Hukumu rufaa Dk Pima, wenzake yaahirishwa
Muktasari:
- Jana Januari 18, 2024 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ilipanga kutoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wawili wanaopinga kuhukumumiwa miaka 20 jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha
Arusha. Hukumu ya Rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wawili, iliyokuwa itolewe jana imeahirishwa hadi Februari 9, 2024.
Agosti 31, 2023, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, Serafini Nsana aliwahukumu kifungo cha miaka 20 jela Dk Pima, aliyekuwa Mweka hazina wa Jiji la Arusha, Mariam Mshana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji, Innocent Maduhu.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2023, washitakiwa walikuwa wakikabiliwa na makosa tisa ikiwamo utakatishaji wa Sh103 milioni.
Hata hivyo, Dk Pima na wenzake hawakuridhishwa na hukumu hiyo na walikata rufaa hiyo ambayo ilisikilizwa mwishoni mwa mwaka jana na Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Jana Alhamisi Januari 18, 2024, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mariam Mchomba, aliahirisha kusomwa kwa hukumu hiyo akisema bado haijakamilika kuandikwa.
Amesema rufaa hiyo ilipangwa kwa ajili ya hukumu ila kutokana na kutokukamilika kuandikwa, inaahirishwa hadi Februari 9, 2024.
Katika rufaa hiyo, waomba rufaa walikuwa na sababu saba ikiwemo Mahakama iliyomfunga haikuwa na mamlaka kwa sababu hakukuwa na ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kumshitaki mteule wa Rais.
Nyingine wanadai kuwa kesi hiyo haikuwa imethibitishwa kupita kiwango cha mashaka, na Hakimu kushindwa kuchambua ushahidi ipasavyo na makosa mengine hayakuthibitika.
Awali Mei 24, 2022 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi watumishi sita wa Halmashauri ya jiji la Arusha akiwemo Dk Pima ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mbali na kesi hiyo akina Dk Pima wanakabiliwa na kesi nyingine mbili, ambapo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2022 watuhumiwa ni Dk Pima, Mariam, Maduhu na Nuru Ginana (aliyekuwa mchumi), wakikabiliwa na makosa manne ikiwemo ufujaji na ubadhirifu na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Katika kesi nyingine ya uhujumu uchumi namba 4/2022 watuhumiwa ni Dk Pima, Mariam, Maduhu na Alex Daniel, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na makosa manne likiwamo ufujaji, ubadhirifu na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Katika kesi hizo mbili watuhumiwa walishasomewa maelezo ya awali na zinasubiri kukamilika kusikilizwa kwa kesi namba 5/2022, ndipo zianze kusikilizwa.