Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatari: ARV zatumika kunenepesha kuku, nguruwe

Muktasari:

Wanasayansi, watafiti wakutana kujadili, matumizi holela ya ARV yanavyochangia usugu wa dawa.

Mbeya. Matumizi ya dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARV) kunenepesha mifugo, yametajwa kushika kasi nchini na kuchangia usugu wa dawa hizo unaotokana na ulaji wa mazao ya mifugo kama vile kuku na nguruwe.

Kutokana na hilo, Serikali imelazimika kufanya vikao na wadau wa sekta ya afya na mifugo kuweka mikakati ya pamoja kutafuta suluhisho la udhibiti wa matumizi holela ya dawa na kutoa elimu kwa jamii.

Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Mololo Noah amesema hayo jana kwenye kongamano lililokutanisha wadau wa afya, mifugo, watafiti, na wanasayansi kutoka vyuo mbalimbali kujadili changamoto za sekta ya afya lililoandaliwa na Shirika la HJFMRI.

"Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi holela ya ARV kunenepesha kuku na nguruwe hali inayochangia mlaji kupata madhara ya usugu wa dawa kutokana na wingi wa mabaki ya vimelea kwenye kitoweo," amesema.

Hata hivyo, amesema bado hawana takwimu kwa sababu wanandelea kufanya utafiti na sasa wako kwenye kampeni ya mkoa kwa mkoa ambayo wakiimaliza watakuwa na uhalisia wa picha kamili na kutoa taarifa.

Dk Noah amesema kutokana na changamoto hiyo, sekta ya afya inaendelea na udhibiti na kutoa elimu kwa wananchi kuachana na matumizi yasiyo sahihi.

Hayo yanafanyika wakati ambao utafiti ulionukuliwa na Mwananchi Septemba 13, 2024 uliotolewa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) ukionyesha asilimia 5.8 ya waviu na wanaotumia dawa, wanakabiliwa na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.

Mtafiti Mwandamizi Kitengo cha Maikrobiolojia na Kinga Muhas, Dk Doreen Kamori amesema walifanya utafiti huo mwaka 2020 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara.

Dk Kamori amesema sababu zinazochangia tatizo hilo ni pamoja na kuingizwa nchini dawa ambazo zinachangia usugu na watu kutokuwa wafuasi wazuri wa kutumia dawa.

Mbali ya ARV kutumika kunenepesha mifugo na kuleta usugu wa dawa, amesema dawa nyingine zinazotumiwa ni antibiotiki.

"Ndiyo maana tunahamasisha watoa huduma za afya kuzingatia sheria za utoaji wa dawa kwa kufuata maelezo ya wataalamu wa afya na maelezo ya daktari pindi wanapohudumia wagonjwa," amesema.

Visababishi vya usugu

Dk Noah amesema usugu wa dawa unatokana na ulaji wa mazao ya mifugo iliyonenepeshwa kwa kutumia ARV na kusababisha mwili kuwa na kiwango kikubwa cha dawa.

"Sisi binadamu tunapokula nyama na mayai ambayo mzalishaji alitumia dawa kunenepesha mifugo anapata usugu wa dawa," amesema.

Dk Noah amesema ili kufikia malengo ya kupambana na hali hiyo Serikali imekuja na kampeni kabambe ya ‘Holehole itakucost’ yenye lengo la kutoa elimu ili kuelimisha jamii.


Wadau wanena

Mkurugenzi Mradi wa Shirika la HJFMRI Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Dk Emmanuel Bahemana amesema matumizi holela ya ARV yamesababisha wastani wa asilimia 3.9 mpaka 19.3 ya watu wanaoishi na VVU kubainika kuwa na usugu wa dawa mpya ya kufubaza virusi aina ya Dolutegravir (DTG).

"Matumizi holela na ulaji wa mazao ya nyama zilizokuzwa na ARV umesababisha usugu wa dawa licha ya jitihada mbalimbali za kubadili dawa za Waviu (watu wanaoishi na virusi vya ukimwi) lakini kutokana na hali hiyo kuna shaka ya kuwepo kwa takwimu kubwa ya wagonjwa kubainika na usugu kwa siku za mbeleni," amesema.

Dk Bahemana amesema kutokana na hali hiyo endapo hatua stahiki za kudhibiti matumizi holela ya dawa hazitachukuliwa kuna uwezekano mkubwa kukawa na ongezeko kubwa la maambukizi ya VVU na kupunguza nguvu kazi.

"Dawa mpya ya DTG miaka miwili iliyopita iliweza kufanya vizuri katika mapambano ya VVU lakini kutokana na matumizi holela wastani wa asilimia 3.9 mpaka 19.3 ya watu wanaotumia dawa za kufubaza maambukizi ya Ukimwi wamebainika kuwa na usugu wa dawa," amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema wamelazimika kufanya kongamano la pamoja likihusisha sekta za mifugo, afya, watafiti, na wanasayansi ili kusaka mwarobaini wa kudhibiti matumizi holela ya ARV kunenepesha mazao ya wanyama.


Wizara ya Afya

Dk Chacha Mangu kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga, Kitengo cha Udhibiti wa Magonjwa amesema kumeibuka changamoto kubwa ya matumizi holela ya dawa za binadamu kwa wanyama na kusababisha athari ya usugu wa vimelea vya magonjwa yasiyosikia tiba.

Amesema tafiti mbalimbali zimefanywa nchini na kuonyesha ongezeko kubwa la matumizi ya ARV na kusababisha usugu wa vimelea vya magonjwa kushindwa kukabiliana na dawa.

"Kongamano hili ni moja ya mikutano ya kujadili masuala ya afya, magonjwa yanayohusisha binadamu, wanyama na mazingira lenye lengo la kujadili changamoto za matumizi holela ya dawa, hususani ARV na kutoka na mikakati ya pamoja," amesema.

Mkazi wa Nonde jijini Mbeya, Rehema Mwanjonde ameomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuweka kampeni maalumu ya mapambano dhidi ya matumizi holela ya dawa ili kuokoa kizazi cha sasa hususan waathirika wa maambukizi mapya ya VVU.

"Tunaona wadau wakiwemo Shirika la HJFMRI kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (Pepfar) namna wanavyopambana na vita dhidi ya VVU kuokoa maisha ya Watanzania. Inapofika watu wachache kwa masilahi yao binafsi wanafanya uharibifu, sheria ichukue mkondo wake," amesema.


ARV kunenepesha mifugo

Ofisa Mfawidhi Bodi ya Nyama Tanzania (TMB)   Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dk Mpoki Alinanuswe amesema suala la ARV kunenepesha mifugo ni kama inavyofanya kazi katika mwili wa binadamu kuimaisha kinga na kuleta hamu ya kula.

"Siyo kwamba zina kemikali zinazoweza kumnenepesha mnyama kwa sababu asili ya ARV ni kuongeza kinga za mwili na kumsaidia mwathirika wa VVU kuongeza hamu ya kula na kuimarisha afya, ndiyo sababu watu wakitumia kitoweo hupata athari ya usugu wa dawa mwilini," amesema.

Dk Alinasuswe ambaye ni ofisa mifugo ameshauri jamii kuacha matumizi ya ARV kulisha mifugo ili kuepuka madhara kwa binadamu kukosa tiba sahihi pindi anapohitaji huduma za matibabu.

"Siwezi kuzungumza moja kwa moja kama ARV ina vimelea vya kunenepesha mazao ya nyama lakini matumizi yake kwa binadamu hulinda afya na ndiyo mfumo huo kwa wanyama," amesema.


ARV, kuongeza uzito

ARV hutengenezwa kudhibiti au kupunguza uzalishaji wa virusi vya Ukimwi (VVU) kwenye mwili.

Mtu anayetumia ARV anaweza kuongezeka uzito kwa sababu kwa kuwa humsaidia kudhibiti virusi vya Ukimwi, hivyo baada ya mwili kuwa na kinga bora, afya kwa ujumla inaweza kuimarika.

Hali hii huweza kujumuisha kuongezeka kwa hamu ya kula na hivyo uzito kuongezeka.

ARV zinapoimarisha kinga na kuzuia uharibifu zaidi, mwili unapata nafasi ya kurekebisha uzito uliopotea.

Mbali ya hayo, baadhi ya aina za ARV zinaweza kusababisha mabadiliko ya kimetaboliki, kama vile kuhifadhi mafuta mwilini (lipodystrophy), hali inayoweza kuongeza uzito au kubadilisha jinsi mafuta yanavyosambazwa mwilini.