Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanza upandikizaji uloto

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akizungumza na mtoto Elisha aliyepandikizwa uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Muktasari:

  • Huduma ya matibabu ya upandikizaji uroto kwa wagonjwa wa selimundu inakuwa ya kwanza nchini Tanzania na itasaidia kuokoa vifo na kupunguza idadi ya wagonjwa 11000 ambao wanazaliwa na ugonjwa huo nchini kila mwaka.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amezindua huduma ya upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa Selimundu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa.

Majaliwa amezindua huduma hiyo leo ambayo Tanzania itakuwa ya kwanza katika Ukanda wa nchi za Mashariki na kati huku ikiwa ya saba kwa nchi za Afrika.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Mei 10, 2023 Majaliwa amesema Serikali imewekeza Sh2.7 bilioni kuanzisha huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Majaliwa amesema Wizara ya Afya iweke utaratibu wa kupima selimundu kwa watoto wanaozaliwa ili wapate matibabu mapema.

Amesema huduma hiyo inafanya hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa hospitali ya pili nchini kutoa huduma ya upandikizaji uloto ikitanguliwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilianza upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa saratani ya damu.

“Huduma hii ni muhimu kwani inaleta nafuu Kwa wagonjwa wanaopata maumivu mara kwa mara kwani itawafanya kuweza kushiriki shughuli mbalimbali na kupunguza gharama kwa Serikali kuwahudumia wagonjwa hao nje ya nchi” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dk Alphonce Chandika amesema huduma hiyo itasaidia nchi kupunguza idadi ya wananchi wanaoishi na selimundu ambao asilimia 50 hadi 90 huwa katika hatari ya kufariki kabla kutimiza miaka mitano.

Chandika alisema Tanzania inakabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu ambapo inashika nafasi ya nne Duniani na takriban watoto 11000 huzaliwa na ugonjwa wa selimundu Kila mwaka.

“Tumeendelea kufanya juhudi za kuanzisha huduma nyingine za kibingwa na bobezi, ninayo furaha kuufahamisha umma wa Tanzania na nchi jirani kuwa kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kutoa huduma ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell) nchini,” amesema Chandika.

Aidha huduma hiyo tayari imetolewa kwa awamu ya kwanza kuanzia katikati ya Januari 2023 na kupandikiza watoto watatu ambao wanaendelea vizuri na kuruhusiwa kwenda nyumbani ambapo watakuwa kwenye uangalizi kama wagonjwa wa nje (out patients).

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kati ya watoto 11000 wanaozaliwa na ugonjwa wa selimundu ni watoto 6000 pekee ndio wanahudhuria huduma za kliniki hivyo kuna idadi kubwa ya wagonjwa waliopo mtaani na wanaendelea kuugua au kufariki.

Ummy amesema jana alikutana na Waziri wa fedha kuangalia namna watakavyoweza kusaidia matibabu ya watoto 40 waliopo kwenye foleni ya matibabu huku akisema 20 wataanza kupata huduma kwa msaada wa Serikali.

Gharama za upandikizaji wa uroto kwa wagonjwa wa Seelimundu zinatajwa kuwa kati ya Sh50 hadi 55 milioni kwa mgonjwa mmoja nchini wakati nje ya nchi, matibabu hayo hupatikana kwa gharama ya kati ya Sh120 hadi 150 milioni