Hofu mchele mbovu kutoka nje yatanda

Moshi. Shehena ya mchele unaoelezwa kuwa mbovu na haufai kwa matumizi ya binadamu, unaingizwa kila siku mkoani Kilimanjaro kupitia njia za panya zilizopo Wilaya za Rombo na Moshi na kuchanganywa na mchele mzuri na kuuzwa.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza mchele huo unaingizwa kutoka Kenya na wafanyabiashara wasio waaminifu wakipitia maeneo ya Tarakea na Munga wilayani Rombo na Kitobo, Madarasani na Mariatabu Wilaya ya Moshi.

Inaelezwa kwa siku malori kati ya matano na 10 aina ya Fuso huingia nchini kupitia njia hizo za panya na kuingia katika barabara rasmi za Tarakea-Himo na baadaye barabara ya Moshi-Himo na huhifadhiwa kweye maghala.

Baadaye mchele huo huchanganywa na mchele mzuri wa Tanzania na kisha kuuzwa maeneo mbalimbali ya mkoa huo na nje ya mkoa, huku mwingine ukifungwa katika vifungashio kama mchele uliozalishwa na wakulima wa Tanzania.

“Wewe jiulize sisi ndio tunawalisha hao jamaa kwa nafaka, halafu leo eti mchele unatoka kwao unakuja nchini kwetu na ukishachanganywa na mchele mzuri wa hapa Tanzania unauzwa kati ya Sh3,500 hadi Sh3,800,” kilidokeza chanzo chetu.

Mbali na mchele huo kuingizwa kwa malori, pia kuna wimbi kubwa la mchele huo kuingizwa kwa pikipiki kwa kutumia njia za panya na wimbi hilo linatajwa kugeuzwa mradi kwa baadhi ya polisi na mgambo.


Wananchi waeleza

Wakizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu jana, baadhi ya wananchi wa kata ya Makuyuni walisema kwa siku wanashuhudia Fuso nne hadi sita zikiwa zimepakia mchele huo kupitia njia za panya za Madarasani na Kitobo.

Ismail Bakari, mkazi wa Makuyuni, wilaya ya Moshi alisema mchele huo huingizwa kupitia maeneo hayo kuanzia saa 12 jioni hadi saa moja usiku, kila siku na mara chache mchana.

Alidai mchele huo wameelezwa hupelekwa katika magala ya wafanyabishara yaliyopo Himo na Moshi mjini kwa ajili ya kuchanganywa na mchele unaolimwa Moshi na maeneo mengine nchini, kisha kupelekwa sokoni.

Kwa upande wake, Lilian Mushi alisema mchele huo kwa kuutazama huwezi kuutambua, lakini ukipikwa hauna ladha na uko kama makapi.

Mmoja wa mkazi wa Holili wilayani Rombo, alidokeza kuwa mchele huo ulianza kuingia kwa wingi mwaka jana na mkuu wa wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maige na kamati yake ya usalama wamekuwa wakipambana kudhibiti mchele huo.

Mbali na hilo, baadhi ya wananchi walisema mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) waliyemtaja kwa jina la Boniface Mayala anajitahidi kukabiliana na uingizaji wa mchele huo, lakini anazungukwa na baadhi ya askari.


RPC, TRA wanena haya

Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo alipoulizwa kuhusu uingizwaji wa mchele huo na ushiriki wa baadhi ya askari wake, alisema hana taarifa za uingizwaji za michele huo nchini na kwamba atalifanyia kazi.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, James Kasamalo, alisema kwa kipindi cha miezi sita, wamekamata mifuko 2,313 ya mchele sawa na tani 80.6 uliokuwa ukisafirishwa kimagendo kupitia njia za panya.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kwa kipindi hicho cha miezi sita wamakamata magari matatu aina ya Fuso pamoja na pikipiki nne na kwamba zinashikiliwa na mamlaka hiyo wa ajili ya taratibu mbalimbali za kisheria za mamlaka hiyo.

Kasamalo alisema kwa miezi miwili ndio kumekuwepo na wingi wa mchele unaoingia nchini kupitia njia za panya kutoka Kenya.