Fundi mwashi adaiwa kuuawa akibishana na wenzake
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linawashikilia watu wanne wilayani Rombo kwa madai ya kuhusika na mauaji ya fundi mwashi, Benson Machui anayedaiwa kuuawa kwa kuchomwa kisu na kisha mwili wake kutelekezwa katika ofisi ya Kijiji cha Mamsera juu.
Rombo. Watu wanne wakazi wa wilayani Rombo wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wakidaiwa kuhusika na mauaji ya fundi mwashi, Benson Machui (30) kwa kumchoma kisu.
Watu hao wanadaiwa kuuawa Machui, mkazi wa Kijiji cha Old Moshi usiku wa Januari 14, 2024 na kisha mwili wake kuutelekeza katika ofisi ya Kijiji cha Mamsera juu wilayani humo.
Inadaiwa tukio hilo limetokea baada ya kuangalia mpira katika moja ya baa maarufu iliyopo eneo la soko la Mamsera wilayani humo.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kuzungumzia mauaji hayo, hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo leo Januari 16, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema mpaka sasa watu wanne wanashikiliwa na Polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji hayo.
Mwangwala ameeleza vijana hao baada ya kutoka kuangalia mpira usiku katika moja ya baa maarufu iliyopo eneo la soko la Mamsera, walikuwa wakibishara na marehemu hali iliyosababisha ugomvi na hatimaye kifo chake.
"Tarehe 14 usiku, baada ya kumalizika kwa mchezo wa Afcon (Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika), ambao walikuwa wanaangalia kwenye moja ya baa iliyopo hapa Mamsera,kukatokea mabishano fulani baina yao na kusababisha ugomvi na kisha marehemu kuchomwa kisu," amesema.
Amesema marehemu alichomwa sehemu ya mkono wa kushoto na kutokea upande mwingine, hali iliyosababisha kifo chake kutokana na kuvuja damu nyingi.
"Mpaka sasa wameshakamatwa watu wanne na wengine wanaendelea kusakwa kwa kuhusika na tukio hili, ili kubaini hasa chanzo cha tukio ni nini," amesema Mwangwala.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Mamsera juu, Peter Shayo amesema baada ya kupata taarifa za mwili kutupwa ofisini kwake alikwenda eneo la tukio na kushuhudia mwili huo ukiwa chini huku ukivuja damu sehemu mbalimbali mwilini.
"Tulipata taarifa kuna mtu amefia hapa ofisini kwangu, nilifika ile asubuhi na niliukuta mwili ukiwa chini na ulikuwa unavuja damu sehemu mbalimbali, nilitoa taarifa polisi na walikuja kuuchukua mwili," amesema.
Aidha, mwenyekiti huyo wa kijiji amewataka wananchi wa maeneo hayo kutoa taarifa pindi anapoonekana mgeni anayetilia mashaka, ili hatua zichukuliwe mapema dhidi yake
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, wilayani Rombo kwa ajili ya uchunguzi.