Gubu katika familia lazua mauaji

Thursday January 21 2021
By Aurea Simtowe
By Fortune Francis

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa linamshikilia Pendo Carlos kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kambo na kujaribu kuwaua wanaye wawili katika tukio linaloelezwa kuhusishwa na gubu la wakwe zake.

Pendo ambaye kwa sasa yupo mahututi katika Hospitali ya Sinza, Palestina baada ya kujaribu kuondoa uhai wake kwa sumu, anadaiwa kufanya mauaji hayo juzi mchana nyumbani kwake Tegeta A ambapo licha ya kumuua Belinda Carlos (17), pia aliwatumbukiza watoto wake Bertha (4) na Brighton (6) ndani ya shimo la kuvunia maji ya mvua.

Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio na kuwa wanamshikilia mwanamke huyo akiwa hospitalini kwa tuhuma hizo.

Akizungumza na Mwananchi jana, mdogo wake Pendo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema siku ya tukio akiwa katika duka analosimamia alipokea ujumbe kutoka kwa dada yake (Pendo) kuwa anataka kujiua yeye na watoto wake.

“Nilipopata ujumbe huo nilikimbia hadi nyumbani, nilipofika milango ilikuwa imefungwa nikaruka ukuta kuingia ndani, madirisha mengine yaligoma kufunguka, hivyo nikavunja moja kwa shoka,” alieleza.

Alisema mlango wa chumba cha dada yake ulikuwa umefungwa, hivyo aliuvunja na kukuta Belinda akiwa amepoteza maisha huku shingoni kwake kukiwa na mtandio na pembeni kukiwa na sumu ya kuua panya iliyokorogwa.

Advertisement

“Kuhusu wale watoto waliokuwa kisimani nilijua kupitia rafiki yake Pendo ambaye pia alitumiwa ujumbe akiambiwa sehemu walipo, hivyo jitihada za haraka za kuwaokoa zilifanyika na kwa sababu kulikuwa hakuna maji mengi walikutwa wazima,” alisema kijana huyo.

“Katika ujumbe ule alimwambia rafiki yake kuwa Belinda yupo chumbani kwake (Pendo) na wale wawili wapo kwenye kisima cha maji na mimi nimeshaenda kujiua,” alinukuu ujumbe huo.

Alisema kwa muda ambao walipokea ujumbe kutoka kwa dada yake, ilionekana tayari alikuwa amefanya kitendo hicho.

“Ninapofanyia biashara si mbali, ujumbe ungekuja kwa wakati ningemkuta. Chanzo cha haya yote ni mgogoro wa mali uliopo kati ya dada na familia ya mume wake,” aliongeza.

Alibainisha kuwa mgogoro huo ulianza baada ya mume wa Pendo Carlos Myakunga (52) kufariki dunia Mei 2020 kwa maradhi.

“Kabla ya kifo cha mumewe familia hizo zilikuwa zikiishi vizuri,” alisimulia kijana huyo.

Ili kumaliza mgogoro huo walikuwa wanasubiri maamuzi ya mahakama juu ya mirathi ya mume wa Pendo ambaye alikuwa mhasibu katika moja ya makampuni nchini.

Taarifa ya Polisi

Wakati mdogo wake akisimulia hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema jana kuwa taarifa ya tukio hilo ilitolewa na Roda Beda (ndugu wa mtuhumiwa) baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa mtuhumiwa (Pendo) uliosomeka kuwa “mdogo wangu nimeamua kujiua kwa sababu ya kunyanyaswa na wakwe zangu.”

Alisema baada ya Roda kupokea ujumbe huo alikimbilia nyumani na alipona hakuna dalili za kufunguliwa mlango alifanya jitihada za kuvunja geti na kuingia ndani.

“Baada ya kuingia ndani alikuta mwili wa binti wa mume wa dada yake aitwaye Belinda Carlos (17) umelazwa chini na wakati akiendelea kuchunguza chanzo ndio aliposikia kelele za watoto wakilia ndani ya shimo la kuvunia maji ya mvua na kuomba msaada kwa wananchi na kufanikiwa kuwatoa watoto wawili Bertha (4) na Brighton (6) wakiwa hai kutokana na shimo hilo kuwa na maji machache,” alieleza kamanda huyo.
  

Advertisement