Fahamu namna bodaboda zinavyotoa ajira kwa wanawake

Jalia Mushi akiwa amebeba abiria akiendelea na majukumu yake eneo la Mabibo Hosteli jijini Dar es Salaam. Picha na Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Kazi ni kazi bora mkono uende kinywani. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na maisha ya wanawake wanne waliojitosa kujitafutia kipato kwa kufanya shughuli ya kubeba abiria kwa kutumia pikipiki, maarufu kama bodaboda.

Wanawake hawa waliofikiwa na Mwananchi ni sehemu ya wengine 30 wanaofanya kazi hii jijini hapa iliyozoeleka kufanywa na wanaume.

Katika makala hii, wanawake hao wanazungumzia kazi hiyo, faida wanayopata na changamoto wanazokumbana nazo katika kazi hiyo.

Waliingiaje kazini?

Janeth Shirima, anayefanya kazi Feri jijini hapa anafungua pazia la mazungumzo na Mwananchi akieleza alipenda kuendesha pikipiki kitambo, hivyo akiwa nyumbani wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, alijifunza kupitia bodaboda ya kaka yake.

Katika harakati za kusaka maisha, anasema mwaka 2020 alikuwa akiuza nguo eneo la Feri, jirani na kijiwe cha bodaboda, ndipo alipovutika na safari yake ya kufanya kazi hiyo ikaanzia hapo.

“Siku moja nikiwa pale kuna kaka anayeendesha boda tunamwita Uchebe, alinizoea sana, akaniuliza kwa utani kama naweza kuendesha boda. Nilimjibu naweza, akanipa pikipiki nikaendesha.

“Wakati naiendesha kuna mwingine tunamwita Mchungaji akaniona, akavutiwa na uendeshaji wangu. Akaniambia ana boda nyingine kaiweka ndani, hivyo anaona ni wakati wa kuitengeneza na kunipa niendeshe,” anasimulia Janeth, mwenye miaka 33 ambaye kijiweni amezoeleka kwa jina la Manka.

Anaeleza Mchungaji alimpatia pikipiki na akawa anampatia Sh10,000 kwa siku kutokana na makusanyo ya fedha alizopata kwa kazi hiyo.

Kutokana na uchakavu wa pikipiki hiyo, ilihitaji matengenezo ya mara kwa mara, hivyo Janeth anasema baada ya miezi mitatu kwa msaada wa wenzake alipata nyingine.

Anasema alifanya kazi hadi Januari mwaka jana alipopata ajali ya kugongwa na gari eneo la Tabata Segerea njiapanda ya kwenda Bonyokwa.

Janeth anasema mwenye pikipiki alimvumilia kwa kipindi chote cha miezi saba aliyokuwa akijiuguza kwa kuwa katika ajali hiyo alivunjika mfupa wa paja.

“Miaka miwili baadaye niliachana naye, baada ya kupambana kupata pikipiki yangu, ambayo fedha nyingine nilikopa kwenye kikoba. Nilinunua mpya kwa Sh3 milioni,” anasema.

Janeth anatoa wito kwa wanawake kutochagua kazi ilimradi iwe halali, akisema maisha ya kumtegemea mtu hayafai.

“Kupitia kazi hii licha ya kulipa kodi na kujikimu kwa matumizi mengine, inaniwezesha kumlea mtoto wangu baada ya kutengana na baba yake. Mtoto wangu anasoma darasa la tano na ninamsomesha shule binafsi,” anasema.

Kwa upande wa Veronica Mgaya, anayefanya kazi Kimara Baruti, tofauti na Janeth anasema alianza kazi hiyo baada ya kupata changamoto ya kutengana na mzazi mwenzake waliyeishi naye jijini hapa na kulazimika kurudi kwao mkoani Mbeya kujipanga upya.

Anasema ili kuhakikisha anamudu malezi ya mtoto wake ambaye hivi sasa ana miaka 13 anayesoma darasa la sita, aliamua kujikita katika kuendesha bodaboda.

Veronica, ambaye kijiweni anajulikana kama ‘Mama Love’, anasema kwa miaka saba walipokuwa wakiishi pamoja alikuwa mama wa nyumbani. Anaeleza alijifunza kuendesha pikipiki hata kabla ya kutengana na mzazi mwenzake ambaye alikuwa akiendesha chombo hicho cha moto.

Anasema awali kabla ya kuanza kazi alijiuliza jamii itamchukuliaje kwa kuwa alijulikana kama mke wa mtu na mama wa mtoto mmoja.

“Nilipiga moyo konde na kuingia barabarani, tena kwenye kijiwe ambacho mzazi mwenzangu ndipo anafanyia kazi pia,” anasema Veronica.

Anaeleza alianza kuendesha pikipiki ya mtu na baadaye alipata pikipiki ya mkopo ambao aliulipa kwa kufanya kazi kwa mwenye pikipiki na kuukamilisha ndani ya mwaka mmoja.

Anasema kutokana na kazi hiyo, hivi sasa anasoma elimu ya sekondari aliyoikosa awali kutokana na hali ngumu ya familia yao iliyosababisha kuishia darasa la saba.

Mbali na Veronica, Mwananchi ilizungumza na Brigita Ambrose, ambaye ana miaka mitatu katika kazi ya bodaboda na kijiweni kwake ni Kimara.

Anaeleza baada ya kuchoshwa na kazi ya kuuza dukani kwa mtu aliamua kuendesha bodaboda.

Mwaka mmoja baada ya kuanza kazi anasema alipata ujauzito akalazimika kupumzika mimba ikiwa na miezi saba.

Anasema baada ya kujifungua alirejea kazini na kwa sasa mtoto wake ana miaka mitatu, akilazimika kumuacha kwa rafiki yake waliyepanga nyumba moja.

Brigita mwenye miaka 21, anasema bado hajafanikiwa kumiliki pikipiki, hivyo anaendelea kuendesha ya bosi wake na anapeleka hesabu ya Sh10,000 kila siku.

Kijiweni Kariakoo Msimbazi, ni eneo la kazi la Jalia Mushi, mwenye uzoefu wa miaka mitatu.

Jalia anasema awali alifanya kazi ya kusambaza vinywaji vikali kwenye kampuni ya kuoka mikate, lakini kutokana na shauku ya kutaka kujiajiri, aliamua kuendesha bodaboda.

Akizungumzia ajali, Jalia anasema baadhi ya bodaboda hawajui sheria za usalama barabarani, wengi wakijifunza kuendesha mtaani.

Anasema yeye yuko makini awapo barabarani, akimshukuru Mungu kwamba hajawahi kupata ajali.

Huduma kwa familia

Janeth anasema mwisho wake wa kufanya kazi ni saa 12.30 jioni, anafanya hivyo ili aweze kukaa na kufuatilia maendeleo ya mtoto wake.

Anasema nafasi yake kama mama bado ipo palepale, licha ya kazi yake ya kushinda barabarani.

Akizungumzia anavyopanga majukumu ya kifamilia, Veronica anasema huamka mapema kufanya shughuli za nyumbani, lakini ikitokea akapata mteja wa mapema zaidi asubuhi, humpeleka na baadaye hurejea kuendelea kuzifanya.



Veronica anasema mtoto wake alipokuwa mdogo alikuwa akimwacha kwa majirani na baadaye hurejea kumuangalia, lakini sasa anasoma darasa la sita, anamudu kujipikia.

Anaeleza huwa anafunga kazi saa moja usiku ili kuwa na mtoto wake, akiamini kuchelewa kurudi nyumbani si sababu ya kupata fedha nyingi.

Brigita anasema analazimika kuamka saa 11 alfajiri kuandaa uji wa mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu kwa sasa.

“Inapofika saa nne asubuhi huwa narudi kumwangalia mtoto. Kazi huwa nafunga kati ya saa mbili na saa nne usiku,” anasema.

Changamoto wanazopitia

Veronica anasema moja ya changamoto anazokabiliana nazo ni abiria kutomwamini, baadhi wakitaka kujua uzoefu wake wa kuendesha pikipiki.

Anasema anapowafikisha safari yao ndipo huaminiwa.

Anaeleza kuhamishwa kwa kituo cha mabasi yaendayo mikoani kutoka Ubungo kwenda Mbezi Luis na ongezeko la bajaji kumeifanya kazi hiyo kuwa ngumu tofauti na awali.

Kuhusu safari za usiku wa manani, Veronica anasema anaweza kufanya kazi iwapo anamfahamu mteja huyo.

Brigita anasema, “Niliwahi kuingia mkataba wa bodaboda nikafikisha miezi sita, baada ya kuuguliwa na mtoto kwa miezi kadhaa niliporudi kazini nikakuta amepewa mtu mwingine”.

Anasema hilo lilimfika pia alipokwenda kujifungua kwa kuwa alikuwa amebakiza miezi mitatu kumaliza mkataba ili pikipiki iwe mali yake lakini bosi aliichukua.

“Wanawake tunapitia changamoto nyingi katika kazi hii, tunaiomba Serikali ituangalie kwa jicho la karibu, ikiwemo kutupatia mikopo isiyo na masharti magumu.

“Mikopo tupewe moja kwa moja badala ya kupitia vikundi kama ilivyokuwa inafanyika kabla ya kusimamishwa kwa ile inayotolewa na halmashauri,” anasema.

Kauli za wadau

Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya waendesha bodaboda na bajaji mkoa wa Dar es Salaam, Said Chenja anasema wanalenga kutengeneza kitengo maalumu kwa ajili ya waendesha pikipiki wanawake ili kuongeza idadi yao. Pia kuhakikisha wanawapatia mafunzo.

Alisema wanaangalia uwezekano wa kuzungumza na benki kuwezesha mikopo ya pikipiki kutolewa kwa wanawake, kwa kuwa mikataba wanayoingia na wamiliki wa vyombo hivyo inawaumiza.

“Mikataba na mabosi kwa muda mrefu tumekuwa tukipiga nayo kelele kuwa inatuumiza. Mpaka unamaliza unaweza kujikuta unanunua boda kwa Sh4 milioni wakati dukani unapata hadi Sh1.7 milioni,” alisema.

Chenja alisema mkoani Dar es Salaam pikipiki zilizosajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni 400,000.

Alisema chama hicho kina wanachama zaidi ya 200,000 na kati yao 30 ni wanawake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala, Jomaary Satura alisema ni vigumu kutoa mkopo kwa mtu mmoja mmoja kwa kuwa hutolewa kwa vikundi.

Alisema mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vijana dhamana yake ni kikundi.

Satura aliwashauri kuunda kikundi cha watu watano ambacho kinaruhusiwa kisheria kupata mkopo ili waweze kupata pikipiki tano kila mmoja awe na yake.

Maisha ya kijiweni

Janeth anasema kwa kawaida huamka mapema kuwahi kijiweni ambako yeye ni mwanamke pekee na huko hukumbana na mzaha kutoka kwa wenzake.

“Kwa kawaida saa 11 alfajiri huwa nipo kijiweni, basi wakija wenzangu utasikia, ‘wewe mwanamke unamhudumia mume wako saa ngapi, kama saa hizi ushafika kijiweni kabla yetu.

“Hela unazokusanya unakwenda kumhonga nani, mpaka uamke usiku hivi,” anaeleza Janeth.

Jalia anasema kuna baadhi ya watu hufika kijiweni wakijifanya abiria lakini lengo lao ni kumtongoza.

Anasema wapo wanaomshangaa awapo barabarani, akionekana kama kitu cha ajabu, lakini kuendesha bodaboda ni kazi kama wanavyofanya wanaume.

Kwa upande wake, Brigita anasema baadhi ya abiria wanawake hawawaamini, hata wanapokwenda vijiweni huwapita na kwenda kupakia pikipiki ya dereva mwanamume.