Jaji Warioba akemea ukabila, udini Tanzania

Wednesday October 13 2021
jajipic

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akizungumza katika kongamano la kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

By Peter Elias

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi na wananchi kukemea masuala ya ukabila, udini, ukanda na uchama kwa sababu yanaweza kuligawa Taifa.

Warioba alisema hayo Dar es Salaam jana katika kongamano la kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Kauli hiyo ya Warioba imekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kusema kumekuwapo na maneno kuwa, anawaadhibu baadhi ya watu kutokana na makabila yao, hata hivyo alisisitiza kuwa, haangalii kabila la mtu bali anaangalia kazi yake.

Jana, Warioba alisema mambo ya ukabila, udini, ukanda na uchama yameanza kurudi nchini, hivyo ni muhimu yakakemewa kama alivyofanya Mwalimu Nyerere ili Taifa liendelee kuwa na umoja.

“Ukabila unaanza kuzungumzwa sana, udini unaanza kuzungumzwa sana, ukanda unazungumzwa sana, uchama unazungumzwa,” alisema Warioba.

“Watanzania wenzangu, tukemee watu wote wanaotaka kuleta mambo ya ukabila, udini, ukanda na uchama, tuwe kitu kimoja, tuilinde amani yetu ambayo Mwalimu Nyerere alituachia.”

Advertisement

Warioba alisema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyewaunganisha wananchi licha ya tofauti zao za makabila, dini na ukanda, pia, alifanikiwa kuwafanya kuwa kitu kimoja na Taifa moja la Tanzania.

Warioba alisema Kiswahili kilikuwa silaha kubwa ya kuliunganisha Taifa na Mwalimu Nyerere aliweka msisitizo kwenye lugha hiyo kwa sababu alitambua ukabila ungechelewesha kupata uhuru.

“Sasa tumefika wakati tunasema sheria zetu ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili, mimi nasema elimu yetu yote itumie Kiswahili,” alisema Jaji Warioba.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku alisema falsafa ya Mwalimu Nyerere ilijikita kwenye mambo mawili ambayo ni usawa kwa binadamu wote na kujitegemea.

Alisema ukiwa kiongozi una wajibu wa kuhakikisha rasilimali za Taifa hili ni mali ya wananchi wote na sharti zitumike kwa usawa badala ya kujilimbikizia mali.

Butiku alisema hilo ndilo jambo alilofanya Mwalimu Nyerere hadi alipofariki dunia.

“Falsafa ya kujitegemea msingi wake ni kwamba kila mtu afanye kazi ili ajitegemee. Usawa maana yake wote tuwe na haki ya kuzifikia rasilimali zilizopo. Mwalimu Nyerere aliyaishi mambo hayo na ndiyo falsafa ya uongozi wake,” alisema Butiku.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula alisema Mwalimu Nyerere alipenda kutumia vikao vya chama kupeleka jambo lake na hilo lilisaidia kulinda amani na umoja wa kitaifa uliopo sasa.

“Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa vikao, mawazo yake mengi aliyapeleka kwenye kamati kuu au halmashauri kuu. Kwa hiyo vikao hujenga undugu,” alisema Mangula ambaye aliwahi kuwa mwalimu katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Pia, alisema umoja wa Tanzania umejengwa na umekuwa ukijengwa na Mwalimu Nyerere tangu alipokuwa akipigania ukombozi wa Taifa hili na miaka saba ya harakati hizo, wananchi waliungana naye.

Advertisement