Hisia tofauti kushuka kwa takwimu za mimba shuleni

Muktasari:

  • Wakati Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya Kusini ikishtushwa na matumizi makubwa ya dawa za kuzuia mimba kwa wanafunzi, wadau wa elimu nchini wameomba utafiti wa kina kujua sababu za kushuka kwa utoro unaosababishwa na wanafunzi kupata mimba.

Wakati Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya Kusini ikishtushwa na matumizi makubwa ya dawa za kuzuia mimba kwa wanafunzi, wadau wa elimu nchini wameomba utafiti wa kina kujua sababu za kushuka kwa utoro unaosababishwa na wanafunzi kupata mimba.

Hofu ya wadau inatokana na hisia kuwa huenda idadi kubwa ya wanafunzi wanatumia dawa hizo, hali ambayo pia inaweza kuwaathiri kiafya.

Hata hivyo, Serikali imesema mikakati ikiwamo ujenzi wa mabweni, imechangia kupunguza mimba kwa wanafunzi

Hivi karibuni TMDA kanda ya Kusini imebaini kuwapo kwa matumizi makubwa ya dawa aina ya Depo-Provera (sindano), hali ambayo inaweza kusababisha ugumba na utasa.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake hivi karibuni, meneja wa TMDA kanda hiyo, Engelbert Bilashoboka alisema katika uchunguzi wao, wamebaini kuwa baadhi ya wazazi wanashiriki kuwatafutia watoto dawa hizo.

Katika uchunguzi huo, walifanikiwa kupata taarifa za uuzwaji wa dawa hizo mitaani, huku zikiwa zimebebwa kwenye mabegi na kuwakamata watu watatu waliohusika na uuzwaji holela wa dawa hizo mitaani na kuwakuta nazo zenye thamani ya Sh200, 000 na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

“Kanda hii kuna matumizi makubwa ya dawa za kuzuia mimba; cha kushangaza zinauzwa hadi mitaani hii ni hatari kubwa kwa mabinti wadogo hasa wanaochezwa wakiwa na umri ndogo, zinaweza kusababisha ugumba na utasa kwao.


Utafiti

Hoja ya wadau wa elimu kutaka utafiti zaidi imekuja kufuatia ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayoonyesha kuwa wanafunzi wa shule ya msingi walioacha shule kutokana na mimba wamepungua kwa asilimia 12.8 huku wa sekondari wakipungua kwa asilimia 16 kati ya mwaka 2019 na mwaka 2020.

Ripoti hiyo iitwayo BEST 2021 inaonyesha kuwa ni wanafunzi 989 pekee wa shule za msingi ndiyo waliokatisha masomo yao baada ya kupata ujauzito mwaka 2020 ikilinganishwa na wanafunzi 1,135 waliokuwapo mwaka 2019.

Kwa upande wa sekondari, mwaka 2019 wanafunzi 5,398 waliacha shule kwa sababu ya ujauzito idadi ambayo ilipungua hadi 4,543 mwaka 2020 ikiwa ni pungufu ya wasichana 855.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, wanasema nguvu zaidi zinapaswa kuwekwa katika darasa la sita na saba kwa shule za msingi, huku upande wa sekondari iwe kwa wanafunzi wa kidato cha pili hadi nne.

Hiyo ni kwa sababu madarasa hayo yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya wasichana wanaobeba mimba.

Madarasa hayo mawili kwa shule za msingi yalitoa wasichana 782 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya wasichana wote walioacha shule mwaka 2020.

Kwa upande wa sekondari madarasa tajwa awali yalitoa asilimia 84.17 ya wasichana walioacha shule kutokana na mimba.


Mikoa

Wakati kwa upande wa shule za sekondari mimba zikionekana walau upungufu wake ni mkubwa kuliko shule za msingi, lakini mkoa wa Morogoro bado ulikuwa na idadi ya wanafunzi wengi waliopata mimba kuliko mikoa mingine.

Ndani ya mkoa huo, wasichana 344 wa shule za sekondari waliacha shule baada ya kupewa mimba huku Arusha ikifuata kwa wasichana 337 kukatishwa masomo yao huku mikoa ya Mwanza na Dodoma ikifuatia kwa wasichana 340 na 305, mtawalia.

Wakati mikoa hiyo ikiwa na idadi kubwa mikoa ya Katavi na Njombe ilikuwa na idadi ndogo ya wanafunzi walioacha shule kwa ajili ya mimba ambapo idadi yao ilikuwa 15 na 77, mtawalia.

Akizungumzia suala hilo, Rebecca Gyumi ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative alisema mimba kwa upande wa sekondari, zimepungua kiasi huku akidhani kuwa huenda kuna mwamko kwa jamii baada ya kuona namna gani mimba za utotoni zinavyoleta mdondoko wa wanafunzi shuleni.

“Sidhani kama tumefanya utafiti wa kujua hili limesababishwa na nini, hivyo huenda pia hatua zinazochukuliwa kwa wale wanaowapa ujauzito wanafunzi kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake,” alisema Gyumi.

Alisema hatua hizo huenda pia zimefanya wale waliokuwa wanaona wanafunzi kama kundi ambalo wanaweza kuwarubuni kurudi nyuma na kuacha tabia hizo.

Anasema mwamko wa elimu kwa wazazi na kutaka kupeleka watoto wao shule, huenda imekuwa moja ya sababu ya kupungua kwa mimba hizo.

“Pia wasichana kutambua fursa walizonazo na ndoto wanazoweza kufikia, kuna hamasa kuhusiana na elimu na nafasi yake baada ya kumaliza elimu yake,” alieleza.

Alisema takwimu za wanafunzi wanaocha shule kwa upande wa shule ya msingi si kubwa sana kama sekondari.

“Lakini upungufu huu hatuwezi kuudharau, tuangalie nini kimetokea na baadaye itakuwaje,” alisema Gyumi.

Mtafiti wa masuala ya elimu, Muhanyi Nkoronko alisema kuongezeka elimu inayotolewa jamii kumekuwa kukipunguza changamoto zilizokuwa zikimzuia msichana kwenda shule.

“Hamasa ya kuhakikisha msichana anapata elimu imekuwa kubwa, Serikali imejenga mabweni inapunguza vishawishi. Baadhi ya mada zinazofundishwa shuleni ikiwemo ujinsia na uzazi, zimewafanya watoto kupata uelewa juu ya namna wanavyoweza kujilinda dhidi ya mimba,”alisema Nkoronko.

Alisema wadau pia wamekuwa wakipiga kelele na kuweka fedha katika kufanya tafiti zao kuelimisha wanafunzi juu ya afya ya uzazi jambo ambali limeleta mabadiliko chanya.

Kwa upande wake, Catherine Sekwao ambae ni mdau wa elimu alisema ni vyema utafiti wa kina ufanyike ili kujua ni njia zipi zilizotumika kupunguza kiasi cha mimba kwa wanafunzi.