Huyu ndiye Dk Bashiru Ally

Huyu ndiye Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo yaliyoibua mjadala ni uteuzi wa aliyekuwa katibu mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally kuwa balozi na katibu mkuu kiongozi.

Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo yaliyoibua mjadala ni uteuzi wa aliyekuwa katibu mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally kuwa balozi na katibu mkuu kiongozi.

Ni uteuzi ambao haukutarajiwa uliokwenda sambamba na msomi huyo kuteuliwa kuwa balozi, wengi wanajadili uzoefu wake wakiamini anaweza kuitumikia vyema nafasi hiyo.

Uteuzi wa Dk Bashiru ulitangazwa jana Ijumaa Februari 26, 2021 na mapema leo Rais John Magufuli amemuapisha kwa mujibu wa katiba ya nchi  na kuanza kutumikia upya wadhifa wake huo mpya.

Dk Bashiru Ally alizaliwa Januari mosi, 1968 katika Wilaya ya Bukoba vijijini Mkoa wa Kagera na kupata elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Katerero wilayani humo kati ya mwaka 1980-86.

Mwaka 1987 alijiunga na shule ya sekondari ya Kilosa mkoani Morogoro alikosoma kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka 1990 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Ihungo iliyopo Bukoba alikosoma kidato cha tano na sita na kumaliza mwaka 1993.

#Live: Kuapishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Bashiru Ally

Mwaka 1997/98 alijiunga na Chuo kikuu cha Dar es salaam akisomea shahada ya kwanza sayansi ya siasa na kumaliza mwaka 2000 ambapo aliunganisha na kusoma shahada ya uzamili aliyomaliza mwaka 2002.

Mwaka 2003 aliajiriwa na taasisi ya Haki Elimu lakini mwaka huohuo alihamia Chuo kikuu cha Mzumbe ambako alifundisha kwa mwaka mmoja kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kama mhadhiri msaidizi.

Akiwa chuoni hapo aliendelea na kusoma akichukua shahada ya uzamivu kuanzia mwaka 2011 hadi 2015.

Amewahi kuwa makamu mwenyekiti na kaimu mwenyekiti wa Chama cha kitaaluma cha UDSM (Udasa), makamu Mwenyekiti wa chama cha wanataaluma nchini.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Mei, 2018 Dk Bashiru akiwa mhadhiri mwandamizi katika idara ya sayansi ya siasa UDSM vilevile  alikuwa akiongoza kurugenzi ya mijadala na makongamano.

Ni mtafiti na mwandishi wa makala mbalimbali zilizochapishwa kwenye matoleo ya machapisho mbalimbali na kiitikadi amejipambanua kama mjamaa na mfuasi wa sera za hayati Mwalimu Julius Nyerere hata kabla ya kuweka wazi kuwa yeye ni mwanaCCM.

Kuhusu familia Dk Bashiru alioa kabla hata hajaanza kusoma chuo kikuu mwaka 1994. Yeye na mkewe Zulaika Hashim walijaliwa kupata watoto wawili wa kike, Halima na Hasanat.