Fidia kwa wakazi Bonde la Msimbazi fupa gumu

Dar es Salaam. Wakati wakazi wanaopisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi wakidai kuwa fidia walizopangiwa kulipwa hazilingani na thamani halisi ya nyumba zao, Serikali imesema uthamini uliofanyika haukuhusisha ardhi, bali mali zinazohamishika zilizokutwa katika eneo husika.
Kufanyika kwa uthamini huo, kunatokana na mpango wa Serikali wa kuendeleza bonde hilo unaofanyika kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB).
Kampuni binafsi ya NORPLAN Limited ndiyo iliyopewa kazi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufanya uthaminishaji makazi ya wananchi hao na imeshalitekeleza hilo mapema mwaka huu.
Machi 8 mwaka huu, katika ukumbi wa DRIMP uliopo jijini hapa, kampuni hiyo ilianza kutoa ripoti ya uthamini kwa wananchi hao, shughuli ambayo iliibua utata miongoni mwa wakazi hao kwa kile kilichoelezwa kuwa fedha inayotakiwa kulipwa haiendani na thamani ya nyumba zao.
Mmoja wa wakazi hao, Teresia Thadei alisema anashangaa nyumba yake yenye vyumba viwili anatakiwa kulipwa Sh1.2 milioni.
‘‘Sasa nikilipwa kiasi hicho cha fedha nitafanya nini, maana haitoshi hata kununua kiwanja mjini,” alisema Teresia.
Naye Matilda Kalumba alisema nyumba yake yenye ukubwa wa vyumba 12 anatakiwa kulipwa fidia ya Sh4 milioni, kiasi alichodai ni kidogo kulingana na thamani halisi
Mwananchi mwingine, Kheri Said alisema kulingana na maelezo ya wathamini hao, uthamini haukuhusisha viwanja bali majengo pekee.
“Kama wamefanya uthamini wa majengo tupu ina maana hayakuwa kwenye ardhi? Hii inashangaza,” alieleza.
Serikali yafafanua
Akifafanua mtanziko huo, Mratibu wa Miradi ya Serikali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, Humphrey Kanyenye, alisema uthamini uliofanyika haukuhusisha ardhi, bali mali zinazohamishika zilizokutwa kwenye eneo husika.
Kanyenye alisema uthamini umehusisha mali zisizohamishika pekee na si ardhi kama ilivyotarajiwa na wengi. Hilo linatokana na kile alichokifafanua kuwa, maeneo hayo yalishatolewa notisi na Serikali tangu mwaka 1979 kwamba hayapaswi kuendelezwa na mwananchi yeyote.
Pamoja na notisi hiyo, alisema baadhi ya wananchi wamejenga makazi ya kudumu na kuishi, hivyo malipo yanafanywa kwa huruma ya Serikali.
“Kwa kuwa eneo lilitolewa notisi tangu mwaka 1979 hakuna fidia ya ardhi itakayolipwa baadaye bila kuangalia ukubwa. Kitawekwa kiwango kinachofanana kwa wote,” alieleza.
Hata hivyo, alisema kwa wale waliokuwa na ardhi pembezoni na eneo hilo na wana hati miliki, watalipwa ardhi kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Kanyenye, kabla ya kuanza uthamini wananchi walishirikishwa tangu mwaka 2021 na wote walikubali.
“Tatizo baadhi ya wananchi walikuwa na matarajio makubwa, sisi tumekuta nyumba imeshaharibiwa na mafuriko...’’ alisema.