Gari la shirika la umma ladaiwa kuua mwanafunzi, wananchi wafunga barabara

Wananchi wakiwa eneo la Mbwewe Bagamoyo Mkoani Pwani ilipotokea ajali.

Muktasari:

  • Mwanafunzi huyo anakuwa wa 11 kufariki dunia kwa kugongwa na gari katika eneo hilo na huyu wa safari hii anadaiwa kugongwa na gari lililokuwa na namba za Serikali.

Bagamoyo. Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Amani Voda, Hamisi Mchelewa amepoteza maisha baada ya kugongwa na gari lenye namba za shirika la umma ambalo halijatambuliwa.

Ajali hiyo imetokea leo Jumatatu Aprili mosi, 2024 katika eneo la Kibindu wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na ajali hiyo, Diwani wa Mbwewe, Omary Abbas amesema "mwanafunzi huyu amegongwa na gari la Serikali na amekufa palepale, huyu ni mwanafunzi wa 11 kupoteza maisha kwa kugongwa na gari eneo hili ambalo wanafunzi wanavuka,” amesema diwani huyo.

Amedai baada ya ajali kutokea, wananchi walifunga barabara kwa kuweka magogo na magunia ya mkaa wakishinikiza kujengwe matuta leo kabla ya kuruhusu magari kuendelea na safari.

"Tuko hapa na Mkuu wa Kituo cha Polisi na ofisa mtendaji tunajaribu kuwaomba wananchi wafungue barabara, sisi tumebeba dhamana ya kusimamia hiki wanachokitaka, wamekubali kufungua na sasa magari yanaendelea na safari,” amesema Diwani Abbas.

Akizungumzia muda wa barabara kufungwa, Abbas amesema wananchi hao waliifunga barabara hiyo kwa zaidi ya saa nne kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa mane mchana hali iliyosababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo kutoka na kwenda mikoa ya Kaskazini.

"Gari limeandikwa SU, hili ni la Serikali (Shirika la Umma),” amesema diwani huyo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema tayari wanalishikilia gari hilo kwa uchuguzi zaidi.

“Ni kweli gari hilo limemgonga na kumuua mwanafunzi na wakati Askari wa Usalama Barabarani alipokuwa anapima ajali, wakajitokeza wananchi wakafunga barabara, lakini wameshaifungua baada ya mazungumzo na gari tumelikamata tunaendelea kulichunguza zaidi kujua mmiliki ni nani,” amesema kamanda huyo.