Ewura yacharuka wanaoficha mafuta, Bodaboda wahaha
Madereva wa pikipiki wakiwa kwenye foleni katika moja ya kituo cha mafuta wilayani Handeni mkoani Tanga wakisubiria mafuta kutokana na uhaba wa kupatikana huduma hiyo. Picha na Rajabu Athumani
Muktasari:
- Mpaka sasa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imefungia utoaji huduma kwa baadhi ya vituo baada ya kubaini kuficha mafuta, ikiwemo Camel Oil cha Msamvu na Mtemba cha Tuliani mkoani Morogoro.
Handeni. Chemba ya wafanyabiashara Wilaya ya Handeni mkoani Tanga imeishauri Serikali, kuchukua hatua kwa waingizaji mafuta wakubwa nchini ambao ni wamiliki wa vituo vya mafuta, wakiwatuhumu ndiyo wanahusika kuficha mafuta.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wilaya ya Handeni, Aldof Lyakundi wakati akiongea na Mwananchi leo Jumanne Septemba 5, 2023 na kusema kuwa changamoto iliyopo ni wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza mafuta, kuyaficha ili wauze wao wenyewe.
Amesema wafanyabiashara hao huagiza mafuta kutoka nje na kuyahifadhi kwenye stoo zao, ili baadaye bei ikipanda wanauza kwenye vituo vyao na kukataa kusambaza kwenye vituo vya wafanyabiashara wadogo kwa sasa.
"Wafanyabiashara wakubwa ndio chanzo cha hili tatizo la uhaba wa mafuta, wanaagiza na kuficha wakisubiri bei ipande ndio wauze kwa wafanyabiashara wadogo. Serikali lazima ichukue hatua madhubuti katika hili bila kufanya hivyo wananchi wataendelea kuteseka hawa wanaangalia faida yao siyo jinsi wananchi wanavyoteseka," amesema Lyakundi.
Ameongeza kuwa mafuta kwenye vituo vikubwa vyote yapo ila wamiliki hawataki kuwauzia wenye vituo vidogo, nia wanasubiria kupanda kwa bei hivyo Serikali inatakiwa kuthibiti suala hilo ambalo linaumiza wananchi.
Dereva wa bajaji Stendi ya Chogo Handeni Mustafa Msita amesema kuwa, mafuta ni kweli yapo kwani wapo watu wanauza mitaa kwenye vidumu, ina maana ipo sehemu wanachukua na kuja kuuza mtaani.
"Kama mfanyabiashara amenunua lita moja kwa Sh3500 kwa uhalisia hawezi kuuza chini ya hapo, lazima bei iwe juu. Hivyo kutokana na hilo na haya mambo ya dola kupotea wakae chini tunaumia wananchi," amesema Msita.
Mwenyekiti Halmashauri ya Mji Handeni, Mussa Mkombati ameongeza kuwa uhalisia mafuta kwenye vituo yapo, ila wanachopingana wafanyabiashara na Ewura ni kwamba bei inayopangwa ipo chini ya walivyonunua.
"Halmahauri ya mji Handeni hali ni mbaya madereva wanalala kwenye vituo vya mafuta kwa ajili ya kuweka foleni, hili suala lazima litafutiwe ufumbuzi wa kudumu maana linatesa wananchi wetu," alisema Mkombati.