Harusi ya nyota wa filamu India yatia fora

Muktasari:

Priyanka Chopra, ambaye aling'ara katika filamu ya "Barfi",  ameolewa na mwanamuziki wa Marekani Nick Jonas na harusi yao ya kifahari ilifanyika kwa siku mbili; Jumamosi na Jumapili.


New Delhi. Nyota wa filamu wa Bollywood, Priyanka Chopra na mwanamuziki wa Marekani, Nick Jonas Jumapili usiku nwalifanya tamasha kubwa la muziki kwa ajili ya wagenmi waliohudhuria harusi yao iliyofanyika Jumamosi.

Chopra mwenye umri wa miaka 36 na Jonas, 26, walitumbuiza nyimbo zenye mahadhi ya Kihindi wakati marafiki zao wakipiga makofi katika tamasha hilo lililofanyika kwenye jumba la kifahari la Umaid Bhawan katika jiji la Jodhpur, magharibi mwa India.

Juzi wawili hao walianza kuachia picha zao za harusi zinazoonyesha walikuwa na wamepambwa na wanaume 12 na wanawake 12, wasichana wanne na mshika pete, wote wakiwa wamevalia nguo zilizobuniwa na Ralph Lauren.

Chopra alivalia gauni la mikono mirefu linaloonyesha ngozi mithili ya nyavu, lakini likiwa na maua mikononi, shingo ndefu na shela yenye urefu wa futi 75.

Tamasha hilo lilimaanisha harusi yao imefanyika kwa siku mbili na kupachikwa sifa ya "Harusi ya Mwaka".

Chopra alianza kung'ara katika tasniua ya filamu wakati alipoigiza kama Alex Parish katika tamthiliya ya "Quantico", lakini filamu zilizompa umaarufu zaidi ni “Barfi” ambayo ameigiza kama mtoto mwenye ugonjwa wa akili, na “Bajirao Mastani” ambayo ameigiza kama malkia katika jamii ya zamani ya India. Pia ametayarisha filamu kama ya “Koffee with Karan,” na amesema kuwa kwa sasa anashirika kuandaa filamu Hollywood.

Mbali na uigizaji, Chopra anajulikana kwa kuimba na kudansi.

Usiku wa Jumapili ulitawaliwa na burudani za tamaduni za Kihindi kwa ajili ya wanaharusi hao ambao walipeana ahadi za ndoa Jumamosi katika shughuli iliyokuwa ya Kikristo.

Chopra alisema shoo hiyo ya "sangeet" ambayo ilijumuisha wasanii wengi, ilianza kwa nyimbo kali na mashindano ya kudansi baina ya familia hizo mbili za muziki.

"Ilikuwa ni burudani safi. Kila familia ilitoa stori yetu kwa kutumia muziki na dansi, ikiwa imeambatana na kicheko na upendo," alisema Chopra katika akaunti yake ya Instagram.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe hiyo ni kaka yake Jonas anayeitwa Joe Jonas na mchumba wake ambaye ni mcheza sinema wa Uingereza na nyota wa filamu ya "Game of Thrones", Sophie  Turner.

Mbunifu wa mavazi wa Marekani, Ralph Lauren alisema kampuni yake pia ilihusika katika kubuni shughuli hiyo.

"Ralph Lauren ilipewa heshima kubwa kubuni nguo za wanaharusi pamoja na wengine walioshiriki katika harusi," alisema mmbunifu huyo.