Iundwe tume kurejesha umoja na mshikamano nchini

Saturday April 03 2021
By Mussa Juma

Tangu kutangazwa kifo cha Rais wa tano, John Magufuli, Machi 17 na kuapishwa kwa Rais wa sita, Samia Suluhu Hassan na kutoa hotuba yake ya kwanza akiwa Rais, mwanga mpya wa Tanzania ijayo unaonekana.

Kauli za Rais Samia kuwataka Watanzania kuwa wamoja kama Taifa, kufarijiana, kuonyesha upendo, undugu na kudumisha amani zimefungua ukarasa mpya.

Rais Samia pia kutoa kauli kuwa sasa si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini, siyo wakati wa kutazama yaliyopita, bali kutazama yajayo kunaleta faraja katika Taifa.

Hotuba yake hiyo Rais Samia kusema wakati huu si wa kunyoosheana vidole, bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, inaonyesha neema zaidi katika taifa hili.

Hata katika mazishi ya Magufuli wilayani Chato, Machi 26, Rais Samia aliendelea kusisitiza umoja na mshikamano kwa Watanzania, jambo ambalo linaonyesha dhamira yake njema kuwaunganisha Watanzania wote.

Kauli hizi za Rais na hata baadhi ya viongozi wa dini na wastaafu, zinaonyesha taswira mpya ya Tanzania ambayo inakwenda kuondoa mgawanyiko ulioanza kujitokeza kutokana na tofauti za kiitikadi.

Advertisement

Pia kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James kuomba radhi kwa kauli zake na vijana wengine wa CCM, wakati wa harakati za kisiasa ni jambo linaloendelea kufungua ukurasa mpya wa Tanzania.

Mwenyekiti wa UVCCM, James ameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa, kukiri makosa na kutaka kusahau yaliyopita na kusonga mbele kama alivyosema Rais Samia.

Hata hivyo, mambo haya ili yaende vizuri na kuratibiwa vema na kuchukuwa tahadhari ya kutorejea nyuma ni muhimu kuundwa kwa tume ya maridhiano. Tume hii itawakutanisha wanasiasa wa vyama vyote, wafanyabiashara, Serikali na watu wengine kujadili mustakabali mpya wa Taifa na kusahau tofauti zetu.

Wale waliokimbia nchi kwa sababu mbalimbali warudi nchini, kushirikiana na Serikali kuijenga Tanzania yao.

Kauli za maridhiano na kutorejea kule tulipojikwaa zinapaswa kutamalaki katika vyombo vyote vya dola, vyama vyote vya siasa, jumuiya ya wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi na katika asasi za kiraia.

Waswahili walisema mficha maradhi mauti humuumbua, hivyo ni vema kabla ya kuendelea kuumbuana kuwepo na maridhiano ya kweli katika jamii.

Lakini pia maridhiano yanapaswa kuonekana wazi hata katika vyombo vya habari kwa kurejeshewa uhuru wao wa kufanya kazi kwa weledi na kulisaidia taifa kufikia malengo yake, hasa ya kuchochea maisha bora kwa wananachi.

Hivyo, nirejee mtazamo wa wadau mbalimbali kuwa ni muhimu sasa kuundwa tume ya maridhiano, ili kuzika tofauti zote katika jamii na watu wafanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na Katiba ya nchi.

Ni ukweli ulio wazi uchaguzi mkuu uliopita ulichangia kuibua mpasuko katika jamii, lakini pia matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea yalikuwa hayana afya kwa taifa.

Hata hivyo, ni muhimu kuendelea kumuenzi Rais John Magufuli kwa kuendeleza miradi mikubwa inayoendelea kwa kupata maridhiano ya pamoja juu ya utekelezwaji wake.

Hakuna aliyewahi kujitokeza kupinga miradi hiyo inayoendelea nchini, lakini kulikuwa na maoni tofauti katika njia zinazotumika katika uendelezaji wa miradi hiyo.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ambavyo zilikuwa ndoto za hayati, Rais Magufuli.

Tunaweza kuendelea na hali iliyopo sasa, lakini nionavyo haina afya, kwani bado kuna mpasuko katika jamii.

Lakini Tanzania ina bahati kubwa kuwepo hadi sasa marais wastaafu ambao bado wanaheshimika na wanasiasa wote na Watanzania ambao wanaweza kushauri jambo na likakubaliwa na pande zote.

Watanzania wengi bado wanataka kuendelezwa kwa amani, utulivu, kuvumiliana na kuheshimiana miongoni mwa wanasiasa, ili kuenzi umoja na mshikamano katika taifa hili ulioachwa na waasisi hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume.

Itoshe kushauri kuundwa kwa tume ya maridhiano itakayokaa na kusikiliza pande zote katika jamii na kutoa ushauri kwa Serikali, ili ambayo yanaweza kurekebishwa yarekebishwe na wadau wote washikane mikono na kusonga mbele.


Mussa Juma ni mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi 0754296503.

Advertisement