Elon Musk kuwekeza Tanzania

Elon Musk

Muktasari:

Wakati Tanzania ikipokea maombi ya huduma ya intaneti kwa njia ya setelaiti (Starlink), wadau wamesema itachochea uchumi wa kidijitali na itakuwa nafuu na yenye kasi.

Da es Salaam. Wakati Tanzania ikipokea maombi ya huduma ya intaneti kwa njia ya setelaiti (Starlink), wadau wamesema itachochea uchumi wa kidijitali na itakuwa nafuu na yenye kasi.

Taarifa hizo zinasema, huenda hadi kufika Machi 2023 teknolojia hiyo inayomilikiwa na Kampuni ya SpaceX itakuwa imeingia nchini.

Kwenye tovuti yao rasmi, Starlink inayomilikiwa na tajiri Elon Musk ilitangaza mpango wao wa kuleta huduma hizo nchini kati ya Januari na Machi 2023, kama wataruhusiwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miezi miwili imepita tangu Tanzania izindue huduma ya intaneti ya 5G yenye kasi zaidi.

Hata hivyo, mpango wa Starlink kuingia nchini utategemea idhini ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari aliithibitishia Mwananchi kuwa kampuni hiyo ya Starlink ilituma maombi ya kutoa huduma ya intaneti nchini.

“Ndiyo, ninayo taarifa kuwa kampuni hiyo ilituma maombi kupitia tovuti ya TCRA,” alisema Dk Bakari.

Hadi sasa, Nigeria na Msumbiji ndizo nchi pekee za Afrika zimeruhusu Starlink kufanya kazi baada ya kuwapatia idhini kutoka mamlaka zao za udhibiti.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo alisema Starlink itakuwa na matokeo chanya na itateka soko kama itawanufaisha watumiaji, hasa kwenye kukidhi mahitaji yao.

“Ikiwa huduma itafika nchini itasaidia wakulima kupata habari kuhusu hali ya hewa na jinsi wanavyoweza kuboresha mazao yao, itasaidia wafanyabiashara kufanya biashara zao mtandaoni na kupata mafunzo yanayokusudiwa, itawafanya wateke soko kwa kuwa watakuwa wameyafikia mahitaji ya watumiaji.

Mdau wa teknolojia, Jumanne Mtambalike alisema huduma ya mtandao ya Starlink itachochea uchumi wa kidijitali.

Mtambalike, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures, alisema huduma hiyo itachagiza sekta mbalimbali kuanzia kilimo, elimu hadi afya.

Teknolojia ya intaneti ya Starlink inapatikana baada ya kuunganishwa kwa satelaiti nyingi ambazo hutumika kutoa huduma ya intaneti kwenye maeneo mbalimbali duniani, hasa ya vijijini.