Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ILO yaahidi kuendelea kuimarisha haki za kazi Tanzania

Muktasari:

  • Jaji Yose Mlyambina, amestaafu na kuagwa rasmi katika utumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Dar es Salaam. Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeahidi kuendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha mfumo wa haki za kazi nchini, likisisitiza umuhimu wa taasisi imara zinazoweza kutoa haki kwa wafanyakazi na waajiri kwa wakati na kwa ufanisi.

Ahadi hiyo imetolewa wakati wa hafla ya kumuaga Jaji Yose Mlyambina aliyekuwa akisimamia Divisheni ya Kazi ya Mahakama Kuu ya Tanzania na kumkaribisha Jaji Ntemi Kerekamajenga anayechukua nafasi hiyo.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa ILO Kazi House, Dar es Salaam, iliwakutanisha wawakilishi wa Mahakama, Serikali, vyama vya wafanyakazi, waajiri, wanasheria, washirika wa maendeleo pamoja na viongozi wa ILO.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO inayohudumia Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Caroline Mugalla, amesema mfumo madhubuti wa haki za kazi ni msingi muhimu wa kuendeleza ajira zenye staha na haki za kijamii.

Amesema ushirikiano kati ya ILO na Mahakama ya Tanzania umechangia kuongeza upatikanaji wa haki, kuimarisha heshima kwa haki za wafanyakazi na kujenga taasisi zenye uwezo wa kushughulikia migogoro ya kikazi kwa ufanisi.

“Mfumo wenye ufanisi wa haki za kazi ni nguzo muhimu katika kuendeleza ajira zenye staha na haki za kijamii. ILO inathamini ushirikiano wake wa muda mrefu na Mahakama ya Tanzania ambao umeimarisha upatikanaji wa haki na taasisi za soko la ajira,” amesema Mugalla.

Aidha, amempongeza Jaji Mlyambina kwa mchango wake katika kuimarisha sheria na maamuzi ya kazi nchini, akibainisha kuwa katika kipindi chake kulikuwa na mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa kwa ushirikiano na ILO.

Miongoni mwa mafanikio hayo, amesema ni uchapishaji wa maamuzi ya kesi za Divisheni ya Kazi ya Mahakama Kuu pamoja na programu za kuwajengea uwezo majaji na wadau wengine wa sekta ya sheria.

Ameeleza hatua hiyo ilisaidia kuongeza ubadilishanaji wa maarifa na kuimarisha uwiano katika utoaji wa maamuzi ya migogoro ya kazi.

Aidha, amemkaribisha Jaji Kerekamajenga katika nafasi yake mpya na kueleza utayari wake wa kuendelea kushirikiana na Mahakama katika kuimarisha upatikanaji wa haki za kazi, uwezo wa taasisi na utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya kazi.