Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Grace mwanamke anayejivunia mafanikio katika uhandisi

Mhandisi Mwandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Grace Musita

Muktasari:

Mhandisi Mwandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Grace Musita amesema wasichana wengi wanashindwa kumudu masomo ya uhandisi kwa sababu ya kukatishwa tamaa wakielezwa ni magumu, hivyo hawataweza kufaulu.


Dodoma. Mhandisi Mwandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Grace Musita amesema wasichana wengi wanashindwa kumudu masomo ya uhandisi kwa sababu ya kukatishwa tamaa wakielezwa ni magumu, hivyo hawataweza kufaulu.

“Wasichana wana woga mwingi kutokana na kusikia, mtu anaambiwa hesabu ni ngumu na anaamini kuwa ni ngumu lakini si kwamba ni ngumu kweli,” alisema Grace alipozungumza na gazeti hili jijini Dodoma.

Alisema hata mwaka 2003 alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jumuiya ya chuo hicho ilikuwa imejijengea mazingira kuwa masomo ya uhandisi ni magumu, hivyo kuwafanya baadhi ya waliokuwa wameomba kozi hizo kuahirisha dakika za mwisho.

Hata yeye alisema alikutana na changamoto hiyo, akiwa msichana mdogo.

Alisema wanafunzi aliowakuta wakisoma masomo hayo walimweleza kuwa kuna wanafunzi zaidi ya 30 walifeli hivyo kumshauri naye achague kozi nyingine.

Grace alisema baadhi ya wanafunzi walikuwa wakisema kuna shahada za kubeba na shahada za kuzitafuta ambazo zilihusu masomo ya uhandisi.

“Wakawa wananiuliza ‘kwa nini msichana mdogo uje huku kwenye kutafuta, kwa nini usiende kwenye kubeba?’ lakini mimi nilikuwa napenda hesabu sana kwa hiyo sikuvunjika moyo wala kukata tamaa, niliendelea na masomo ya uhandisi kwa kuongeza nguvu na bidii,” alisema.

Hata upande wa vyoo, katika chuo hicho, alisema wakati anasoma vilikuwa vimeandikwa wanaume tu, hakukuwa na mlango ulioandikwa wanawake kama ilivyo ada katika maeneo mengine ya umma.

Hata hivyo, pamoja na changamoto zote hizo Grace alisema walikuwa wasichana wanane tu kati ya zaidi ya wanafunzi 150, lakini walimaliza 78, wakiwamo wasichana wote wanane.

Hata baada ya kuanza kufanya kazi alisema alikutana na changamoto ya mafundi kutochukulia kwa umakini maelezo aliyokuwa akiyatoa katika ujenzi.

“Utasikia uliona wapi wahandisi wanawake halafu wadogo. Lakini kwa sababu unajua hata chuo vitu hivyo vipo huwezi ukanuna au ukawasema ama kuwafukuza wala kuwashangaa, unawaelekeza tu mnaendelea na kazi,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzimaliza kwa ubora mkubwa uliosifiwa na watu, uliwafanya mafundi kuelewa kwamba hata wanawake wanaweza kwenye eneo hilo.

Anavyogawa muda wake         

Grace, mama wa watoto watatu, alisema changamoto aliyonayo ni kukosa muda mrefu wa kukaa na familia yake kutokana na kuhama hama kwenda ilipo miradi ya shirika.

“Nikienda katika mradi narudi mara mojamoja kuangalia familia. Hiyo ndiyo changamoto ya mama mhandisi, hutaweza kuwabeba watoto wakati wote, labda kabla hawajaanza shule,” alisema.

Hata hivyo, anamshukuru mumewe kwa kuyaelewa mazingira ya kazi zake, kwani ndiye anayekaa muda mrefu na watoto.

“Kazi zetu ni za hadi usiku, sasa asipokuelewa (mume) kutamwekea mazingira ya kuhisi tofauti. Wanavyosema zege halilali ni kweli, usipomaliza linatengeneza crack (mpasuko). Sio zege tu halilali hata miradi tunayoendelea nayo ina pressure kubwa, inatakiwa kukamilika kwa wakati,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kutoka kazini saa sita usiku ni jambo la kawaida, lakini mumewe analifahamu kwani katika miradi waliyokuwa wanaifanya jijini Dar es Salaam alikuwa anaiona hali halisi.

Hata hivyo, mhandisi huyo anasema uhandisi haimaanishi kuwa mbali na jamii au mambo ya imani hivyo yeye ni katibu wa kamati ya ujenzi ya Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmel Kihonda mjini Morogoro na ni mweka hazina wa Jumuiya ya Mtakatifu Theresa wa Avila Kihonda. Vilevile, alisema anasimamia na kuongoza kikundi cha Peace Women Group cha Morogoro pia.

Kilichomvutia kuwa mhandisi

Grace alisema tangu akiwa shule ya msingi hata sekondari alikuwa analipenda somo la hisabati.

“Nakumbuka wakati nikiwa Jangwani walinipa jina la Grace marking scheme kwa sababu tukifanya mtihani wa hesabu tukishapewa majibu ulikuwa unachukuliwa na wenzangu kwa ajili ya kufanya masahihisho. Namshukuru Mungu ni uwezo ambao alinipa, maksi zangu hazikuwa chini ya 95,” alisema.

Licha ya kufaulu somo hilo, Grace alisema alikuwa anapenda kufundisha wenzake na siku ya mtihani wa hisabati hakuwa na presha ya kujisomea, bali ya kuwafundisha wenzake.

Alisema hiyo ilimfanya wakati wa kuchagua kozi za kusoma chuo kikuu watu wamwambie anafaa kuwa mhandisi, ingawa awali alitamani kuwa mhasibu, taaluma ya baba yake. Maoni hayo ya watu wengine alisema yalimshawishi kuchagua kozi ya uhandisi, hivyo kuwa mmoja kati ya wanafunzi wawili waliotoka Sekondari ya Tabora.

Miradi mikubwa aliyoisimamia

Alipohitimu chuo kikuu alisema alichukuliwa kufanya kazi katika Kampuni ya Ujenzi ya Estim ambayo wakati huo ilikuwa inajenga Jengo la Amani Place Bulding lililopo Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.

Kati ya wahitimu watatu waliochukuliwa kwenda kusimamia mradi huo, alisema msichana alikuwa peke yake.

Mradi mwingine ambao Grace anajivunia ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya Serikali katika Mji wa Serikali wa Mtumba ambako NHC walijenga majengo ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Alisema mradi huo ulikuwa na presha kubwa na wa haraka kutokana na muda uliotakiwa kumalizika kuwa mfupi.

“Pale kweli dhana ya kufanya kazi usiku na mchana ilionekana kwa sababu ulikuwa unaingia kazini saa moja asubuhi na unatoka saa nane usiku. Ni jambo la kawaida kuja kukaguliwa saa sita usiku na wakaguzi kutoka wizara mbalimbali,” alisema.

Alisema mradi huo kwa kawaida ulitakiwa uchukue mwaka mmoja, lakini ulitekelezwa kwa ubora unaotakiwa kwa kufuata hatua zote zinazotakiwa ndani ya miezi mitano tu.

Mradi mwingine ni ujenzi wa nyumba 1,000 mkoani Dodoma ambapo NHC ipo katika awamu ya kwanza inayohusisha nyumba 404. Katika awamu ya kwanza alisema anasimamia ujenzi wa nyumba 101 za ghorofa nane kila moja huko wilayani Chamwino. Vilevile amesimamia ukarabati wa shule kongwe.

Maghorofa kuanguka

Iwapo utaratibu wa ujenzi utafuatwa, ikiwamo kupima udongo, kutumia vifaa bora na ukaguzi wa kila hatua, Grace alisema jengo la ghorofa haliwezi kuanguka.

Wakati wa ujenzi, alisema mhandisi haruhusiwi kwenda hatua nyingine bila uthibitisho wa ubora wa mhandisi wa halmashauri na msanifu majengo.

Grace alisema majengo mengi yanayoanguka ni yale yasiyo na usimamizi mzuri au ambayo baadhi ya hatua za ujenzi wake zinarukwa pengine kutumia vifaa visivyolingana na mahitaji.

“Kwenye miradi ya Serikali hicho kitu huwezi kukikuta (kutofuatwa na kuzingatiwa kwa utaratibu). Kwenye msingi tu wa jengo ukienda tofauti ni shida na kuna hatua za awali ambazo maclient (wateja) wanazikwepa kwa sababu ya gharama ndiko kunakosababisha majengo kuanguka,” alisema.