Hatima kesi ya kina Sabaya leo

Muktasari:

Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anatarajiwa kutoa uamuzi iwapo washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la.

Arusha. Hatima ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita iwapo wana kesi ya kujibu au la inatarajiwa kujulikana leo.

Januari 10, Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili sabaya na wenzake alisema leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha itatoa uamuzi huo baada ya jamhuri kufunga kesi kwa upande wao.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule aliieleza shauri lilipangwa kwa ajili ya kusikiliza ila upande wa jamhuri wanaomba kufunga kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili wa utetezi, Mosses Mahuna alieleza kuwa hawana pingamizi na ombi lililowasilishwa na kuwa licha ya wao kuwa na fursa ya kufanya mawasilisho kushawishi mahakama endapo watuhumiwa wana kesi ya kujibu au la, hawatatumia fursa hiyo.

“Kiutaratibu mahakama inapaswa ku determine watuhumiwa kama wana kesi ya kujibu au la, na kwa upande wetu tuna haki ya kuleta submissions ili kuieleza na kushawishi mahakama endapo wana kesi ya kujibu au la.

“Upande wetu hatutatumia hali hiyo, tunaomba kuiachia mahakama ili yenyewe ipitie vielelezo na mwenendo na kusema kama wana kesi ya kujibu au la,” alisema. Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 13 na vielelezo 12.

Washtakiwa hao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Juni 4, mwaka jana na kuanzia Septemba 23, mwaka jana kesi lilianza kusikilizwa.

Mbali na Sabaya, washtakiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya ambao wanakabiliwa na makosa matano.

Shtaka la kwanza wanadaiwa Januari 22, 2021 waliongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linalowakabili washtakiwa wote saba kwamba walipokea Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya pekee anadaiwa kujihusisha na rushwa na kwamba alichukua Sh 90 milioni, matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.