Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HESLB yaja kivingine urejeshaji wa mikopo

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji  Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed (kulia) wakisaini makubaliano ya ushirikiano kwa ajili ya kutoa fursa za ajira kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Muktasari:

 Wanufaika wasiorejesha mikopo kutafutiwa fursa za ajira kuwawezesha kulipa kidogokidogo.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imeingia makubaliano na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA),  ili kutafuta fursa za ajira kwa wanufaika kuwawezesha kurejesha mikopo.

HESLB imesema hadi sasa inadai Sh700 bilioni kutoka kwa wanufaika 222,532 ambao ni kati ya 754,000 waliopatiwa mikopo ya elimu ya juu.

Fursa hizo za ajira zitakuwa kwenye sekta mbalimbali zikiwamo za utalii, madini, uzalishaji na kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia amebainisha hayo leo Machi 18, 2024 wakati wa utiaji saini makubaliano ya ushirikiano na ZEEA.

Amesema kwa kuanza fursa zitakuwa kwenye sekta ya utalii.

"Tumeangazia maeneo makuu matatu katika ushirikiano huu, kwanza ni kutafuta fursa za ajira kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ili waweze kuirejesha na wengine wanufaike,” amesema na kuongeza:

"Pia, tutashirikiana na ZEEA kuandaa mafunzo ya kuongeza ujuzi na fursa za ajira katika sekta mbalimbali tukianza na ya utalii, ambazo zitasaidia kuongeza kasi ya kurejesha mikopo kutoka kwa wajasiriamali walionufaika na mikopo ya elimu ya juu."

Dk Kiwia amesema: "Tunaendelea kuongeza jitihada na kubuni mikakati ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa ushirikiano na wadau kwa kutengeneza fursa za ajira, kuwajengea  mazingira ya kuwawezesha kupata ajira ili wanufaika hao sasa waanze kurejesha mikopo kidogokidogo," amesema.

Dk Kiwia amesema kutakuwa na kituo cha kuwajengea uwezo ili waweze kujiajiri, kuajiriwa, na wale watakaopenda kupitia vyuo vikuu mbalimbali watajiandikisha na kupewa fursa hizo.

"Ni wao kujitokeza kwa wingi, Bodi ya Mikopo tuna kanzidata ambayo tutaitumia, tunatoa fursa hii kwa wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu," amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed, amesema watafanya kazi na vyuo vikuu,  wakilenga kuhakikisha kila anayehitimu anapata kazi kwa kujiajiri au kuajiriwa.

"Wanachopaswa ni kujisajili tu na kuja kwetu, tunaamini hawa wanafunzi ni wajasiriamali watarajiwa lazima tuwatayarishe huko na kuingia kwenye soko la ajira," amesema.

“Kwa makubaliano haya tunatarajia wanufaika ambao wako katika sekta isiyo rasmi watajitokeza na kuanza kurejesha mikopo. Pia tunatarajia ongezeko la wanafunzi wanaohitaji kunufaika na fedha zinazorejeshwa, hivyo kuufanya mfuko wa kugharimia wanafunzi kuwa stahimilivu," amesema Dk Kiwia.

Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo Samora Edmund, aliyesoma Chuo cha Ufundi Arusha, amesema mkakati huo utakuwa na manufaa kwa wahitimu wasio na ajira.

"Wengi wanahitimu na ajira hakuna, hivyo kama Bodi itawasaidia itapata marejesho, pia kwa atakayepata fursa atakuwa amejikomboa kwenye ajira,” amesema.

Edmund amesema kikubwa ni Bodi kuweka utaratibu mzuri wa makato ili yasiwaumize.

Mnufaika mwingine, Mary Edward wa Chuo Kikuu cha Tumaini amesema ni mkakati mzuri japo umechelewa kuanza.

"Utasaidia watu wengi kurejesha  mikopo, kama tunavyojua ajira sasa ni ngumu, hivyo Bodi inapowatengenezea fursa hizi, kwanza itakuwa na uhakika wa pesa zake kurejeshwa," amesema.

Amesema ni utaratibu mzuri kama utakuwa na mazingira rafiki kwa wanufaika wa mikopo hiyo.