Google Veo 3 yatajwa kupindua tasnia ya filamu duniani

Muktasari:
- Veo 3 inakuwezesha kuweka sauti, kuondoa kelele na hata mazungumzo kwenye ubunifu wa video yenye sauti asilia.
Dar es Salaam. Teknolojia ya Akili Mnemba inayotengeneza maudhui ya picha na video inazidi kushika kasi, baada ya kampuni ya Google kuja na toleo la programu (Generative AI) ya VEO 3 inayoweza kutengeneza video zenye sauti, mandhari, pamoja na mazungumzo ya wahusika.
Awali, wakati wa kuanza kwa Akili Mnemba, sehemu kubwa iliweza kutengeneza picha kisha video na sasa ni video zenye mazungumzo ingawa hakuna waigizaji. kamera bali ni Akili Mnemba pekee.
Ikumbukwe Akili Mnemba ni teknolojia inayowezesha kompyuta na mashine kuiga uwezo wa binadamu kama vile kujifunza, kufikiri, kufanya uamuzi, na kuwa na ubunifu. Katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, fedha, mawasiliano pamoja na utengenezaji maudhui.
Hata hivyo imetajwa hatua hiyo inaweza kusaidia sekta ya filamu katika uandaaji hata hivyo inaweza kutishia soko lake kwa kuwa uwezo wa video hizo ni mkubwa kuanzia, mandhari na wahusika ukilinganishwa na baadhi ya filamu halisi zinazoigizwa.
Teknolojia hiyo ya Veo 3 inashindana na nyingine ya kampuni ya OpenAI iitwayo Sora ikiwa ni mwendelezo wa kampuni hizo kubwa katika ushindani wa soko la teknolojia ya akili Mnemba.
Siku mbili zimepita tangu Google kutangaza kuja na Akili Mnemba ya mazungumzo ya Gemini kwenye kipengele cha kutafuta cha ‘Google Search’ ikiwa ni kushindana na ChatGPT ya OpenAI na huduma nyingine za Akili Mnemba, ambazo zinaitishia Google kwenye utafutaji wa mtandaoni
Ujio wa Veo 3, unatajwa kuwa ubunifu mkubwa ingawa unaweza kutishia kazi za wahusika wa kutengeneza maudhui wakiwemo waigizaji, wahariri na washika kamera.
kwa mujibu wa Google DeepMind na tovuti ya CNBC, Veo 3 inaweza kujumuisha sauti zinazojumuisha mazungumzo kati ya wahusika pamoja na sauti za wanyama.
"Veo 3 ina uwezo wa kuboresha kutoka kwenye maandishi na picha hadi video zenye sauti Eli Collins,” Makamu wa Rais wa bidhaa wa Google DeepMind, amenukuliwa.
Akizungumza na Mwananchi mwanamaudhui wa mtandao wa YouTube, Rashid Mansa amekiri kuwa hatua hiyo ni nzuri kurahisisha muda wa kusubiri filamu kwa muda mrefu kwa kuwa AI itaondoa kizingiti cha muda na teknolojia kwa wale wanaonunua kamera na vifaa vya maigizo.
Amesema ina faida kwa waigizaji nyota wenye majina makubwa watakopewa fursa za kutumiwa mionekano yao kwenye filamu zitakazoigizwa kwenye video hizo mpya.
“Lakini pia itakuwa kilio kwa waigizaji chipukizi ambao hawajatoka kwa sababu AI inatengeneza wahusika wa kufikirika wa aina mbalimbali. Pia wanaopata kazi ni wale watakaoingiza sauti kwenye video hizo,” amesema.
Amesema kwa upande wa wahusika wa kuandaa video wanapaswa kujifunza namna ya kutengeneza kupitia teknolojia hiyo kwa kuipa maelekezo sahihi ili itengeneze video wanazotaka.