Huu hapa ujumbe wa Pasaka wa viongozi wa dini, waamini

Muktasari:

  • Watoto wataka mwenendo mzuri wa wazazi ndani ya familia kama nguzo imara ya malezi bora kwao.

Handeni/Mikoani. Baadhi ya viongozi wa dini na waamini wameadhimisha sikukuu ya Pasaka wakiitaka jamii kudumisha amani ndani ya familia, kwani isipokuwepo ni chanzo cha matukio ya ukatili wa kijinsia na mauaji.

Akihubiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Handeni, Mchungaji wa kanisa hilo na mkuu wa Jimbo la Magharibi, Ismail Ngoda leo Machi 31, 2024 amesema amani inatakiwa kuwepo katika ngazi zote, ili kuzuia uhalifu.

Amesema watu wanatakiwa kuepuka mambo yanayoweza kuleta uvunjivu wa amani katika familia, kwani kwa sasa wanaume na wanawake wote wamekuwa wakifanya ukatili kwa nyakati tofauti, sababu kubwa ni kukosekana amani katika mioyo na familia zao.

Mchungaji Ngoda amesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakifanya ukatili kwa wanaume zao, chanzo cha yote ni kukosekana kwa amani na imani kwa watu.

"Yesu ameleta amani, ujumbe wa amani uendelezwe mahali pote ili nchi yetu na ulimwengu kwa ujumla pawe mahali pa amani, ujumbe wa Yesu alipofufuka ni amani kwa watu wote kwa kusema amani iwe nawe. Ni amani kwa familia, ndoa na kila mtu," amesema.

Muumini wa kanisa hilo, Elihaika Mfuko, amesema chanzo cha machafuko katika jamiii ni kukosekana uvumilivu kwenye ndoa na jamii kwa ujumla.

Amesema hakuna uaminifu katika ndoa, kila mmoja hamuamini mwenzake.

Mfuko ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema hali hiyo imekuwa na madhara mengi, ikiwemo kuwepo watoto wa mitaani ambao wana wazazi, ila kutokana na kukosekana amani ya ndoa, wazazi waliachana na kuacha watoto wakiteseka, hivyo ni wakati wa familia kuona umuhimu wa kuitunza amani.

Henry Mbise, amesema kutokumfahamu Mungu na watu kuacha kuabudu ndiyo chanzo cha machafuko yote.

Kutoka Njombe

Waamini wametakiwa kuendeleza mema waliyokuwa wakiyatenda katika kipindi cha Kwaresima kwa kufunga, kusali na kuwasaidia watu wenye uhitaji kama njia mojawapo ya kumpendeza Mungu.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Eusebio Kyando amesema kipindi cha Kwaresima waumini walitumia muda huo kujiandaa na maadhimisho ya Pasaka kwa kufundishwa kufunga, kusali na kuwasaidia wahitaji.

Amesema hayo yalikuwa mazoezi kwa ajili ya kujenga tabia na mwenendo mzuri wa kumpendeza Mwenyezi Mungu.

"Maana yake Pasaka kama mwanga na nuru kama tunavyoimba sisi Wakatoliki katika mbiu ya Pasaka tunatangaza kwamba sasa tupo tayari kuanza maisha mapya ya amani, mwanga na mapendo; maisha ya kujenga amani katika familia, jamii na katika ujirani wetu," amesema Kyando.

Anglikana Kibaha

Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Gabriel, Kibaha, Exavia Mpambichile amesema maadhimisho ya Pasaka kwa Wakristo yanapaswa kuwa kwa vitendo na si kuishia kwenye maneno pekee.

Amesema hayo leo Machi 31, 2024 wakati wa mahubiri kwenye ibada ya Pasaka kanisani hapo.

Amesema dhamira ya Wakristo kuadhinisha sikukuu hiyo ni kutafakari mienendo ya maisha wanayoishi, ili yaendane na kanuni za Kristo wanayomkumbuka.

"Tunaposema Yesu amefufuka lazima tuangalie mambo kadhaa, ikiwemo kujitenga na vitendo vya nguvu za giza, matendo yote ya dhambi na kuendeleza utu wema," amesema.

Mpambichile amesema ni vema Wakristo wakatafakari juu ya mwenendo wa maisha yao kama wanaenenda kwa kufuta kanuni za Mungu, ili kuwa kielelezo kwa wengine.

"Kujitafakari ni kuangalia namna unavyoishi kivitendo na kuwa na mwelekeo mmoja si leo uko kanisani, kesho uko maeneo yanayohusika na nguvu za giza, hapo hakuna unachokifanya zaidi ya kupoteza muda ndani ya nyumba za ibada," amesema.

Muumini wa kanisa hilo, Rukia Charles amesema wakati wa kuadhimisha Pasaka ni vema kutoa sadaka kwa watu wenye mahitaji maalumu na si kusherehekea nyumbani au maeneo ya starehe pekee.

"Kuna watu walio kwenye makundi maalumu wanahitaji kusaidiwa kwa mambo mbalimbali, ikiwemo chakula na hata mavazi," amesema.

Malezi bora

Kwa upande wao, wanafunzi wa shule ya Jumapili kanisani hapo wamesema mwenendo mzuri wa wazazi ndani ya familia ni nguzo imara ya malezi bora kwa watoto.

"Waendeleze upendo walionao kwao na hata kwetu watoto wao na pale tunakokwenda kinyume wasituhurumie, bali watuonye ili tukiwa na umri wa utu uzima tuwe kwenye mwenendo mzuri," amesema Adriano Mbio.

Amesema ili kudhihirisha hilo, kuna umuhimu wa wao kuwa makini na watoto wakati wowote hasa pale wanapoona mabadiliko ya mwenendo wao na kuchukua hatua kwa wakati.

Emmanuel Thawe, amesema matunzo ni moja ya kinga ya watoto kutojiingiza kwenye vitendo vya ombaomba vinavyoweza kuwayumbisha na kujikuta kwenye wakati mgumu.

"Matunzo kadri ya uwezo walionao ni muhimu kwetu na pia wasitukataze kujifunza mambo mazuri hasa mafundisho ya kanisa," amesema.

Rosemary Victor, amesema ingawa elimu ya shule za msingi ni muhimu kwa watoto, lakini suala la maadili linapaswa kuwekewa mkazo kwa watoto ili kupata kizazi bora cha baadaye.

Mkoani Kigoma

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, Joseph Mlola amesema ni vema kila muumini akawa na maisha ya toba kila siku ya maisha yake kwa kuendeleza waliyoyaishi wakati wa kwaresima.

“Maisha tuliyoishi katika siku 40 za Kwaresima ndiyo yawe maisha yetu ya kila siku kwa kuacha dhambi, kujitenga na uovu, tuishi maisha matakatifu na kutenda mema,” amesema.

Askofu Mlola amesema Yesu Kristo anapofufuka kwao na wao wasikubali kubaki kaburini, bali wanatumwa kuwa mashahidi kwa maisha wanayoishi na maneno yao kuutangaza ukweli huo.

Baadhi ya waamini wamesema Pasaka inawakumbusha ufufuko wa Yesu Kristo ni ushindi kwao, ili wawe huru na mbali na dhambi.

Maria Ibrahimu, amesema wanatumia sikukuu hiyo kutafakari kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo kuwa kama ishara ya upendo kwao, kwani aliwafia kwa ajili ya dhambi zao.

Jacob Mussa, amesema ni kipindi cha kukaa na familia na kusaidia wengine wasionacho na si kufanya matendo yasiyofaa katika jamii.

Imeandikwa na Rajabu Athumani, Seif Jumanne, Sanjito Msafiri na Happiness Tesha