Halmashauri yapewa siku 14 kung’arisha Jiji la Mbeya

Muktasari:

  • Kauli hiyo imekuja baada ya wananchi katika eneo la Kabwe kuwasilisha kero ya uchafu na uwepo wa wamachinga katika mkutano wa CCM ikiwa ni maadhimisho ya miaka 47 ya chama hicho. 

Mbeya. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amemtaka Mkurugenzi wa jiji hilo, John Nchimbi kumaliza kero ya uchafu unaowakabili wananchi ndani ya siku 14, ikiwa pamoja na ununuzi wa magari ya kuzolea taka.

 
Pia ameitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (machinga) katika stendi ya daladala ya Kabwe jijini humo kufikia Februali 30 mwaka huu.


Kauli hiyo imekuja baada ya wananchi katika eneo la Kabwe kuwasilisha kero ya uchafu na uwepo wa wamachinga katika mkutano wa CCM ikiwa ni maadhimisho ya miaka 47 ya chama hicho. 


Akizungumzia katika mkutano huo leo Februari 2, 2024, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John Nchimbi amekiri jiji hilo kuwa miongoni mwa majiji machafu nchini, akiitaka kampuni ya Suma JKT waliyoingia nayo mkataba kuhakikisha hali ya usafi inapatikana.


Kuhusu kununua magari ya kukusanyia taka, Nchimbi amesema suala hilo linawezekana na litawekwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.


"Suma JKT ndio tuliwapa zabuni kwa kata tano za jiji na kulikuwa na tatizo la vifaa, lakini wanatarajia kuongeza magari kufika saba ili kuona usafi unarejea jijini hapa," amesema Nchimbi.


Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Mwalunenge amesema haridhishwi na utetezi wa Nchimbi, akishauri kuwa halmashauri hiyo kununua magari ya kuzolea taka.


"Hayo majibu yako yanafikirisha sana Mkurugenzi (Nchimbi), ina maana kwa uwezo wa halmashauri haiwezi kununua magari yakazoa hizi taka na kutengeneza faida, kuliko hizi kampuni ambazo zinaonekana kushindwa.


"Wewe ni kijana na umeletwa hapa kwa mkakati, tunaona nguvu na uwezo ulionao, iweje suala la  uchafu iwe kero kila maeneo ya jiji, sisi kama chama (CCM) tunatoa siku 14 uchafu uishe na Tarura (Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini) hakikisheni barabara zote zinapitika," amesema Mwalunenge.


Kuhusu suala la wamachinga kufanyia shughuli zao kwenye eneo la stendi ya daladala Kabwe, Mwalunenge amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa hadi kufikia Februari 30, 2024 kuwaondoa eneo hilo na kuwapeleka sehemu yao uwanja wa ndege wa zamani 'Old Airport'.


Awali akiwasilisha kero katika mkutano huo, mfanyabiashara Madenge Mfukuzasimba amesema waliopangisha kwenye soko la Sido hukosa wateja kutokana na shughuli nyingi kuishia nje ya soko walipo wamachinga.


"Ikifika mchana hadi jioni barabara ya kuingia sokoni inafungwa shughuli zote zinahamia hapa Kabwe, sisi tunalipa kodi sasa mwisho wote tutahamia hapa ili kutafuta riziki," amesema Mfukuzasimba.


Kwa upande wake, DC Malisa amesema wanasubiri kukamilika kwa barabara ya Vunjabei, Februari 28 mwaka huu watatekeleza maelekezo hayo ili kuondoa changamoto ya wafanyabiashara waliopo soko la Sido kukosa wateja.


Ktika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Serikali imetenga zaidi ya ekari 52,000 katika Halmashauri ya Chunya kwa ajili ya kilimo akiwataka vijana wenye nia na uhitaji wa kilimo cha soya kufika ofisi ya Mkurugenzi na Mkoa kujiorodhesha.


"Mazingira ya lile eneo hayajawa mazuri kutokana na miundombinu ya barabara, ambapo tunashirikiana na Benki ya Dunia (WB) kujenga njia, ila kama vijana wataweza kutumia usafiri wa pikipiki waje kujiorodhesha wapatiwe eneo hilo ambalo lipo katika mpango wa ‘Jenga kesho iliyo njema’ (BBT), chini ya Wizara ya Kilimo," amesema Homera.