Ekari 500 zatengwa vijana walime Musoma

What you need to know:
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini imetenga jumla ya ekari 500 kwaajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji unaotarajiwa kutekelezwa na Taasisi ya kilimo ya vijana.
Musoma. Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini imetenga ekari 500 kwaajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji unaotarajiwa kutekelezwa na Taasisi ya kilimo ya vijana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa taasisi hiyo mkoani Mara leo Septemba 17, 2023; Kaimu Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo, Ismail Mafuru amesema eneo hilo limetengwa katika bonde la kilimo la Bugwema kata ya Bugwema.
"Eneo linafaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama Alizeti,Mahindi, Dengu na mazao megine ya biashara na chakula,kila kitu kiko tayari hata mkitaka kulima kuanzia leo njooni,"amesema
Katibu wa taasisi hiyo mkoani Mara, Anna Frank amesema mbali na eneo hilo la Bugwema lakini pia Wilaya za Rorya na Serengeti tayari nazo zimetenga maeneo kwaajili ya taasisi hiyo kuanzisha miradi ya kilimo.
"Tunashukuru Serikali za wilaya za Rorya na Serengeti kwani wao pia tayari wametenga maeneo ila tulishindwa kuyafikia maeneo hayo kutokana na changamoto ya ukosefu wa mafuta kwenye vituo ila muda si mrefu tutatembelea maeneo hayo,"amesema
Ofisa Maendeleo Wilaya ya Butiama, Rebecca Sanga ameitaka taasisi hiyo kuwa kielelezo kizuri kwa vijana kwa maelezo kuwa licha ya kuwepo fursa nyingi katika kilimo lakini vijana wengi bado hawajanufaika na fursa hizo.
"Changamoto kubwa kwa vijana wanataka mali kwa haraka wakati kilimo kina fursa nyingi lakini ni mchakato na sio kitu rahisi, Serikali imetengeneza mazingira kwa vijana kutokana na umuhimu wao lakini bado hawajatumia nafasi hiyo vema,”
"Fursa zipo kuanzia ofisi ya Rais hadi katika halmashauri kuna mifuko mingi inayotoa mikopo kwaajili ya vijana lengo ni kuhakikisha vijana wanafikia malengo na wanakuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo na biashara hali itakayosaidia kuboresha uchumi wao na wa taifa kwa ujumla kwani kilimo kinalipa hasa ukikijulia,"amesema Rebecca
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Bunda, Adelina Mfikwa amesema wataalamu wa kilimo katika wilaya hiyo wapo tayari kutoa msaada wa kitaalamu ili taasisi hiyo iweze kufanya vizuri na kufikia malengo ambayo yatapelekea vijana wengi kuingia kwenye kilimo.
"Tayari Serikali imetengeneza mazingira wezeshi kwaajili ya kilimo hususan kwa vijana na sisi tuko tayari kutoa msada wa kitaalamu shughuli hizi ziwe za kitaalamu ili kilimo chetu kiwe chenye tija sasa kazi kwenu vijana," amesema Adelina
Akizindua taasisi hiyo, Ofisa Kilimo Mkoa wa Mara, Kutilikwa Lazaro amewataka vijana kujitokeza na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo ili kijikwamua kiuchumi.
"Kilimo ni ajira vijana jitokezeni kuna fursa nyigi huko, Serikali yenu tayari imeona kuna umuhimu wa kuwasaidia kuyafikia malengo kupitia sekta hii kinachotakiwa ni utayari wenu tu,"amesisitiza