Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hofu mradi wa maji kukamilika Ruangwa, mkandarasi alia na malipo

Eneo la mradi huo likiendelea na ujenzi

Muktasari:

  • Mradi huo wenye thamani ya Sh119 bilioni unaotarajiwa kukamilika Julai 2025 unatarajia kunufaisha wakazi 123,657 katika vijiji 56 mkoani Lindi, licha ya kuwapo kwa wasiwasi kutokana na mkandarasi kuchelewa kulipwa.

Ruangwa. Hofu katikati ya matumaini ya kupata maji safi imetanda wilayani Ruangwa mkoani Lindi baada ya mkandarasi wa mradi unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa mazingira Vijijini (Ruwasa) kucheleweshewa malipo yake.

Mradi huo wenye thamani ya Sh119 bilioni unaotarajiwa kukamilika Julai 2025 unatarajia kunufaisha wakazi 123,657 katika vijiji 56 mkoani Lindi.

Vijiji 34 vitanufaika kutoka wilaya hiyo huku 21 vikitokea Wilaya ya Nachingwea kimoja Wlaya ya Lindi vijijini kimoja.

Mkazi wa Kijiji cha Chimbila A, Zaituni Juma akizungumza Jumanne Julai 9, 2024 amesema baadhi ya maeneo wilayani Ruangwa hadi sasa wanatumia maji ya chumvi hivyo ujio wa mradi huo utasaidia kuondoa changamoto hiyo.

"Maji tunayotumia sasa hivi ni maji ya chumvi, tunaishukuru Serikali kwa kuleta mradi mkubwa wa maji katika wilaya yetu ilikuondoa changamoto ya kutumia maji ya visima ambayo sio mazuri sana kwa matumizi ya binadamu,”amesema Zaituni.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mradi, Nurani Mohamed amesema mradi huo wa maji ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini japokuwa wanakabiliwa na changamoto ya malipo kwa mkandarasi.

"Changamoto kubwa iliyokuwepo ni mkandarasi kulipwa fedha asilimia chache lakini tunashukuru kwa jitihada anazofanya hadi kufikia asilimia 40 ya utekelezaji  wa mradi,"amesema Mohamed.

Naye Mkandarasi kutoka kampuni ya Emirets Building Company, Saidi Msangi ameiomba Serikali kujitahidi kulipa kwa wakati ili aweze kumaliza mradi huo mapema na wananchi wapate maji safi na salama.

"Changamoto kubwa ni malipo hadi sasa nimelipwa asilimia 15 tu, naiomba Serikali inilipe kwa wakati ili nikamilishe mradi  na wananchi wapate maji safi na salama,"amesema Saidi.

Akizijibu hoja hizo za mkandarasi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ruwasa, Lucy Koya amesema changamoto zote wamezichukua na watakwenda kuzifanyia kazi huku akimshukuru mkandarasi kwa kuendelea na kazi licha ya kucheleweshwa kwa malipo.

"Changamoto zote tumezichukua na tunakwenda kuzifanyia kazi, lengo la Serikali kuhakikisha maji yanafika maeneo yote ya vijijini kwa asilimia 85 na lengo la  Rais Samia ni kumtua mama ndoo kichwani, niwahakikishie wananchi wa Mkoa wa Lindi, mradi huu utamalizika kwa wakati na wananchi watapata maji safi na salama,”amesema Lucy.