Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya kina Dk Pima yapangiwa utaratibu, tarehe kuanza kusikilizwa

Muktasari:

Leo Mahakama ya Hakimu Mkazi ilipanga kutaja kesi mbili kati ya tatu zinazowakabili ambapo zilipangiwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Novemba 8 hadi 10, 2022.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga utaratibu mpya wa kuanza kusikiliza kesi tatu za uhujumu uchumi zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wanne.

Mbali na Dk Pima watuhumiwa wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Fedha katika halmashauri hiyo, Mariam Mshana, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango na uchumi, Innocent Maduhu, Alex Daniel na Nuru Ginana (aliyekuwa mchumi).

Mahakama hiyo imepanga Novemba 9, 2022 kuanza kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2022 inayomkabili Dk Pima, Mariam na Maduhu kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.

Leo Alhamisi Novemba 3, 2022 mahakama hiyo ilipanga kutaja kesi mbili kati ya tatu zinazowakabili watuhumiwa hao ambapo awali ziliahirishwa Oktoba 20, 2022 na mahakama hiyo ilipanga kuanza kuzisikiliza kesi hizo kwa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 8 hadi 10.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule huku utetezi ukiwakilishwa na Wakili Sabato Ngogo.

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2022 inayomkabili Dk Pima, Mariam, Maduhu na Ginana, Wakili Janeth aliieleza mahakama kuwa shauri hilo limepangwa leo kwa ajili ya kutajwa na lilishapangiwa kuanza kusikilizwa kuanzia Novemba 8, mwaka huu hivyo wanaomba waendelee na tarehe hiyo.

Hakimu Mbelwa amesema licha ya mara ya mwisho shauri hilo kupangiwa tarehe za kuanza kusikilizwa, kwa kuwa mashauri yote matatu yanahusisha watuhumiwa watatu kati ya hao watano, ni lazima kesi hizo zipishane kwenye usikilizwaji.

“Mara ya mwisho tulipanga kama alivyoeleza wakili wa Serikali leo tulipanga kuanza kusikiliza mfululizo ila kwa bahati mbaya watuhumiwa ni wale wale kasoro wawili, kwa hiyo hatuwezi kusikiliza zote kwa wakati mmoja, inabidi tukubaliane kesi lazima zipishane ianze moja zifate nyingine,”

Hakimu huyo amesema kesi hiyo itakuwa ya tatu kusikilizwa ambapo itaanza kusikilizwa Disemba 2, 2022.

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 4/2022 inayowakabili Dk Pima, Mariam, Maduhu na Daniel, Wakili Janeth aliieleza mahakama kuwa nayo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na ilishapangiwa tarehe za kusikiliza.

Hakimu Mbelwa alieleza kuwa mazingira ya kesi hiyo yanafanana na kesi ya awali, hivyo nayo itasubiri na badala ya kuanza kusikilizwa mfululizo Novemba 8 hadi 10 itaanza kusikilizwa Novemba 21, 2022.

Katika kesi hizo mbili namba 3 na 4 watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa nane ambayo ni ufujaji na ubadhirifu na matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.

Hakimu Mbelwa alieleza kuwa kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2022, inayomkabili Dk Pima, Mshana na Maduhu ambayo haikupangwa leo, ndiyo itakayokuwa ya kwanza kuanza kusikilizwa Novemba 9, 2022 ambapo katika kesi hiyo watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ikiwemo kosa la utakatishaji fedha Sh103 milioni.