Ijue historia siku ya Valentine, vijana wafunguka wanavyoadhimisha

Muktasari:

  • Sikukuu ya wapendanao imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka duniani kote, huku vijana wakiwa mstari wa mbele, kwa bahati mbaya wengi wao hawana uelewa mpana kuhusu siku yenyewe.

Dar es Salaam.  Ikiwa imesalia siku moja kabla ya Februari 14 ambayo huadhimishwa siku ya wapendanao, maarufu kama “Valentine Day”, baadhi ya watu wamekuwa na desturi ya  kusherehekea kwa kupeana zawadi mbalimbali ikiwemo maua na kadi.

Tofauti na kupeana zawadi hizo, inaelezwa watu wengine huitumia siku hiyo kinyume na dhima yake halisi, kwani wapo wanaoitumia  kufanya ngono/uzinzi, bila kujua historia ya siku hiyo ilitoka kwa mtu aliyepinga dhambi ya uzinifu.

Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya historia ya www.countryliving.com, wakati wa karne ya tano kulikuwa na kiongozi aliyeitwa Mfalme Claudius II ambaye aliamini askari anapooa hawi mkakamavu na pia muda mwingi anawaza kuhusu familia yake, zaidi ya kitu kingine chochote.

Hivyo, alipiga marufuku ndoa kwa askari. Kitendo hicho hakikuwafurahisha watu wengi, akiwamo Padri Valentino. Kiongozi huyo wa kidini aliendelea kufungisha ndoa kwa siri.

Mfalme Claudius alipopata habari hizo aliamuru Padri Valentino akamatwe na kuuawa.

Mtakatifu Valentino aliuawa Februari 14, ndiyo maana ikatangazwa rasmi kuadhimishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama baba wa upendo na mtetezi wa wanandoa. Historia inaonyesha kuwa aliyetangaza kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius.

Pia, ipo simulizi nyingine inayosema akiwa gerezani kwa amri ya Mfalme Claudius, Padri Valentino aliandika barua iliyokuwa na salamu kwa binti aliyekwenda kumsalimia gerezani, mwisho wa barua alihitimisha kwa kusema ‘Kutoka kwa Valentino wako’. Tangu hapo, Valentino anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake huadhimishwa ulimwenguni kote.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, baadaye, Padri Valentino alikuja kutangazwa kuwa Mtakatifu.

Vijana wanavyosherehekea

Vijana wametoa maoni tofauti kuhusu siku hii wakieleza namna wanavyoielewa, kwani siku hiyo hutawaliwa na mambo makubwa ambayo ni kupeana zawadi, mitoko ya usiku na kuonyeshana upendo kwa namna mbalimbali.

Mkazi wa Tabata, Alex Kamanga amesema amewahi kusherehekea siku ya Valentine kwa kwenda na mpenzi wake kwenye mgahawa kupata kinywaji na chakula cha jioni, huku wakizungumzia safari ya penzi lao.

Amesema anaitambua Valentine kama siku ya wapendanao na ndiyo siku ambayo mwanamume na mwanamke wanapaswa kuonyeshana upendo zaidi ya siku nyingine ndani ya mwaka mzima.

“Katika maisha yangu ya mahusiano, niliwahi kusherehekea sikukuu ya Valentine kutokana na msukumo kutoka kwa mpenzi wangu, tulikuwa tunakwenda sehemu kula chakula cha jioni na kujadiliana namna ya kuboresha penzi.

“Wanawake ndiyo wanaichukulia serious sana kama siku ya kuadhimisha upendo, lakini sisi wanaume tunaona kawaida tu. Tunaadhimisha kuwaridhisha wapenzi wetu,” amesema kijana huyo.

Kwa upande wake, Diana Lamson amesema kwake Valentine ni siku ya zawadi na anatarajia kupokea zwadi kutoka kwa mpenzi wake kama ishara ya upendo kwake. Hata hivyo, anasema yeye hana kawaida ya kumpa zawadi, bali anapokea.

“Sisi tunaadhimisha siku ya Valentine kwa kupena zawadi, natarajia hata kesho ataniletea zawadi. Huwa nafurahi sana nikipata zawadi na hiyo inanionyesha kwamba ananipenda,” amesema msichana huyo.

Hata hivyo, Flora Sixtus amekuwa na mtazamo tofauti akieleza kwake haoni tofauti kati ya siku ya wapendanao na siku nyingine, wao wanaonyeshana upendo kila siku na wakati watakapojisikia.

“Upendo wa kweli hausubiri siku ya Valentine, sisi tunapendana kila siku na hii Valentine tunaiona ya kawaida kwa sababu ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku,” ameeleza mwanamke huyo, mkazi wa Mabibo.