Hakimu aomba vielelezo kesi inayowakabili viongozi wa Serikali

Muktasari:

  • Upande wa Jamhuri katika kesi ya ubadhilifu wa fedha za umma zaidi ya Sh8.4 trilioni inayowakabili baadhi ya mawaziri na wakuu wa taasisi wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wapewe nakala ya maombi na viambatanishi ili waweze kuwasilisha kiapo kinzani.

Dar es Salaam. Upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na Jamhuri katika kesi ya ubadhilifu wa fedha za umma katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zaidi ya Sh8.4 trilioni inayowakabili baadhi ya mawaziri na wakuu wa taasisi wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wapewe nakala ya maombi na viambatanishi ili waweze kuwasilisha kiapo kinzani.

 Pia wameiomba mahakama hiyo wapewe siku saba ili waweze kuwasilisha kiapo kinzani.

Mtanzania, Thomas Nkola maarufu 'mkulima' amefungua maombi hayo ambapo anataka kuwashtaki Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, January Makamba, Profesa Makame Mbarawa.

Wengine ni  Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, Emmanuel Tutupa, Japhet Justine, Maharage Chande na Habinder Sigh Seth.

Nkola akiwakilishwa na Wakili, Penina Ernest alifungua maombi matano katika mahakama hiyo kati ya hizo tatu zimetajwa kwa mara ya kwanza leo Mei 29, 2023 shauri namba 17/2023 ipo kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, kesi namba 14/2023 kwa Huruma Shaidi na namba 13/2023 ipo kwa Pamela Mizengo.

Wajibu maombi hao wakiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Saraji Iboru na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patric Mwita na Tulimanywa Majigo walieleza mahakama hiyo kuwa maombi hayo yamekuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita aliomba mahakama hiyo wapewe nakala ya maombi na viambatanishi Ili waweze kuwasilisha kiapo kinzani.

"Tunaomba upande wa watoa maombi watuletee viambatanishi vyote kwa kuwa kuna wajibu maombi wametajwa wameisababishia taifa hasara tunahitaji nakala zote kama zilivyo msije mkachomoa karatasi kwenye ripoti ya CAG.

Baada ya maelezo hayo mahakama hiyo imemtaka wajibu maombi wawasilishe viapo kinzani ndani ya siku saba huku mtoa maombi ametakiwa awasilishe viambatanishi vyote vinavyohusiana na maombi ya shauri hilo.

Shauri namba 14/2023 lililopo mbele ya Hakimu Shaidi limeahirishwa hadi June 8, 2023 Kwa ajili ya kutajwa na shauri namba 17/2023 lililopo mbele ya Hakimu Mrio limeahirishwa hadi Juni 12, 2023 huku shauri namba 13/2023 lililopo mbele ya Hakimu Mizengo limeahirishwa hadi Juni14, 2024 kwa ajili ya kutajwa.

Katika maombi namba 17/2023 iliyotajwa mbele ya Hakimu, Mrio ya ubadhirifu wa fedha za umma katika ripoti ya CAG inayowakabili Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Waziri Dk Nchemba na Profesa Mabarawa pamona na Tutuba na Justine.

Katika maombi namba 14/2023 iliyotajwa mbele ya hakimu, shahidi ya ubadhilifu wa fedha hizo inayowakabili

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Makamba, Chande na Seth.

Maombi namba 13/2023 iliyotajwa mbele ya Hakimu,Mazengo ya ubadhilifu wa fedha hizo inayowakabili Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,waziri Dk Nchemba na Profesa Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Kadogosa.

Wakili wa kujitegemea anayemwalisha, Nkola alidai kwenye kesi  zote, mteja wake anadai watu hao wamefanya ubadhilifu wa fedha za umma hatua za kisheria zichukuliwe ikiwezekana warudishe fedha hizo au wafilisiwe.

Alidai katika ripoti ya CAG ya Mwaka 2021/2022 Dk Mwigulu, Tutupa na Japhet wanatuhumiwa kukopa fedha Sh1.2 trilioni kinyume na bajeti bila ridhaa ya Serikali ambapo inapatikana katika ukurasa 55 na 56 wa ripoti hiyo.

Pia, alidai katika ukurasa wa 32 na 33 wa ripoti ya CAG Makamba, Chande na Seth wanatuhumiwa kuisababishia hasara ya Sh342 bilioni.

Katika makosa ambayo mteja wake aliyofungua katika maombi hayo ni kula njama, kuiba fedha za umma, uhujumu uchumi na kusababishia Serikali hasara, matumizi mabaya ya ofisi na kupuuza amri za mahakama.