Jaji mkuu wa Tanzania awaonya mahakimu wanaochelewesha kesi

Friday November 27 2020
jajimkuupic
By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewaonya mahakimu wanaochelewesha kesi bila sababu ya msingi na kuwataka kutumia mamlaka yao ya kikatiba kuhakikisha zinasikilizwa na kutolewa uamuzi kwa wakati.

Profesa Juma amesema hayo leo Ijumaa Novemba 27, 2020 wakati akiwaapisha mahakimu wakazi 39 wa mahakama za mwanzo na wilaya.

“Kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi bila sababu hasa za mauaji, ugaidi, utakatishaji fedha, dawa za kulevya, nyara za Serikali na kesi za uhujumu uchumi.”

“Wananchi wanalalamika sana na wanayo sababu ya kulalamika hasa katika mahakama za Wilaya na Mahakama za hakimu mkazi,” amesema Profesa Juma.

Amewataka mahakimu kutofanya kosa la kukubali kuahirisha kesi bila kupokea sababu za msingi.

“Uhakimu wako utaimarika endapo siku zote utazingatia sheria ukiongozwa na taratibu, kanuni na nyaraka zinazotolewa mara kwa mara na viongozi wa mahakama.”

Advertisement

“Hivyo basi, uhuru wenu katika maamuzi ni maagizo ya kujenga demokrasia na utawala wa sheria. Uhuru wa mahakama na uhuru wa hakimu ni kwa faida ya nchi kwa ujumla, na sio kwa faida au utashi wa Hakimu au Jaji husika,” amesema.

Jaji huyo amewaonya mahakimu hao wapya, kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri simu zao za mikoani ili kuepuka kuingilia uhuru wao na wajiepushe kupokea shinikizo kupitia simu za mkononi.

“Chungeni sana simu zenu za mkononi maana hizi zinaweza kutumika kuingilia uhuru wenu katika kufikia maamuzi yenu. Kwa ufupi, usipokee shinikizo kupitia simu za mkononi” amesema.

Amesema, “vishawishi visivyotakiwa vinaweza kutoka kwa ndugu, familia, marafiki, majirani, kiongozi wa kiroho na wengine ni lazima muangalie upya zawadi mbalimbali mnazopewa kutoka kwa marafiki, misaada, mahusiano, wapi mnatembelea, makundi gani ya starehe au mapumziko mnayoshiriki pamoja na hata picha mnapiga..., Mnapiga picha na nani.”

“tambueni shinikizo au ushawishi usiotakiwa unaweza kukufikia kupitia makundi ya mitandao ya kijamii.”

Amesema  yapo malalamiko ya mahakimu kutembelewa katika ofisi zao na marafiki, ndugu na  jamaa wakati wakijitayarisha kuanza mashauri akitaka wageni wote kuacha shida zao kwa hakimu mfawidhi au watendaji wa mahakama.

“Unaweza kuwa hakimu unayefahamu sana sheria na taratibu za kisheria na za mahakama lakini bila uadilifu, umahiri wako unaweza kutumika kuzorotesha au kupoteza haki halali za wengine, hivyo suala la uadilifu limepewa uzito mkubwa katika kanuni za maadili za maofisa mahakama,” amesema na kuongeza

Pia aliwaonya baadhi ya maofisa wa mahakama kujiunga katika makundi ya mitandao ya kijamii ambayo hayana maadili huku wengine wakitumia majina bandia katika mitandao  hiyo  kushiriki majadiliano ambayo hayaendani na maadili yao.


Advertisement