Asilimia 60 ya uvunaji wa mkaa nchini ni haramu
Muktasari:
Kimsingi, biashara ya mkaa inategemewa zaidi na wananchi wenye kipato cha chini katika maeneo ya vijijini ambako Watanzania wengi ndiko wanakoishi.
Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania bado wanategemea mkaa na kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Mahitaji haya makubwa yanachangia kuwapo kwa soko kubwa hususan la mkaa katika maeneo ya mijini.
Kimsingi, biashara ya mkaa inategemewa zaidi na wananchi wenye kipato cha chini katika maeneo ya vijijini ambako Watanzania wengi ndiko wanakoishi.
Licha ya biashara hiyo kutegemewa na wananchi wenye kipato cha chini, watu wanaojihusisha na uchomaji wa mkaa wamezidi kuwa maskini kwa vile wafanyabiashara wamekuwa wakiwalangua kwa bei ndogo huku wao wakiuza bei kubwa sokoni jambo linalowaacha kwenye hali ya umaskini wa kipato.
Mkurugenzi wa mipango na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kilongo anasema biashara ya mkaa ni sawa na mazao mengine ya misitu kwa kuwa imeruhusiwa kisheria.
Changamoto za utaratibu
Hata hivyo, biashara hiyo kuanzia uvunaji wa misitu hadi usafirishaji imejaa changamoto nyingi licha ya kuruhusiwa na Serikali kupitia kifungu cha 2(2.2) cha mwongozo wa uvunaji mazao ya misitu wa mwaka 2017.
Kilongo aliwaambia wajumbe wa kikao cha utekelezaji wa randama ya makubaliano ya kuunganisha nguvu za pamoja katika kuzikabili changamoto zinazoikabili sekta ya misitu Kanda ya Ziwa mjini Geita kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya uvunaji na usafirishaji wa mkaa nchini unafanyika kinyume na sheria. Wajumbe 150 kutoka halmashauri za wilaya 30 za mikoa ya Kanda ya Ziwa wakiamo mameneja wa TFS, washauri wa maliasili, maofisa waTamisemi, menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na mwakilishi wa wajumbe wa bodi ya ushauri ya wakala kwa Wizara ya Maliasili na Utalii walihudhuria kikao hicho.
Anasema kwa Dar es Salaam pekee zaidi ya magunia 500,000 ya mkaa huingia kila mwezi yakiwa hayajulikana eneo ulikovunwa na kutumia leseni au hati ya kusafirishia mazao ya misitu zaidi ya mara moja. “Takwimu zinaonyesha kuwa moja kati ya makosa yanaonekana ni kujirudia kwa leseni zaidi ya mara moja au kutumika baada ya muda wa ukomo na kuzidisha kiasi cha magunia kilichopo kwenye leseni,” anasema.
Mkurugenzi huyo anasema kutumika kwa leseni na hati za kusafirishia mazao ya misitu zaidi ya mara moja kunatokana na kutokuwapo kwa mfumo mzuri wa utunzaji kumbukumbu kwenye maeneo ya wilaya na vizuizi.
Kilongo anasema tatizo jingine ni ukaguzi wa vibali vya mazao ya misitu na kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watumishi ambao huruhusu mazao ya misitu kupita bila kugongwa mihuri ya vibali kwa lengo la kuwaruhusu wafanyabiashara kutumia kibali zaidi ya mara moja.
Anaongeza kuwa, kuzidisha uzito ulioidhinishwa kulingana na utaratibu uliowekwa na Serikali ni kinyume na sheria akisisitiza kwamba, “uzito wa gunia la mkaa ni kilo 50 lakini bado uzito wa gunia la mkaa unazidi kilo 100 na wafanyabiashara kulipia tozo za chini tofauti na ujazo.”
Usafirishaji na uvamizi
Kilongo anasema ukiukwaji wa muda wa usafirishaji mazao ya misitu hususan mkaa unaofanywa na waendesha baiskeli wa Kanda ya Ziwa na wafanyabiashara wengine wa mazao ya misitu ni kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa taarifa za TFS, wastani wa pikipiki 582 husafirisha mkaa kuingia jijini Dar es Salaam kwa siku kila moja ikiwa na kati ya magunia matatu mpaka sita kinyume cha sheria.
Hata hivyo, kampeni na operesheni zinazoendelea kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na kikosi cha usalama barabarani imesaidia kupunguza wimbi la biashara hiyo. “Hili tunapaswa kulikemea kwa nguvu zote na pia tuchukue hatua maana linachangia kuharibu misitu. Hatuna budi kuilinda misitu maana ndiyo uhai wetu na katika kupambana na haya yote lazima tushirikiane, misitu ni ya thamani,” anasisitiza.
Kilongo anasema changamoto nyingine ni misitu kuvamiwa na uvunaji haramu unaoendelea ambao unasababisha kupotea kwa uoto wa asili na mapato ya Serikali.
“Sasa sisi ambao tumekabidhiwa dhamana kwa maana ya meneja misitu wa wilaya anayeshughulikia misitu ya wilaya na ofisa misitu wa wilaya ambaye yuko Tamisemi tumeona ni vyema tukae tukumbushane majukumu yetu. Tunaposema tunataka kuhifadhi, tunahifadhi wapi na tunahifadhi nini,” anasema.
Anaongeza kuwa, masuala yanayojitokeza zaidi ni uvunaji ambao kila mtu anataka kuvuna anavyotaka kwa kuwa kuna kipato kinachopatikana, lakini kabla ya kuvuna lazima maeneo yanayovunwa yaanishwe, uwapo mpango wa usimamizi, mpango wa uvunaji na kiasi kinachovunwa lazima kijulikane na kile kinachobaki ili mwisho wa siku mapato ya Serikali yajulikane.
Biashara ya mkaa
Mara kadhaa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepiga marufuku usafirishaji wa mkaa kutoka wilaya moja kwenda nyingine kwa lengo la kukabiliana na ukataji wa miti ambao una mchango katika uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi nchini.
Marufuku hizo zimekuwa zikiibua mijadala mbalimbali katika mitandao ya jamii, vyombo vya habari na hata mitaani kuhusiana na hatua ya Serikali ya kudhibiti uvunaji haramu wa mkaa huku wengine wakizihusisha hatua hizo na upigaji marufuku wa nishati hiyo.
Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa mstari wa mbele kutafuta suluhisho la kudumu la nishati hiyo, ambapo TFS imekuwa ikishirikiana na asasi mbalimbali za kiraia za uzalishaji wa nishati mbadala na pia kuzungumza na wazalishaji wa gesi ili wazalishe katika ujazo mdogo itakayouzwa kwa bei nafuu.
Miongoni wadau wanaoshirikiana na TFS katika kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ni kampuni moja inayotumia teknolojia ya kisasa kuzalisha na kusambaza mkaa endelevu iliyopo Mafinga mkoani Iringa.
Kampuni hiyo ni miongoni mwa nyingi nchini zinazozalisha na kusambaza mkaa unaotokana na taka zitokanazo na uchakataji wa mbao na mabaki ya miti ikiwa ni teknolojia inayosaidia kupunguza matumizi makubwa ya mkaa unaotokana na misitu asilia katika miji mikubwa.
Mwanri, Silayo wanasemaje?
Mtendaji mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos anasema misitu inakabiliwa na changamoto nyingi, ambapo kuanzia Kanda ya Ziwa kuelekea kusini inaathirika kwa kasi kutokana na uharibifu unaotokana na tabiachi, shughuli za kibinadamu kama ukataji wa miti kwa ajili ya nishati, mbao; kilimo cha kuhamahama na kadhalika.
“Zipo pia shughuli za ufugaji, uchimbaji madini na uvamizi wa misitu na moto unaoanzishwa na watu mbalimbali. Tunapaswa tuweke mikakati ya kuutokomeza,” anasema.
Anasema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya watendaji kuwalazimisha wananchi wanaomiliki misitu vijijini kuifyeka kwa kisingizio cha kuendeleza maeneo yao kupitia kilimo.
“Hili likemewe kwa nguvu zote na pia tuchukue hatua maana linachangia kuharibu misitu yetu. Hatuna budi kuilinda misitu yetu maana ndiyo uhai wetu. Na katika kupambana na haya yote lazima tushirikiane, misitu yetu ni ya thamani,” anasisitiza.
Hata hivyo, mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri anawataka wakuu wa wilaya ambao sasa wanapaswa kuongoza harakati za ulinzi wa misitu katika maeneo yao kutenga muda mwingi wa ziada kushughulikia rasilimali ya misitu ipasavyo.
“Mkakati ni ile mbinu ya kuwa na mpango wa pamoja, lakini huku nyuma lazima uanze na lengo. Ukiwa na mikakati unaweza kufika mbali katika shughuli zako,” anasema.
“Mnajua nini, misitu ikiharibika maji hayatakuwapo na maji yasipokuwapo hata watu hawatasubiri kufukuzwa, isipokuwa wataondoka wenyewe maana kile kitu muhimu wanachokitegemea hakitakuwapo, hivyo ni wajibu wenu kusimamia hili.”
Ardhi ya Tanzania Bara ina eneo lenye ukubwa wa hekta milioni 88 ambapo asilimia 55 imefunikwa na misitu. Misitu ya matajiwazi ina ukubwa wa hekta milioni 44.7 (sawa na asilimia 93 ya eneo lote la misitu) huku asilimia saba ikiwa ni misitu ya Lindimaji, mikoko, ya Pwani na mashamba ya miti.
Kwa mujibu wa ripoti ya tathmini ya rasilimali za misitu iliyofanyika mwaka 2009-2014 iliyotolewa na Wizara ya Malisili na Utalii kupitia taarifa ya tathmini ya rasilimali za misitu (Naforma), moja ya tatu ya eneo lililofunikwa na misitu linamilikiwa na Serikali kuu katika takribani misitu 500 huku mbili ya tatu ya eneo likiwa chini ya usimamizi wa Serikali za mitaa yaani misitu 231, vijiji na sekta binafsi.