Gwajima: Usawa wa kijinsia haubomoi taasisi ya ndoa, unaimarisha

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima wakati wa uzinduzi wa mradi wa 'Wanawake Sasa'unaolenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi ili kubadili fikra za kutambua uwezo sawa wa wanaume na wanawake katika katika uongozi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Wanajamii wametakiwa kuacha dhana potofu kuwa uwezeshwaji wa wanawake ni kisababishi cha kuvunjika kwa ndoa kwani ni mamlaka nyingine yenye utawala wake ambayo ni lazima kuitii na kuiheshimu.
Dar es Salaam. Jamii imehimizwa kuachana na dhana potofu kuwa kuwa uwepo wa usawa wa kijinsia katika masuala mbalimbali ikiwemo uongozi ni moja kati ya sababu inayopelekea kuteteleka kwa taasisi muhimu ya ndoa.
Wito huo umetolewa Septemba 19, 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima wakati wa uzinduzi wa mradi wa 'Wanawake Sasa' unaolenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi ili kubadili fikra za kutambua uwezo sawa wa wanaume na wanawake katika katika uongozi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Gwajima amesema uwezeshwaji wa wanawake kufikia usawa wa kijinsia haupelekei ndoa kuvunjika kama baadhi ya watu wanavyodhani.
"Nimekuwa nikisikia mahala kila wakitaja masuala ya usawa wa kijinsia minong'ono inaibuka kuwa 'ndio wanataka kuja kubomoa ndoa eeh' "
"Nilimsikia mama Mongela akisema ndoa ni taasisi kongwe na kipekee ambayo kanuni zake za uendeshaji haziingiliani na mambo mengine"amesema.
Amesema ndoa ni mamlaka nyingine yenye utawala wake ambayo ni lazima kuitii na kuiheshimu.
"Ukienda kuibomoa ndoa kwa kuwa umepewa nafasi ya kuwa kiongozi na kuwezeshwa ni kwa utashi wako na wala siyo lengo la kupigania usawa wa kijinsia"anasema.
Amesema kuwa lengo ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na siyo kuwakandamiza wanaume.
"Hata mimi nimeolewa na sichanganyi mambo, nikifika kule nina kiongozi wa taasisi ambaye ninapaswa kumuheshimu, watu wengi wanajichanganya hapa naomba kupitia huu mradi uongeze uelewa katika hili"amesema.
Ameongeza kuwa kuna haja ya elimu kuendelea kutolewa kwa wanaume na wanawake ili kila mmoja aweze kutekeleza majukumu yake huku heshima ya asili kati ya baba na mama katika familia zisibomolewe.
"Tusipoongea mambo haya kwa msisitizo tutakuwa tunatengeneza wanawake ambao wamepotoshwa na watu wengine ambao wanataka kuvuruga mwisho kunapelekea kutokea kwa migogoro katika familia ambayo inasababisha changamoto mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani"amesema.
Pia Gwajima amehimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombania nafasi mbalimbali za uongozi.
Ameesema Tanzania imekuwa ikifanya jitihada ya mbalimbali katika kuwezesha usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha inamaliza vikwazo vinavyoleta ugumu katika utekelezaji wa jambo hilo.
Amesema miongoni mwa hayo ni pamoja na kutambuliwa kwa kosa la ukatili wa kijinsia kwenye uchaguzi Violence Against Women in Elections (VAWE) kama kosa la uchaguzi.
"Kifungu nambari 135 kinatambua kosa la unyanyasaji wa jinsia kama kosa la uchaguzi. Katika hili, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kutambua kosa la Ukatili wa Kijinsia kwenye Chaguzi Violence Against Women in Elections (VAWE) kama kosa la uchaguzi"amesema.
Hata hivyo wakati wa uwasilisho wa mada Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Zanzibar, Siti Ali alisema pamoja na kumuhamasisha mwanamke kushiriki katika nafasi mbalimbali ni muhimu kwanza kuhakikisha anawezeshwa kiuchumi pamoja na kujengewa uwezo wa uongozi ikiwemo kuzungumza mbele ya watu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WILDAF), Anna Kulaya amesema mradi wa Wanawake Sasa unatarajia kuleta mabadiliko makubwa ya kifikra, mitazamo, mifumo, sera na sheria ili jamii itambue kuwa suala la Wanawake na Wasichana kushiriki katika siasa, uongozi na michakato yote ya demokrasia ni la msingi na ni haki yao ya kikatiba.
"Ni haki yao kuwa viongozi, ni haki yao kushiriki michakato ya demokrasia, ni haki yao kuchagua au kuchaguliwa kuwa viongozi katika ngazi zote za maamuzi."amesema.