Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya ndiyo mahitaji ya  wanawake katika Dira 2050

Lilian Liundi, Mkurugenzi TGNP

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa wanawake hao, pamoja na mambo mengine dira hiyo inapaswa kuwa na mrengo wa kijinsia, ikibeba masuala ya usawa wa jinsia kama nguzo ya utekelezwaji wake.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kukusanya maoni ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, wanawake wamebainisha wanachokihitaji katika dira hiyo kama msingi wa kufikiwa kwa matarajio yao.
Kwa mujibu wa wanawake hao, pamoja na mambo mengine dira hiyo inapaswa kuwa na mrengo wa kijinsia, ikibeba masuala ya usawa wa jinsia kama nguzo ya utekelezwaji wake.

Ili kufikia hatua hiyo, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, unaohusisha asasi takribani 200 za kiraia unapendekeza mchakato wa utayarishwaji wa dira husika, utokane na ushiriki wa wanawake na wanaume, bila kujali tofauti za rika, itikadi, dini, kabila, maumbile wala tabaka.

Gema Akilimali, Mwenyekiti wa TGNP

Mtandao huo unaoratibiwa na Mfuko wa Ruzuku Tanzania (Women Fund Tanzania-Trust) na Mtandao wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) unaoratibiwa na WILDAF, pamoja na mambo mengine unalenga kuwezesha umiliki wa pamoja wa ajenda ya maendeleo ya taifa.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni miongoni mwa taasisi zilizopo katika mtandao huo.

Akizungumzia matamanio ya wadau hao katika dira ya mwaka 2050, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi anasema kufikia mwaka huo hakupaswi kuwepo kaya itakayokosa chakula bora na cha kutosha.

Sambamba na kukosa chakula, anasema hakupawi kuwa na mtu atakeypatwa na madhara yoyote kutokana na kukosa huduma hiyo.

Ukiachana na chakula, kwa mujibu wa Liundi, elimu itakayotolewa mwaka 2050 inapaswa imkomboe mwanamke kudai na kutetea haki zake, kumwezesha kutumia vipaji vyake na kujisimamia kama raia huru na kuakisi uasilia na ubora wa maisha ya sasa.

Pia, anasema inapaswa kuhakikisha shule zote zinatoa taulo za kike bure, kujenga misingi ya uwajibikaji dhidi ya ubadhilifu wa rasilimali za taifa na kuhakikisha maeneo ya shule na mengine yanayotoa elimu tangu awali, msingi, sekondari na vyuo ni salama kwa watoto wote wa kike na kiume.

Kwa upande wa sekta ya afya, kufikia mwaka 2050 anasema kusiwe na mwanamke hata mmoja atakayepoteza maisha yake anapofanya kazi ya kuzalisha na kuendeleza rasilimali watu.

“Kusiwe na mtoto atakaepoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma za afya, lishe bora, na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji,” anasema.
Pia, anapendekeza huduma za afya ya msingi zipatikane kwa kila mtanzania kwa ubora na gharama nafuu na kila mtanzania amudu bima ya afya yenye ubora kuendana na hali ya maisha.

Akizungumzia upande wa afya ya uzazi, Gemma Akilimali, Mwenyekiti wa TGNP anasema ni muhimu kuzingatia itifaki ya Maputo kuhusu upatikaji na utolewaji wa huduma   bora ya afya ya uzazi kwa rika zote bila ubaguzi.

“Kuhakikisha   hakuna mtoto wa kike anaolewa chini ya miaka kumi na nane (18) na kuhakikisha mimba za utotoni zinakua  historia kwa mtoto wa kike,” anasema Akilimali.
Anasema katika mwaka huo, kila kaya ifikiwe na huduma za maji safi na salama na uboreshaji wa miundombinu na ulinzi wa vyanzo vya maji uzingatiwe.

Amesema pendekezo lingine ni kuwepo kwa usawa wa kijinsia kama suala mtambuka ambalo linapaswa liongoze sekta zote ikiwemo ya uchumi, uongozi, siasa, umiliki wa rasilimali na ufanyaji wa uamuzi.

“Tunadai suala hili liingizwe katika maeneo yote ya dira ikiwemo utangulizi, malengo, utekelezaji, na ufuatiliaji,” anasema mwenyekiti huyo wa TGNP.

Anasema ni vema kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili ikiwemo rushwa ya ngono na udhalilishaji wa kisaikolojia, kiuchumi na kimwili unaokwamisha uwakilishi na ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, vinabaki kuwa historia.

“Kuhakikisha nafasi zote za uongozi na maamuzi una uwakilishi  sawia (50/50),” anasisitiza.


Umasikini

Katika umasikini, Liundi anasema kufikia mwaka 2050 wanatamani kuiona Tanzania inakuwa nchi yenye rasilimali nyingi na zikitumika kwa umakini na uwajibikaji kwa kuzingatia mrengo wa jinsia.

Anasema ni kiu ya mtandao huo kuona umasikini wa hali na mali na ufukara vinakua historia.

“Katika mazingira hayo, wanawake tunadai utajiri wa nchi utatumika kwa njia linganifu unaonufaisha wanawake, wanaume, wasichana, na wavulana,” anasema.
Anasema uwezekaji kwenye vipaumbele vya taifa viende sanjari na kuondoa pengo la ajira na ujira na umasikini uliovikwa sura ya mwanamke na kijiji.


Amani na utulivu

Kwa upande wa amani na utulivu, Mkurugenzi wa WiLDAF Anna Kulaya anasema kufikia mwaka 20250, wanatamani kuona aina zote za ukatili zinakemewa kiuwajibikaji, kiutawala katika  ngazi zote kama ilivyobainishwa katika Katiba.

“Vyombo vyote vya dola vyenye wajibu wa ulinzi wa raia viwajibike kwa raia wote katika ngazi zote kuanzia kaya, jamii, mashuleni na meneo ya kazi dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji,” anasema Kulaya.

Anasema ukatili wa aina yoyote dhidi ya wanawake, wasichana na watoto wa kiume uwe umetokomezwa.

Katika utawala na uongozi bora, anasema ni matarajio ya wanawake kufikia mwaka 2050 kunakuwa na ushiriki sawa wa wanawake kwenye ngazi zote za uongozi wa uamuzi.

“Uwajibikaji wenye mrengo wa kijinsia kwenye usimamzi wa rasilimali za Taifa uzingatiwe, sheria, sera, na taratibu zote kandamizi zinazohalalisha ubaguzi wa kijinsia zimebatilishwa na uwepo wa katiba inayobatilisha sheria na taratibu kandamizi yenye kubainisha haki za wanawake, wasichana,  watoto wa kiume, na watu wenye ulemavu,” anasema Kulaya.

Kadhalika, anasema kufikia mwaka huo, wanataka utekelezaji wa dira uhakikishe unaongozwa na mfumo utakaotumia takwimu za kijinsia ili kuongoza mwelekeo wa nchi kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Kulaya amejenga hoja hizo za kiuchambuzi, huku akionyesha mapengo ya kijinsia katika dira ya mwaka 2025, ikiwemo kutobainishwa kwa usawa wa jinsia kama sehemu ya sifa kuu za dira husika.
Hata hivyo, katika hoja hiyo Mkurugenzi wa TGNP Liundi anasema pengo lingine la jinsia katika dira hiyo, lilibainika katika sifa ya amani, utulivu na umoja akifafanua kulipaswa kuhusishwe masuala ya ukatili wa watoto na wanawake ndani ya familia.
Kwa mujibu wa Liundi, pengo lingine lipo katika sifa ya utawala na uongozi bora, akisema kuna ukimya kuhusu uwajibikaji wenye kuzingatia haki za wanawake, watoto na watu maskini.

“Hususani kama zilivyobainishwa katika katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia.

“Kwenye suala la rushwa, eneo hili halikupambanua rushwa kwa mapana yake, ikiwemo rushwa ya ngono, na hivyo kuathiri utelekezaji na ufuatiliaji,” anasema Liundi.
Anasema Dira hiyo ya 2025 ilina pengo katika sifa ya jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza zaidi, ambao kwa tafsiri yake walioelimika ni watu wanaopinga ukandamizaji wa aina zote.

“Suala la ujenzi wa elimu jumuishi itakayowezesha wanawake kwa wanaume, kushiriki katika muktadha wa soko huria ambalo mara nyingi lina silika ya kuwaacha wengi nje ya maendeleo hususani wanawake, wasichana, na watu wenye ulemavu halikuzingatiwa,” anasema.


Eneo la uchumi

Akizungumzia eneo la uchumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Women Fund Tanzania (WFT), Rose Marandu anasema kunahitajika ujumuishaji wa wanawake na wanaume ili kuepuka jamii isitumbukie kwenye ufukara uliopitiliza.

Hata hivyo, katika uchambuzi wake wa jumla, Marandu anabainisha kuwepo kwa mafanikio katika kupunguza umaskini, ujinga na maradhi, elimu, afya na kupatikanaji wa huduma za msingi.

Lakini, anasema utekelezwaji wa dira hiyo, umekuwa na changamoto kadhaa ambazo ni hulka ya kutegemea misaada, uchumi dhaifu na uwezo mdogo wa kusimamia uzalishaji mali, kadhalika changamoto za utekelezaji.

Kutokana na mapengo ya jinsia, anasema pamoja na kuwa na chakula cha kutosha, bado kuna pengo katika upatikanaji wake na unufaikaji wa chakula hicho. 

“Asilimia 28 ya watoto na vijana walikuwa na udumavu. Takribani asilimia 20 ya familia hazina uwezo wa kumudu mlo wenye kalori za kutosha, huku asilimia 59 za kaya haziwezi kumudu lishe bora,” anasema Marandu.

Anakwenda mbali zaidi na kueleza asilimia 34 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 wamedumaa.

Kuhusu elimu, anasema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna idadi kubwa ya watoto wanaostahili kuwepo shuleni lakini hawapo, ama kwa kusitisha au kutojiandikisha.

“Mfumo wa elimu kuendana sanjari na mabadiliko ya uchumi ni changamoto nyingine hususan kwa wasichana pale ambapo ajira mpya kwenye sekta zinazokua zinahitaji utaalam ambao haupatikani kwenye elimu,” anasema Marandu.
Kadhalika, anasema katika cha utekelezaji wa dira, pengo la jinsia limeonekana katika ajira, uongozi, umiliki mali.

“Sekta pekee ambayo wanawake ni wengi kuliko wanaume, ni kilimo ambapo wanawake ni asilimia zaidi ya 54 ukilinganisha na wanaume asilimia 48,” anasema.
Katika umiliki mali, anasema ni asilimia saba tu ya wanawake wanamiliki wa nyumba wenyewe na asilimia 28 wana umiliki wa nyumba na wenzi wao.

Kuhusu maji safi na salama anasema takriban asilimia tano ya wakazi wa mijini na asilimia 41 ya wakazi wa vijijini wanatumia maji yasiyo salama.

“Ni asilimia 61 tu ya kaya zote Tanzania zina huduma ya maji ndani ya kaya zao. Na kaya asilimia 32 wanapata huduma za maji taka,” anasema.

Kuhusu huduma za afya, anasema masuala ya haki za uchumi, ukatili wa jinsia, na mzigo wa kazi unaosababisha mwanamke wa Tanzania kupoteza maisha wakati anapoendeleza kizazi hayakuguswa.

“Hii inasababisha vifo vya uzazi kuendelea kuwa vingi, kwa mfano katika kipindi kutoka mwaka 2016-2020 vifo vya uzazi vilipungua kutoka 556 kufikia 292 kwa  kila wanawake 100,000 wanaojifungua,” anaeleza.

Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, anasema asilimia 24 tu ya Watanzania wanafikiwa na umeme kwenye kaya zao na kwa walioko vijijini ni asilimia saba.

“Asilimia 88 ya Watanzania wanatumia takriban tani million 20.7 za biomass, mfano kuni na kinyesi cha ng’ombe kama chanzo cha nishati. Wanawake na watoto wa kike wanatembea takriban kilometa 4.8 au saa 4-5 kutafuta nishati, hali ambayo inawaweka kwenye hatari ya kukumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa, rushwa ya ngono, na vipigo,” anasema.