Hakika TRA wabuni mikakati kukusanya kodi

Hakika TRA wabuni mikakati kukusanya kodi

Muktasari:

  • Aprili Mosi wakati akiwaapisha mawaziri, manaibu mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Samia Suluhu Hassan alikonga si tu nyoyo za wafanyabiashara, bali hata Watanzania wa kada zote.

Aprili Mosi wakati akiwaapisha mawaziri, manaibu mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Samia Suluhu Hassan alikonga si tu nyoyo za wafanyabiashara, bali hata Watanzania wa kada zote.

Rais alifanya hivyo kupitia ile kauli yake ya kutaka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi zilizo chini yake, ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya ubunifu katika kukusanya kodi badala ya kutumia mabavu na kuchukua fedha za wafanyabiashara ambao mwisho hufunga biashara zao.

Sisi Mwananchi tumeifananisha kauli hii ya Rais Samia ambayo kwa hakika ni agizo, sawa na msumari wa moto uliogongwa sehemu na wakati sahihi.

Kwa muda mrefu, baadhi ya wafanyabiashara wamepaza sauti kulalamika kuwa watendaji wa TRA wanatumia nguvu kudai kodi badala ya kutengeneza na kupanua wigo wa walipa kodi.

Katika malalamiko yao, baadhi ya wafanyabiashara walidai kuna maofisa wa TRA waliokuwa wakiongozana na askari kutoka vyombo vya ulinzi na usalama walifunga biashara na akaunti zao benki, kutaifisha mali na fedha na hata kutoza kodi zisizostahili.

Baadhi ya wafanyabiashara walijikuta wakiingia kwenye migogoro ya kibiashara na kimikataba baada ya kushindwa kukamilisha malipo kwa akaunti zao kufungwa na TRA wangali bado wako kwenye majadiliano kuhusu makadirio waliyopewa.

Kwa kauli yake mwenyewe, huku akipigiwa makofi na viongozi na watendaji wa Serikali na taasisi zake ambao baadhi yao walikuwa watekelezaji wa vitendo hivyo, Rais Samia alisema mwenendo wa sasa wa ukusanywaji kodi wa kutumia nguvu nyingi badala ya akili na maarifa ni wa kuua walipa kodi na wafanyabiashara.

Huku akimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba kusimamia mambo yote yanayopunguza ari ya kulipa kodi, Rais Samia alisema vitendo hivyo si tu vinaua biashara, bali pia vinasababisha wafanyabiashara kuhamishia biashara zao nchi jirani.

“Sasa wale mnaowakamua na kuchukua vifaa vyao vya kazi na kufungia akaunti zao, mkachukua pesa kwenye akaunti kisa sheria inakuruhusu kufanya hivyo; akitoka hapo anakwenda kufunga biashara anahamia nchi ya pili. Mnapunguza walipa kodi,” alisema Rais Samia.

Japo aliunga mkono maelekezo ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ya kuongeza makusanyo kufikia wastani wa Sh2 trilioni kwa mwezi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, lakini Rais Samia aliagiza jambo hilo lifanyike kwa kuongeza wigo wa kodi na idadi ya walipa kodi.

Ni dhahiri kauli ya Rais Samia imekuja kama zawadi kwa wafanyabiashara katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka kwa sababu kilio chao cha muda mrefu siyo tu kimesikika, bali pia kimefika sehemu na kwa mtu mwafaka hivyo ufumbuzi sasa utapatikana.

Tunachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Rais Samia kwa kauli yake ambayo kwa hakika inakwenda kuponya na kufufua sekta ya biashara, hivyo kuongeza wigo wa kodi na uwekezaji nchini.

Kwa kauli hii, Rais ameleta matumaini mapya kwa kuwaondolea woga wafanyabiashara. Hakika TRA sasa waende kubuni mikakati mipya na kuongeza vyanzo vya kukusanya kodi ili kufikia malengo.

Tuna imani viongozi na watendaji waliopo katika sekta hiyo, watatatua changamoto zilizopo ili wafanyabiashara wasifunge biashara, badala yake walipe kodi na waendelee kufanya biashara kwa maendeleo yao na Taifa kwa jumla.