HABARI MAALUMU: Miaka 32 ya maisha jela, ndugu waliamini alishanyongwa

Robert Moringe

Muktasari:

Ilikuwa Februari 26 mwaka 1993 siku ambayo ndoto za maisha ya Robert Moringe zilizimika, baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, kufuatia kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji.

Arusha. Ilikuwa Februari 26 mwaka 1993 siku ambayo ndoto za maisha ya Robert Moringe zilizimika, baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, kufuatia kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji.

Moringe ambaye wakati huo, alikuwa kamanda wa kikundi cha ulinzi jamii (sungusungu) eneo la Esso katika Jiji la Arusha, alitiwa hatiani baada ya kutuhumiwa kushiriki katika mauaji ya mtuhumiwa wa ujambazi aliyechomwa moto.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi jijini Arusha, Moringe anasimulia kukamatwa kwake, kesi ilivyokuwa, maisha gerezani, kutoka kwake na namna wanafamilia akiwamo mama yake mzazi walivyomsahau mpaka akalazimika kuwaonyesha vyeti kuwa ni yeye Robert Moringe na sasa yuko huru.

Imani ya familia yake ni kuwa ndugu yao alikwishanyongwa miaka mingi, hivyo kumuoana akiwa hai halikuwa suala rahisi kwao kukubaliana na uhalisia huo.


Kukamatwa

Anasema anakumbuka alikamatwa Februari 1990 akiwa na wenzake watatu, wakituhumiwa kwa mauaji.

“Baada ya kukamatwa, nilikwenda polisi nikaandika maelezo kwa sababu sikuwepo siku ya tukio, niliachiwa na kurejea nyumbani,” anasema.

Hata hivyo, alisema baadaye alikamatwa tena kwa madai yeye kama kiongozi wa sungusungu alikuwa na uwezo wa kuzuia kuuawa kwa Michael na ilikuwa Oktoba 22, 1990 ambapo kesi ilifunguliwa.

Moringe anasema wakati huo, alikuwa na miaka 24 na mahakamani alijitetea kuwa hakuwepo siku ya tukio ambalo wananchi walimkamata mtuhumiwa na kisha kumchoma moto.

“Nakumbuka kipindi kile kulikuwa na matukio mengi ya ujambazi katika Jiji la Arusha, watalii walikuwa wanakwapuliwa vitu barabarani, nyumba zinavamiwa, maduka na maeneo mengine yanaibiwa hivyo mitaa mingi ilikuwa na sungusungu,” anasema.

Anakumbuka baadhi watuhumiwa wa ujambazi, walikuwa na chuki na viongozi wa sungusungu wa eneo la Esso na baada ya tukio hilo, waliungana na kuhakikisha wanapoteza kabisa.

“Nakumbuka wakati nasubiri hukumu takribani mwezi mzima sikupata usingizi gereza la Kisongo Arusha na siku ya hukumu nakumbuka alinihukumu Jaji Daniel Matias Nshala,” anasema Moringe.

Anasema siku hiyo alieleza vizuri tukio lilivyotokea kuanzia kukamatwa kwa mtuhumiwa na kisha wananchi kuamua kumchoma moto bila ya yeye kuwapo.

Anasema kuwa Jaji alieleza licha ya maelezo yake hayo, hakuona sababu ya kumwachia huru, kwani kama kiongozi alikuwa na fursa ya kuzuia mtuhumiwa kuuawa, lakini pia kama angemwachia, kungeonekana kuna mazingira ya rushwa.

“Nakumbuka wakati ile kesi ilipokuwa ikiskilizwa, kila mara zilitolewa taarifa mahakamani kuwa nimetoa rushwa. Pia ilidaiwa eti silali gerezani, nalala nyumbani hivyo mazingira hayo yaliharibu ile kesi,” anasimulia.


Miaka 10 baada ya hukumu

Moringe anasema baada ya hukumu hiyo ya Jaji Nshala alikata rufaa, lakini hakuwahi kusikilizwa ila baada ya miaka 10, Tume ya Haki za Binadamu, ilitembelea Gereza la Maweni lililopo Tanga ambako alikuwa amefungwa kusubiri kunyongwa na alieleza nia yake ya kukata rufaa.

Anasema nyaraka za rufaa ambazo alikata zilielezwa kupotea, lakini baadaye zilionekana baada ya tume kufuatilia kwa umakini.

“Rufaa ilipangwa kufanyika Mahakama ya Rufaa Arusha, lakini sikuwahi kusikilizwa kutokana na kukosekana usafiri wa kunipeleka mahakamani kutoka Tanga,” anasema.

Anasema hadi ilipofika siku ya hukumu ya rufaa yake, ambayo ilisikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na marehemu Jaji Augostino Ramadhani hakuwepo na siku anafikishwa Arusha alielezwa tayari rufaa yake imetupwa.

“Baada ya kupata hizo taarifa kutupwa rufaa yangu, sikuwa na njia nyingine ya kukwepa adhabu, nilibaki kulia na kuchanganyikiwa nikiamini nasubiri kunyongwa tu.”

Anasimulia kuwa alikwenda na kutumikia kifungo akisubiri kunyongwa na baadaye alihamishiwa Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, mwaka 2006.


Maisha ya wafungwa

Anasema wafungwa ambao wanasubiri kunyongwa kwa siku hupewa dakika 15 tu za kutoka nje na muda mwingi hubaki ndani.

“Kwa kuwa wanakuwa wengi gerezani, basi kuna baadhi wanaweza kukaa muda mrefu bila kuona hata jua na baadhi wamefikia hatua ya kuchanganyikiwa kutokana na msongo wa mawazo,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Moringe, kila anapokumbuka matukio hayo, hupatwa huzuni hasa anaposikia mtu amefanya mauaji dhidi ya mwingine kwa sababu yoyote ile ikiwamo wivu wa mapenzi.

“Kama utashughudia maisha ya gerezani kwa watuhumiwa wa mauaji, sidhani kama utathubutu kuua mtu, kwani damu ya mtu haiwezi kupotea bure ni lazima utajutia tu.

“Ukiwa kule mwisho wa kukaa macho usiku ni saa tatu hivyo unapaswa kuwa kimya na kulala japo unalala katika kipande cha blanketi moja umetandika chini na jingine unajifunika.

“Nakumbuka kutokana na upweke na kuchanganyikiwa, kuna wakati ulitokea ugomvi, mfungwa mmoja kudai wenzake wanamloga hivyo, kuanza kupigana hadi viongozi wa magereza wakajitokeza na kutoa adhabu,” anasema.


Ahamishwa gereza

Baada ya kutumikia kifungo chake akiwa Gereza la Ukonga, mwaka 2008 alihamishiwa gereza la Lilungu, Mtwara

Moringe anaeleza baada ya kufikishwa gerezani hapo, yeye ndiye alikuwa mfungwa aliyekaa jela kwa mrefu zaidi.

Kutokana na hilo, wenzake walimpenda kwa sababu alikuwa akiwapa ushauri wakati wote wanapohitaji msaada.

“Tuliishi vizuri na walinichagua niwe kiongozi wao wa kupeleka malalamiko na shida zao kwa viongozi wa gereza, kazi ambayo nilifanya vizuri na kuondoa migogoro katika gereza letu,” anasema.

Hata hivyo, anasema changamoto kubwa ilikuwa ni baadhi ya wafungwa waliohukumiwa kunyongwa ambao baadhi walikuwa wamechanganyikiwa na hivyo kuwa wakorofi.


Apata msamaha wa Rais

Moringe ambaye hadi anakwenda gerezani hakuwahi kuwa na mtoto wala mke, anasema Aprili 26, 2020 kutokana na mwenendo wake mzuri gerezani, alikuwa ni miongoni mwa wafungwa 226 waliobahatika kupata msamaha wa Rais John Magufuli.

“Baada ya ule msamaha, tuliambiwa tutapewa namba kwa sababu tumeondolewa adhabu ya kifo, hivyo tutakaa tena miaka 10 gerezani kwa kifungo cha kawaida,” anasema huku akieleza kuwa alijitahidi kuandika barua kukumbushia msamaha wake, bila mafanikio hadi Desemba 12, 2021 wakati Bodi ya Magereza ilipofanya ziara kwenye Geraza la Lilungu na akapata fursa ya kuzungumza.

Anasema akiwa anatumikia kifungo alipata furaha ya ajabu ambayo hakuwahi kuifikiria April 26, 2022 alipopewa taarifa kwamba, ni miongoni mwa wafungwa waliopata msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nakumbuka siku hiyo nikiwa katika majukumu yangu ndani ya gereza, niliitwa na kuelezwa nimepata msamaha na kutakiwa kujiandaa kurudi nyumbani Arusha,” anasema.

Anasema alianza kuwaza siku ikifika na ndipo aliandikiwa kibali cha kutoka gerezani na Mei Mosi alipewa nauli kwenda Dar es Salaam na baadaye Arusha.

“Nakumbuka nilipewa nauli na Sh 10,000 ya kula, baada ya kufika Dar es Salaam nililala stendi ya Magufuli na siku iliyofuata nilipanda basi la kwenda Arusha,” anaeleza Moringe.

Akiendelea kusimulia, anasema akiwa kwenye gari, alikaa kiti jirani na mtangazaji maarufu Abdalah Majura, ambaye alikuwa anakwenda Arusha katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari.

“Nilimjua Majura kwa sababu nilipokuwa nimefungwa Ukonga niliwahi kuzungumza naye na kumpa shida zetu na alitangaza BBC mwaka 2007 ile habari hivyo, alipokuwa anazungumza na kujitambulisha ndipo nilimjua na kumsalimia,” anasema.

Anasema Majura alifurahi kukutana nami na baada ya kufika Arusha, walipiga picha ya ukumbusho.


Akuta mabadiliko Arusha

Moringe anasema baada ya kufika Arusha, alishuka mwisho wa basi saa 10:30 jioni na akamsikia abiria mmoja anakwenda eneo la Unga Ltd, akaomba aende naye na wakaondoka pamoja.

“Mambo mengi sikuyaacha Arusha, barabara nyingi zilikuwa za vumbi, nimekuta zina lami, kuna majengo mengi mapya hivyo nilikuwa naona kama miujiza tu,” anasema.

Alipofika eneo la Unga Ltd Nguzo mbili, alikumbuka kidogo na alimuona mzee mmoja na akamuuliza kama anawafahamu ndugu zake ambao, walikuwa wakiishi eneo la Terati.

“Bahati nzuri yule mzee alisema anamjua mama yangu ila wamehama Terati na kwenda Sombetini na akaniuliza kama nina simu nimpigie mama yangu, nikamwambia sina kisha yule mzee alinipa namba,” anasema.

Anasema baada ya hapo alianza kuelekea eneo la Sombetini na akiwa njiani alikutana na mwanamke mmoja na alimuomba simu apige nyumbani kama alivyoelekezwa na yule mzee.

“Yule dada alichukuwa ile namba na kupiga nyumbani na alipokea mama na alimueleza kuna mtoto wake anataka kuja kumuona, ila mama yake alisema hamkumbuki kwani huyo mtoto alikwishanyongwa siku nyingi,” anasema.


Mama, dada wamsahau

Baada ya kufika nyumbani kwa mama yake, Mwanaisha Athuman Salim (87) alivyomuona hakumkumbuka kabisa.

“Mama alimuita mdogo wangu wa kike Jackline Edward (42), ambaye baada ya kumtaka anitambue pia alisema hanikumbuki na mama alimweleza mimi ni kaka yake Robert ambaye nilihukumiwa kunyongwa mwaka 1993,” anasema Moringe na kumtaja mdogo wake mwingine ambaye yupo hai kuwa ni Ester Edward (47).

Anasema baada ya utambulisho aliwaonesha hati ya kuachiwa magereza, walianza kulia wote nyumbani, lakini aliwaomba watulie ili watu wasijae kudhani kuna msiba na kuzua tafrani.

“Baada ya hapo, tulikaa na kuanza kuelezeana ambapo nilielezwa wadogo zangu, watatu tayari wamefariki, Leonard alifariki mwaka 2020, Ester mwaka 1998 na Alphonce mwaka 2004,” anasema.

Anasema yeye ndiye alikuwa mtoto wa kwanza, hivyo wamebaki wadogo zake wawili Jackline na Angelina.

Moringe anasema kwa sasa anaishi maisha ya shida kwani hajui nini cha kufanya kwa sasa, baada ya kupoteza kila kitu na mwelekeo wa maisha yake.

“Sijui nifanye nini kwani wakati nafungwa nilikuwa na uwezo kidogo wakiwamo ng’ombe tisa, lakini mjomba wangu alikwisha wauza na tayari alifariki,” anasema.

Anasema kwa sasa anaomba watu kumsaidia kuanza upya maisha, kwani anataka kuanza maisha upya ikiwamo kuoa ili awe na familia yake.

“Nilifungwa nikiwa na miaka 24 tu sikuwa hata na mtoto na sasa sina hata rafiki mmoja, ambaye namfahamu zaidi ya mama na wadogo zangu wa kike hivyo naomba msaada nianze maisha mapya,” anasema.

Anasema kwa mtu ambaye anataka kumsaidia anapatikana namba 0782948791 na 0757171910 ambazo zimesajiliwa kwa jina la Asia Said.

“Hadi sasa nimeshindwa kuwa na simu yenye usajili wa jina langu kwani sina kitambulisho cha Nida na bado najitahidi kutafuta msaada ili nipate hicho kitambulisho ila kwa sasa hizo namba natumia muda wote,” anasema.

Anasema ujuzi pekee ambao anao ni ufundi wa magari na udereva hivyo akipata msaada anaweza kuanza upya kuendesha maisha yake.

Akizungumza na gazeti hili, mama yake alisema anamshukuru Rais Samia kwa kumsamehe mwanaye kwani alijua tayari ameshanyongwa.

“Mimi sina cha kufanya, namshukuru Mungu na Rais mtoto wangu kumuona tena baada ya kuwa magereza kwa miaka mingi,” alisema

Kwa upande Jackline pia alisema wanaishukuru Serikali kumwachia kaka yake na sasa ameungana na familia.


Amemuachia Mungu

Anasema baada ya kutoka gereza ni salama baada ya miaka 32, yote yaliyopita anamuachia Mungu, kwani hana wa kumshitakia na sasa anaomba kuwa balozi wa amani nchini.

“Nipo tayari kutumiwa na Serikali na watu wengine kutoa elimu ya watu kuacha kufanya uhalifu ikiwamo mauaji kwani najua shida ambazo watapitia,” anasema.

Anasema atakuwa akitoa elimu katika nyumba za ibada na kwenye makundi ya vijana, ili waishi maisha mema na kutovunja sheria.


Walichokisema LHRC

Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), Mkoa wa Arusha, wakili Hamisi Mayomba anasema mkasa wa kesi ya Moringe ni mfano tosha wa kupinga hukumu ya kifo.