waliohojiwa na Mwananchi kwenye kata ya Tinde wilayani Shinyanga wanasema usafirishaji wa mkaa hufanyika waziwazi, hasa jioni na alfajiri, wakati baiskeli na pikipiki husafirisha mizigo kuelekea manispaa ya mji wa Shinyanga.

Pia, walisema kwa wasafirishaji wenye pikipiki hufanya kazi hiyo usiku mara nyingi.


Walichokisema wazalishaji

Mzalishaji wa mkaa, Maduhu Alphonce maarufu Pako, anasema ukataji miti na uchomaji mkaa bado ni miongoni mwa shughuli chache zinazowaingizia wananchi kipato.

"Tunakata miti, tunaandaa matanuru ya jadi na kuuza mkaa kwa wafanyabiashara wanaoupeleka mjini. Hiki ndicho kinachowasaidia wengi kuishi kwa sababu fursa nyingine ni chache," anasema.

Mzalishaji mwingine, Mponhela Jumanne, anasema biashara hiyo inaendelea kukua kutokana na mahitaji makubwa ya soko.

"Mradi kuna miti na wanunuzi, watu wataendelea kuzalisha mkaa," anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Misitu wa Wilaya ya Shinyanga na Mhifadhi Mwandamizi, Fabian Balere, anakiri kuwa bado kuna changamoto katika kudhibiti uvunaji na usafirishaji haramu wa mkaa.

"Sina takwimu kamili za kuthibitisha kiwango cha asilimia 95, lakini ukiukwaji wa taratibu za uvunaji na usafirishaji bado unaendelea kutokea," anasema.

Anasema mamlaka zinaendelea kufanya doria, ukaguzi na kampeni za uhamasishaji kwa wazalishaji na wafanyabiashara ili kuhakikisha wanafuata taratibu za kisheria huku ikiwawajibisha wanaokutwa na makosa hayo.

Licha ya manufaa ya kiuchumi, wakazi wanasema athari za mazingira zinazidi kuonekana.

Baadhi yao wanaeleza kuwa maeneo yaliyokuwa na misitu minene sasa yamebaki wazi, huku wengine wakisema hali ya mvua na ubora wa ardhi umebadilika kwa miaka ya karibuni.

"Miti ilikuwa mingi sana hapa zamani, lakini sasa maeneo makubwa yamebaki wazi. Wakati mwingine joto linaongezeka na hata kilimo si kama kilivyokuwa awali," anasema Rebeka Hamduni, mwenye umri wa miaka 69.

Mkazi mwingine, Rajabu Njige, mwenye umri wa miaka 76, anasema utegemezi wa mkaa umeziweka kaya nyingi katika mtego wa kuchagua kati ya mahitaji ya maisha na uhifadhi wa mazingira.

"Tunajua miti inapotea, lakini watu wanaendelea kwa sababu wanahitaji fedha na nishati ya kupikia," anasema.

Mbali na athari za mazingira, wakazi pia wanaeleza wasiwasi kuhusu madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Wanawake waliohojiwa walisema hupika katika mazingira yenye moshi mzito kutokana na ukosefu wa mfumo mzuri wa uingizaji hewa.

"Tunapopika, moshi unaathiri kifua na macho. Tumeishi hivi kwa miaka mingi kwa sababu mkaa ndiyo nishati ambayo familia nyingi zinaweza kumudu," anasema Rebeka.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), uchafuzi wa hewa unaotokana na matumizi ya nishati za jadi za kupikia husababisha takribani vifo vya mapema 815,000 kila mwaka barani Afrika. Tanzania pekee inakadiriwa kuwa na zaidi ya vifo 33,000 kwa mwaka vinavyohusishwa na magonjwa yanayotokana na kuvuta moshi wa nishati za biomasi.


Hali ilivyo

Takwimu za Ofisi ya Makamu wa Rais zinaonyesha Kanda ya Ziwa hupoteza takribani hekta 193,424 za misitu kila mwaka, huku Shinyanga ikiwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na uharibifu wa ardhi. Kwa kiwango cha Taifa, Tanzania hupoteza wastani wa hekta 469,420 za misitu kila mwaka.

Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu wa mwaka 2021–2031 unaonyesha kuwa mbinu za jadi za uzalishaji wa mkaa hutumia takribani asilimia 20 pekee ya nishati iliyopo kwenye kuni, huku sehemu kubwa ikipotea wakati wa uzalishaji.

Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya kaya za Shinyanga hutegemea nishati za biomasi kwa kupikia. Kuni zinachangia asilimia 56 ya matumizi hayo huku mkaa ukichangia asilimia 25.8.

Hata hivyo, mfanyabiashara wa mkaa, Dora Katunzi, anasema biashara hiyo inaendelea kuwa na faida kutokana na mahitaji makubwa ya soko.

"Gunia moja huuzwa kati ya Sh32,000 na Sh70,000 kulingana na ukubwa wake. Mahitaji yapo wakati wote kwa sababu kaya nyingi bado zinategemea mkaa," anasema.

Mfanyabiashara mwingine, Dotto Leonard, anasema wafanyabiashara wengi wanafanya shughuli zao nje ya mfumo rasmi.

"Watu wachache sana wana vibali sahihi kwa sababu mchakato wa kuvipata ni mgumu. Wengi wanaendelea kufanya biashara nje ya mfumo rasmi," anasema.

Licha ya sekta ya mkaa nchini kukadiriwa kuingiza karibu dola bilioni moja kwa mwaka, sehemu kubwa ya biashara hiyo bado ipo nje ya mifumo rasmi ya kodi na tozo kutokana na tabia hiyo ya kukwepa vituo vya ukaguzi vya TFS vilivyopo pembezoni mwa barabara kuu ya kwenda manispaa ya mji wa Shinyanga.


Viongozi wanasemaje?

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyambui, Kata ya Tinde, Masesa Mkata Chaula, anasema viongozi wa maeneo husika hushuhudia biashara hiyo kila siku lakini ushiriki wao katika usimamizi wake ni mdogo.

"Mara nyingi tunaona mkaa ukipita hapa, lakini jamii za maeneo haya hazishirikishwi vya kutosha katika kudhibiti biashara hiyo," anasema.

Anasema wakati mwingine viongozi wa maeneo hulazimika kubuni michango isiyo rasmi kusaidia shule na shughuli nyingine za kijamii kwa sababu hakuna mapato rasmi yanayotokana na biashara hiyo yanayorejea kwa jamii.

Naye Diwani wa Tinde, Jafary Makwaya, anasema shinikizo kwa mazingira linaendelea kuongezeka kadiri biashara hiyo inavyopanuka.

"Changamoto inaongezeka kwa sababu biashara inaendelea kukua wakati jamii zinaendelea kuitegemea kwa kiwango kikubwa," anasema.