Homa ya nyani yatangazwa dharura ya kiafya Afrika
Muktasari:
- Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) linachukua hatua juu ya mlipuko wa homa ya nyani (Mpox) ulioenea kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi nchi jirani.
Dar es Salaam. Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) limetangaza dharura ya afya kwa umma kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Mpox.
Hatua hiyo imekuja wakati ugonjwa huo unasambaa barani Afrika, ikieleza lengo ni wito wa wazi wa kuchukua hatua.
Kufuatia hali hiyo pia Shirika la Afya Duniani (WHO) likitarajia kukutana leo Agosti 14, 2024 kwa dharura ili kujadili kuhusu ugonjwa huo.
"Ninatangaza kwa moyo mzito lakini kwa dhamira isiyobadilika kwa raia wetu wote barani Afrika, tunatangaza Mpox kama dharura ya afya ya umma ya usalama wa bara," amesema Jean Kaseya, Mkuu wa CDC Afrika jana Agosti 14 wakati wa mkutano na vyombo vya habari kupitia mtandao.
"Mpox sasa imevuka mipaka na kuathiri maelfu katika bara letu, familia zimesambaratika na uchungu na mateso yamegusa maeneo mengi ya bara letu," amesema.
Kulingana na takwimu za CDC hadi Agosti 4,2024 kumekuwa na wagonjwa 38,465 wa Mpox na vifo 1,456 barani Afrika tangu Januari 2022.
"Tamko hili ni wito wa kuchukua hatua. Ni utambuzi kwamba hatuwezi kumudu tena kuwa watendaji. Ni lazima tuwe makini na wajeuri katika jitihada zetu za kudhibiti na kuondoa tishio hili,” amesema Kaseya.
Mpox huambukizwa kwa kugusana kwa karibu na husababisha vipele, dalili za mafua na vidonda vilivyojaa usaha na unaweza kuua. Ugonjwa huo unaweza kuwa hatari kwa watoto, wanawake wajawazito na walio na mfumo wa kinga mdogo.
Mlipuko huo umekumba nchi kadhaa za Afrika, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu mwaka 1970.
CDC ya Afrika ilionya wiki iliyopita kwamba kiwango cha maambukizi ya virusi kilikuwa kikubwa. Ilisema kuwa zaidi ya wagonjwa 15,000 wa Mpox na vifo 461 viliripotiwa barani Afrika mwaka huu hadi sasa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 160 kutoka kipindi kama hicho mwaka jana.