Hoja Rais kupunguziwa madaraka bado mwiba

Muktasari:

  • Mjadala wa kutaka Rais apunguziwe madaraka umezidi kushika kasi baada ya vigogo kadhaa, akiwamo Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, kuunga mkono hoja hiyo, huku akitaka jambo hilo lifanywe kwa umakini zaidi.

Dar es Salaam. Mjadala wa kutaka Rais apunguziwe madaraka umezidi kushika kasi baada ya vigogo kadhaa, akiwamo Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, kuunga mkono hoja hiyo, huku akitaka jambo hilo lifanywe kwa umakini zaidi.

Sumaye alisema anaamini si kila jambo linapaswa kufanywa na Rais na hoja hiyo inazidi kupata kasi hivi sasa, kwa kuwa nchi iliwahi kupata kiongozi aliyetumia vibaya madaraka yake ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina.

Hoja ya Rais kupunguziwa madaraka imekuwa ikijitokeza mara kwa mara na siku chache zilizopita Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) liliipendekeza jambo hilo kwa tume ya Rais ya kushughulikia mfumo wa haki jinai inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande.

TEC pia lilitaka kuondolewa kwa kinga ya viongozi ili waweze kushtakiwa.

Mara baada ya kutoka kuwasilisha mapendekezo, Dk Camillus Kassala ambaye ni Mkurugenzi wa hadhi ya utu wa binadamu, idara ya haki, amani na uadilifu ndani ya TEC alizungumza na waandishi wa habari akisema suala la kinga kwa viongozi ni miongoni mwa hoja nne walizoziwasilisha.

“Ndio maana kuna vuguvugu la Katiba mpya ili hiyo kinga iondolewe, watu wanaelewa sasa binadamu wote tuko sawa, uwe rais, bosi, tajiri, kamanda wa polisi wote tuko sawa,” alisema Dk Kassala.

Vuguvugu la kupunguzwa kwa madaraka ya rais lilikuwepo tangu wakati wa mijadala ya mabadiliko ya Katiba mpya mwaka 2011 hadi 2015, wadau mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda walipendekeza hilo lifanyike.

Pinda aliieleza Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba Januari 24, 2013 kuwa kuna haja ya kumpunguzia Rais madaraka, kwani amekuwa na mzigo mkubwa wa kuongoza Serikali.”

“Kitu kikubwa ambacho ningependa kiangaliwe kwenye Katiba mpya kwa upande wa madaraka ya Rais, ni katika uteuzi wa viongozi mbalimbali.

“Nimetaka Katiba Mpya impunguzie mzigo Rais, kwani amekuwa na kazi nyingi. Sasa ni vema angepunguziwa mzigo huo, hasa katika masuala ya uteuzi wa viongozi,” alisema Pinda, aliyekuwa Waziri Mkuu hadi mwaka 2015.


Hoja yaendelea

Hoja hiyo imeibuka tena hivi sasa wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ameshaonyesha dhamira ya kuufufua mchakato wa Katiba mpya, huku wanasiasa waliozungumza na gazeti hili wakitaka madaraka ya rais yapunguzwe, hasa eneo la uteuzi wa viongozi mbalimbali.

Akizungumza na Mwananchi jana, Sumaye, aliyekuwa Waziri Mkuu kutoka 1995 hadi 2005 alisema anaamini si kila jambo linapaswa kufanywa na Rais, lakini haiwezekani kumpunguzia zaidi madaraka mkuu wa nchi.

Hilo linatokana na kile alichokifafanua kuwa, rais ndiye kimbilio la wananchi wanapoonewa, hataeleweka atakapofuatwa na kujibu kuwa jambo hilo lipo nje ya madaraka yake.

“Kuna vitu vingine sio lazima rais afanye, lakini sio sawa kumpunguzia zaidi madaraka rais hadi ukafika wakati anaona mwananchi anaonewa anakosa la kusema, kwa kuwa ni nje ya mamlaka yake,” alisema Sumaye.

Hata hivyo, Sumaye alisema madai ya kupunguzwa kwa madaraka ya rais yanashika kasi pale ambapo kuliwahi kutokea kiongozi aliyetumia vibaya madaraka yake.

“Lakini madai haya yamekuwepo bila sababu za msingi, kwa sababu hakuna anayefafanua hasa Rais apunguziwe madaraka gani,” alisema.

Alichokisema Sumaye kinafanana na kile cha Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliyesema ni halali wananchi kudai utekelezwaji wa hilo, lakini muhimu ni kuangalia madaraka gani yapunguzwe.

Alitolea mfano madaraka ya uteuzi. Alisema yanapaswa kuondolewa kwa rais na badala yake kuwepo na chombo kitakachowafanyia usaili wanaostahili kushika wadhifa husika, kisha kitapendekeza majina kwa mkuu wa nchi kwa ajili ya uteuzi.

“Sio rais anaamka anaamua kumteua fulani, kesho anaamua amtoe analeta mwingine, hapana, tufanye kama wenzetu Kenya,” alisema Jaji Werema.

Nguli huyo wa sheria, alisema madaraka aliyonayo rais yanamfanya kuwa mfalme, akipendekeza mabadiliko ili mkuu wa nchi awe na nafasi inayotosheleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Bisimba, alisema haja ya kumpunguzia rais madaraka ina umuhimu kutokana na yale yaliyoshuhudiwa wakati wa uongozi wa awamu ya tano.

“Watu wameyaishi hayo practically (kivitendo), Rais Samia anafanya vizuri lakini wanaogopa akiondoka yeye akija mwingine hataleta yale yale?” alihoji.

Alieleza wingi wa madaraka ndiyo ulioifanya awamu iliyopita kufanya maamuzi iliyoona yanafaa, lakini hayakuwa mazuri kwa wananchi.

“Hili lilikuwa linasemwa tangu zamani, hasa ule wakati wa mchakato wa Katiba mpya, sema tu halikusikika, lakini sasa hivi limepata nguvu baada ya wananchi kuyaona madhila yake,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Bisimba, madaraka makubwa ya Rais, yanamfanya kuwa dikteta na kuamua kila anachotaka, hivyo yanapaswa kugatuliwa ili abaki na machache ya juu kulingana na nafasi yake.


Alichokisema Msekwa

Katibu Mtendaji wa kwanza na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alishauri hoja hizo zisikilizwe na hatimaye ziamriwe kwa kuzingatia taratibu sahihi.

“Kila mtu ana haki ya kutoa na kusikilizwa maoni yake; kwa msingi huo, wanaotaka Rais apunguziwe madaraka wapewe fursa hiyo na mchakato huo uende hadi kufikia mwisho kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo na zitakazowekwa,” alisema Msekwa

Hata hivyo, mkongwe huyo wa siasa nchini aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, alishauri wenye mapendekezo hayo kuainisha maeneo ya Katiba yanayotoa madaraka makubwa kwa Rais na mapendekezo ya kuyarekebisha.

“Kusiwe na hoja za jumla jumla za Rais kupunguziwa madaraka. Hapana! Kila mwenye hoja hiyo ana wajibu wa kuainisha maeneo ya Katiba yenye marekebisho yanayohitajika,” alisema Msekwa, ambaye amewahi kuwa mjumbe katika tume kadhaa za marekebisho ya Katiba.

Naye Anna Abdallah, mkongwe wa siasa alitaka wanaoleta madai hayo ni vema waeleze wapi kiatu kinabana na wapi kimeachia.

“Wasiishie kusema rais apunguziwe madaraka, waeleze madaraka yepi wanayotaka apunguziwe, tusije kujikuta tunampunguzia baba madaraka kwa mtoto wake, matokeo yake ndiyo kama tunayoshuhudia sasa,” alisema.

Alieleza madai hayo yanaibuka kwa kuwa wanaoyaibua hawaelewi hata madaraka yenyewe.


…mchakato wa Katiba

Mchakato huo ulikwama Aprili 2, 2015 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyokuwa ifanyike Aprili 30 mwaka huo hadi itakapotangazwa tena.

NEC ilitoa sababu ya kutokamilika kwa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR).

Alipoingia madarakani, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, hakuonesha dhamira ya kuuendeleza, licha ya wadau mbalimbali kumtaka kufanya hivyo.

Hata hivyo, baada ya Rais Samia kuingia madarakani baada ya kifo cha Rais Magufuli, ameendeleza majadiliano mbalimbali ya maridhiano, ikiwemo suala hilo la kuufufua mchakato wa Katiba.

Katika kuonesha dhamira yake, juzi jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alisema wataongeza Sh9 bilioni kwenye bajeti ya 2023/24 ili kutimiza maagizo ya Rais Samia.

Alisema ongezeko hilo linakwenda kugharimia utekelezaji maagizo ya Rais Samia, ukiwemo mchakato wa Katiba mpya, marekebisho ya Sheria zinazohusiana na demokrasia.

Alisema katika utekelezaji huo, watakwenda kuomba kuidhinishiwa na Bunge katika bajeti ya 2023/2024.