Hakimu kesi ya kina Zumaridi agoma kujitoa

Mshtakiwa namba moja katika kesi ya Jinai namba 12/2022 Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi akiwa ndani ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza kusikiliza kesi inayowakabili. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Katika maombi yaliyowasilishwa Jumatano Novemba 9, 2022 na jopo la mawakili wa utetezi, washtakiwa walimtaka hakimu ajiondoe kwa kile walichotaja kuwa ni kukosa imani naye baada ya kuonekana akichana karatasi wakati kesi ikiendelea bila kueleza nini kinachochanwa na nini kitaandikwa.

Mwanza. Hakimu anayesikiliza kesi ya Jinai namba 12/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake 83 ametupilia mbali maombi ya upande wa utetezi ya kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwa kile alichodai hayana mashiko kisheria.

  

Katika maombi yaliyowasilishwa Jumatano Novemba 9, 2022 na jopo la mawakili wa utetezi, washtakiwa walimtaka hakimu ajiondoe kwa kile walichotaja kuwa ni kukosa imani naye baada ya kuonekana akichana karatasi wakati kesi ikiendelea bila kueleza nini kinachochanwa na nini kitaandikwa.


Pia, washtakiwa hao walidai hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Clescensia Mushi hakuwasomea ushahidi waliyotoa mashahidi watatu katika kesi ndogo iliyoibuka ndani ya kesi ya msingi kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 210 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) ya mwaka 2019.


Akisoma maamuzi kuhusu maombi ya washtakiwa kumtaka ajitoe kwenye kesi hiyo, Hakimu, Mushi amesema baada ya kupitia Sheria, Miongozo na Kanuni za mahakama amejiridhisha kuwa hayana mashiko wala hayakidhi kumfanya ajitoe kusikiliza kesi hiyo.


Huku akinukuu kesi ya marejeo ya Mahakama ya Rufaa kati ya Isack Mwamasita dhidi ya CRDB Bank ya mwaka 2016, Hakimu Mushi amesema kesi hiyo iliainisha zinazoweza kumfanya hakimu ajitoe kusikiliza kesi kuwa ni endapo hakimu ana mahusiano ya karibu na upande mmoja au zote katika kesi husika.


Ametaja sababu nyingine kuwa ni endapo hakimu ni mwanafamilia au ana maslahi katika matokeo ya kesi na kama shahidi aliyeletwa mahakamani ana uhusiano wa damu na hakimu anayesikiliza kesi hiyo.


"Sababu zilizoelezwa na wakili Kitale katika mwenendo wa kesi hii hazioani na sababu zilizoainishwa kumfanya hakimu ajitoe kusikiliza kesi kwa hiyo sitajiondoa katika kesi hii," amesema hakimu, Mushi


Kuhusu suala la kuchana karatasi, Mushi amesema suala la kuchana mwenendo wa kesi ni kosa la jinai hivyo upande wa utetezi ulipaswa kuthibitisha kwa namna gani karatasi za mwenendo wa kesi zimechanwa na taarifa zilizopotea baada ya zilipochanwa.


"Suala la kuchana karatasi za mwenendo wa kesi ni kosa la jinai halimuachi wakili au hakimu salama ikithibitika iko hivyo. Lakini Wakili Kitale anaposhindwa kuthibitisha jambo hilo tafsiri yake ni kwamba anaweza kuangukia kwenye kesi ya jinai kwa sababu ni tuhuma" amesema


Mushi amesema katika kesi ya madai namba 118/2006 kati ya Bahati Makijaa dhidi ya Jamhuri iliyotolewa uamuzi mwaka 2010 katika Mahakama ya Rufaa hukumu yake ilieleza kuwa mahakama ina wajibu wa kuwaeleza mashahidi haki yao ya kusomewa maelezo ya ushahidi japo siyo lazima.


"Makosa yanafanywa na binadamu hata katika kesi ya Bahati Makijaa dhidi ya Jamhuri kulikuwa na makosa ya kutosoma maelezo ya ushahidi yalitokea lakini kesi iliendelea, pia wakili Kitale ulitakiwa kuikumbusha mahakama kuhusu kipengele hicho," amesema


"Sababu zilizotolewa na Kitale hazina mashiko, natupilia mbali maombi ya washtakiwa kwa sababu hayana miguu ya kisheria ya kusimama hivyo nitaendelea kusikiliza kesi hii na maamuzi haya hayana rufaa," amesema Mushi


Kesi hiyo yenye shtaka la kufanya kusanyiko lisilo halali imeahirishwa hadi Novemba 15 mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.