Ewura yavifungia vituo viwili
Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imevifungia vituo viwili vya mafuta kwa kosa la kuhodhi mafuta kati ya Julai na Agosti mwaka huu.
Vituo vilivyotajwa kufungiwa na Ewura ni Rashal Petroleum Limited kilichopo Mlimba mkoani Morogoro na Kimashuku Investment kilichopo Babati mkoani Manyara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema: “Kila tunapokifungia kituo kwa miezi sita, tunataka umma ufahamu kwa sababu hawa ndiyo wanaochangia kusuasua kwa usambazaji wa mafuta hapa nchini.”
Amesema pamoja na mafuta kuwapo nchini, changamato katika maeneo mbalimbali ilichangiwa na baadhi ya wamiliki wa vituo kuyahodhi ili kujipatia masilahi ya kibiashara ikiwamo faida kubwa kutokana na ongezeko la bei ya mafuta kinyume cha sheria.
Ewura imetoa onyo kali kwa wauzaji wa jumla na wamiliki wa vituo vya mafuta, kuwa Serikali inafuatilia suala hilo kwa karibu kupitia vyombo vyake mbalimbali. Kaguo alisema hadi kufikia juzi mamlaka ilikuwa imevisimamisha vituo saba kutokana na kukiuka sheria inayotakiwa kufuatwa.
Kati ya vituo hivyo, alisema vinne ni vya mkoani Morogoro. Alieleza kosa kubwa ni vitendo vya kuficha mafuta jambo linalokiuka sheria walizopewa kama sehemu ya mkataba wao.