Jaji Mutungi: Katiba haitatekwa na wanasiasa

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Dar es Salaam. Siku tano zilizopita, Baraza la Vyama vya Siasa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi lilikutana jijini Dar es Salaam kujadili hatua za mwanzo za utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilotoa Mei 6 mwaka huu, baada ya tangazo la kuanza mchakato wa Katiba Mpya.
Rais Samia alimtaka Jaji Mutungi kuitisha mkutano unaotoa fursa kwa wanasiasa kufanya tathimini ya hoja na mapendekezo ya Kikosi Kazi, ikiwemo suala la mchakato wa Katiba mpya.
Jaji Mutungi anakabidhiwa jukumu hilo kwa wanasiasa waliokuwa chanzo cha mkwamo wa kuendelea mchango wa Katiba mwaka 2014 kupitia Bunge Maalumu la Katiba, huku wananchi wakibakia njiapanda. Rasimu ya pili ya Jaji Warioba ndiyo ilipasua Taifa vipande viwili kupitia mitazamo ya muundo wa Serikali.
Kutokana na changamoto hizo, gazeti la Mwananchi limefanya mahojiano na Jaji Mutungi kufahamu namna gani anaweza kufanikisha mchakato huo ili kufanikisha ndoto za Rais Samia na rekodi ya Watanzania kutengeneza Katiba yao.
“Ofisi yangu ipo kwenye hatua za mwisho kutekeleza maagizo ya Rais Samia kupitia baraza hilo, Rais anapotoa maagizo ya utekelezaji wa jambo hilo ni lazima utaratibu ufuatwe, kwa hiyo katika hatua za kufanikisha kazi hiyo wananchi wasije wakadhani mchakato unahusisha wanasiasa pekee.
“Umma unapaswa kuelewa kitu kimoja, Rais ameonyesha dhamira yake kwamba Serikali ipo pamoja na takwa la wananchi kuhusu upatikanaji wa katiba mpya. Pili, hitaji hili lilionekana hata katika kukusanya maoni ya kikosi kazi, wadau walizungumzia mengi, ikiwemo kuhusiana na mchakato wa Katiba mpya.
“Pia, wananchi suala la maridhiano linaloendelea kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lina umuhimu wake, katika hili wasipuuze. Niwahakikishie mkutano wa wadau utabeba ajenda ya Rais ya mchakato wa Katiba mpya na tutakusanya maoni yao.”
Mwandishi: Je, ni kwa namna gani mkutano huo utaondoa wasiwasi kwa wananchi kuhusu ajenda ya Katiba kumilikiwa na wanasiasa?
Jaji Mutungi: Mkutano huo utakuwa shirikishi kwa watu wote. Tusisahau kwamba vyama vya siasa ni taasisi za umma, kwa hiyo wao pia ni sehemu ya makundi na wanayo haki hiyo, lakini niwatoe hofu baadhi ya wananchi wanaodhania kwamba mchakato huo umeshaporwa na wanasiasa.
Si kweli na wala wasiwe na wasiwasi, Serikali haina nia ya kurudisha mchakato kwa wanasiasa na wanasiasa ambao hawaelewi, wanapaswa kujua hivyo mchakato wa Katiba mpya utajumuisha mpaka mtu wa chini wa kawaida.
Mchakato utahusishwa makundi maalumu yote kama ilivyokuwa mchakato wa mwaka 2014. Ninaamini pia mchakato huu tutafanya hivyo.
Tunataka kutengeneza mazingira ya kukutana na watu wote hata wakati mwingine ambao hawajui kuongea vizuri lugha ya Kiswahili.
Hadidu za rejea za mkutano bado hazijaandaliwa, sisi tutaendesha mkutano lakini hadidu zitatengenezwa na mfumo mwingine. Ninaamini makundi yote nchini yatafikiwa katika mchakato mzima. Nasisitiza wananchi wajue hakuna mtu mwenye haki miliki ya Katiba.
Mwandishi: Rais Samia amekuagiza utazame sheria ya vyama vya siasa, ni maeneo gani yanayolalamikiwa zaidi na wanasiasa kwa ajili ya marekebisho?
Jaji Mutungi: Kwanza wanaolalamika marekebisho katika Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 siyo wote wanasiasa na hata ukiangalia wanaoandika kwenye mitandao ya kijamii siyo kwamba wote ni wanasiasa, ila asilimia kubwa ni asasi za kiraia.
Pili, mara nyingi mapendekezo ya sheria yanapofanyika katika taasisi mbalimbali nchini hupelekwa ngazi zinazohusika, ikiwemo Bunge kwa ajili ya kuendelea na utaratibu wake.
Kama sisi huwa tunaitisha vikao vya wadau kama Baraza la vyama vya siasa kupitia na kuboresha au kurekebisha yale mapendekezo.
Baada ya hapo zinapelekwa bungeni. Hadi sasa ofisi yangu haina uhakika na maeneo mengi yanayopigiwa kelele na wadau kutaka yabadilishwe. Kuna wanaotaka madaraka ya msajili yapunguzwe, bado ni mjadala ulioibuka tangu huko nyuma.
Wapo wanaodai ofisi ya msajili haina uhuru, lakini mimi ninaona tunao uhuru na tunajua mipaka yetu kwa kuwa kina uhuru na mipaka yake.
Wengi wanazungumzia uhuru kwa sababu msajili anateuliwa na Rais, wanataka mfumo ubadilishwe awe anateuliwa na wabunge ndiyo atakuwa huru, japo mimi binafsi sijaelewa hoja hiyo, naona ni shida ya mteuliwa husika, hata kama wewe ni mwoga hata kama ukiteuliwa na nani utakuwa mwoga tu.”
Maoni waliyopendekeza namna gani tubadilishe tunayaheshimu, lakini ni muhimu kufuata misingi na utaratibu wakati wa hatua za mapendekezo.
Mwandishi: Ripoti ya CAG imekuwa ikitaja udhaifu wa vyama vya siasa katika matumizi ya fedha za umma, je, kuna hatua zozote umezichukua?
Jaji Mutungi: Katika ripoti hiyo 2021/2022 imeonyesha vyama viwili pekee vimepata hati chafu, ni hatua nzuri ikilinganishwa na ilivyokuwa huko nyuma. Ofisi yangu imekuwa ikichukua hatua, ikiwemo kuitisha vikao na viongozi wa vyama kubadilishana mawazo na kuwaambia kurekebisha dosari.
Makosa mengine yanayopatikana kila anapopita kukagua CAG ni ya kiufundi, kuna wakati wanaweza kupita kukagua risiti siku hiyo wakakuta baadhi bado hazijafikishwa ofisini.
Kinachotokea CAG akitoa ripoti yake unakuta baada ya siku kadhaa risiti zimefika na zinakuwa zimeziba makosa yaliyoonekana.
Sasa wakati huo unakuta ripoti ya CAG imeshasomwa na vyombo vya habari vimeshatoa taarifa, kuna haja ya kuangalia upya jambo hili.
Lakini pili, ukitoa vyama vinavyopata ruzuku kutoka serikalini kuna baadhi havina fedha kabisa, hali inayosababisha kushindwa kujiendesha kwa kuajiri watendaji wenye uwezo husika, ikiwemo uhasibu.
Ndiyo maana kilio cha vyama kwa sasa ni mfumo wa ruzuku ubadilike, kwamba kila chama angalau kipate fungu kidogo kutoka serikalini waweze kujiendesha kiweledi.
Lakini kuna wakati ofisi ya CAG inatembelea na kusaidia vyama kujua maeneo gani wana shida ili kufanyia mabadiliko kwa ajili ya ufanisi katika maendeleo kama taasisi ya umma.
Mwandishi: Kwani ofisi yako haina mfumo wa kufuatilia kila fedha inayoingia na kutumika katika vyama?
Mutungi: Wakati mwingine ni vigumu kufuatilia vyama vinavyopata misaada kutoka nje ya nchi, kama hatujapata taarifa za uhakika kutoka chama husika. Mambo ya fedha yanahusisha zaidi ya taasisi mbili, inawezekana wakati mwingine ofisi yangu inaweza kukosa taarifa na tunapojua huwa tunawaandikia barua watueleze chanzo cha kupata fedha hizo.
“Kwa dalili tu za matumizi tunaamua kufuatilia kuomba maelezo ili kujua ukweli wa fedha walizotumia na wamezipata wapi, kazi hii tumekuwa tukifanya mara kadhaa” alisema.