Gozbert aeleza alichozungumza mara ya mwisho na Magufuli

Gozbert aeleza alichozungumza mara ya mwisho na Magufuli

Muktasari:

  • Msanii wa muziki wa injili nchini Tanzania, Goodluck Gozbert amesema mara ya mwisho kuzungumza na aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli alimpongeza na kumtaka azidishe juhudi, kauli ambayo hasi sasa imekuwa ikijirudia katika fikra zake.

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa injili nchini Tanzania, Goodluck Gozbert amesema mara ya mwisho kuzungumza na aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli alimpongeza na kumtaka azidishe juhudi, kauli ambayo hasi sasa imekuwa ikijirudia katika fikra zake.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Gozbert amesema mara ya mwisho kuzungumza na kiongozi huyo ilikuwa Aprili 2018 alipomualika katika uzinduzi wa taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Amebainisha kuwa alitumbuiza Ikulu na baada ya hafla fupi alizungumza na kiongozi huyo ambapo alimpongeza na kumtaka aongeze bidii.

 “Maneno aliyoniambia kiukweli yamekuwa yakijirudia mara kwa mara masikioni mwangu na hata sasa baada ya msiba kila ninapokumbuka tukio lile,” amesema Gozbert.

Amesema mwaliko aliopewa na Magufuli ulimpa heshima kubwa inayoendelea kumbeba hadi sasa.

Msanii huyo amesema siku mbili baada ya mwaliko huo, Magufuli alimpigia simu  na kumpongeza kwa album aliyompatia kama zawadi na kufurahi kwa kuwa katika maisha yake hakuwahi kufikiria kiongozi mkubwa wa nchi kama kuwa shabiki yake.

“Nilimpenda sana baba yangu huyu kifo chake kiukweli kimeniumiza sana kwani nimepoteza rafiki,  kiongozi ambaye ameacha alama kwenye maisha na muziki wangu ,”ameongeza Gozbert.